Shamba ni eneo ambalo mkulima anaweza akalitumia kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji kama vile ufugaji na kilimo kwa lengo la kujipatia chakula na pato.
Hata hivyo, baadhi ya wakulima nchini hawana elimu ya kutosha ya namna bora ya kutunz shamba, hivyo kushindwa kuzalisha mazao bora, mengi na yenye tija.
Bila shamba hakuna uzalishaji na shamba bila utunzaji hakuna uzalishaji pia hivyo utunzaji bora wa shamba na mazingira kwa ujumla ndio silaha muhimu kwa mkulima katika kuzalisha yenye.
Ili kuwa na shamba bora na lenye uzalishaji bora unalenga kutunza mazingira, mimea, wanyama, binadamu na udongo, mkulima ni lazima kufanya yafuatayo;
Tathimini ya awali
Kabla ya mkulima ajanza kuandaa shamba lake, anapaswa kufanya tathimini ya awali kubaini hali ya upatikanaji maji, magugu yaliyopo shambani, wadudu waharibifu na njia bora za kuwadhibiti.
Hatua hii itamwezesha mkulima kufahamu njia sahihi anazopaswa kuzitumia katika utunzaji wa shamba lake kulingana na mazingira ya eneo la shamba lililopo.
Wakati wa uandaaji shamba
Wakati wa uandaaji shamba, mkulima anapaswa kuzingatia kanuni tano muhimu ambazo ni:
- Kutoondoa majani yaliyolimwa shambani ambayo baadae yatatumika kama matandazo kusaidia ardhi kubaki na unyevu wa kutosha.
- Mkulima anatakiwa kutolima shamba lake kwa trekta kusaidia kutunza ardhi kubaki na rutuba kwa sababu kilimo cha trekta kina hamisha tabaka la ardhi yenye rutuba.
- Kuchimba mifereji ya kupitisha maji kama shamba lako lipo katika eneo lenye muinuko kuzuia uharibifu wa mazao nyakati za mvua na mmong’onyoko wa ardhi.
- Kujenga uzio wa kibaiolojia kuzunguka shamba lako kwa kutumia miti ya asili kama milonge, miti miba kisha kuchanganya na miti ya matunda. Uzio huu utasaidia upepo kutoharibu mazao na hakikisha unautunza kama unavyolitunza shamba lako kuzuia kuvamiwa na wadudu waharibifu.
Wakati wa upandaji
- Kuchimba mashimo katika eneo ambalo unataka kupanda mbegu. Hatua hii inamsaidia mkulima kulima katika eneo moja kwa muda mrefu na kutoharibu viumbe hai wengine waliopo ardhini.
- Tumia vipimo maalum wakati wa upandaji kwa kuacha nafasi kutoka shimo moja hadi lingine.
- Hakikisha udongo wako una unyevu wa kutosha kwa kuweka matandazo.
- Shindilia udongo kuondoa hewa wakati wa upandaji.
Wakati wa uvunaji
- Wakati wa kuvuna mkulima anatakiwa kuvuna mazao yake pekee na kuyaacha majani ya mmea ndani ya shamba yatakayotumika kama matandazo kwenye ardhi.
- Mkulima anapaswa kubakisha shambani bila kundoa sehemu ya shina la mmea alilovuna, kubaki kama alama atakayotumia kupanda tena wakati wa msimu wa upandaji na kuendelea kusaidia udongo kubaki wenye rutuba.
Faida kwa mkulima
Faida mbalimbali ambazo mkulima atazipata endapo atazingatia kanuni za utunzaji bora wa shamba ni pamoja na;
- Shamba kuendelea kubaki na rutuba ya kutosha.
- Kumpunguzia mkulima gharama za uandaaji na utunzaji wa shamba.
- Mkulima atapunguza gharama za matumizi ya maji shambani kwa sababu shamba litakuwa na ubichi wa kutosha.
- Itampunguzia mkulima gharama ya ununuzi wa mbolea katika urutubishaji wa ardhi.
- Mkulima atapata mazao bora yenye tija kwa matumizi ya chakula na biashara.
- Kuzuia upepo shambani ambao unaathiri mazao na kuondoa virutibisho vya ardhi.
Muhimu
Mkulima anashauriwa kuzingatia kanuni hizi kwani zitampatia matokeo chanya ikiwemo kupunguza gharama za uandaaji wa shamba msimu mwingine wa kilimo.
Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na Bw. Felician Pius kwa namba za simu 0682030948.