Kuna virutubisho ambavyo ni muhimu kwa ukuaji wa mmea. Upungufu wa mojawapo ya virutubishi hivi muhimu utapunguza ukuaji wa mimea. Mavuno yanategemea kiwango cha virutubisho muhimu kwa mmea vipatikanavyo katika udongo.
Mimea yote hutegemea vitu muhimu kukua vizuri. Vitu hivi vinaweza kugawanywa katika makundi mawili;
- Vitu vya madini, kupitia udongo.
- Vitu visivyo vya madini: haidrojeni, oksijeni, na kaboni ambazo zinapatikana kwa wingi katika anga na kwenye mvua au maji.
Madini
Udongo wenye rutuba una virutubisho vyote vikuu kwa lishe ya msingi ya mimea. Virutubisho hivi ni pamoja na nitrojeni, fosforasi, potasiamu, kalsiamu, magnesiamu na salfa, ambazo zikikosekana hudumaza ukuaji wa mimea.
Virutubisho vingine vinavyohitajika ni pamoja na chuma, zinki, shaba / kopa, boroni, molibdenamu, Manganisi, klorini, na nikeli.
Kawaida udongo wenye rutuba pia utakuwa na mabaki ya viumbe hai ambavyo vinaboresha muundo wa udongo na kuleta uhai wa kibiolojia, uhifadhi wa unyevu wa udongo, na pia utunzaji wa virutubisho. pH – Viwango vya asidi (tindikali) hudhibiti upatikanaji wa virutubishi, ukuaji wa mimea na afya ya vijidudu kwenye udongo. Mimea hukua vizuri ikiwa udongo una vipimo vya asidi kati ya 6 na 7.
Changamoto
Udongo katika maeneo mengi hauna viwango vya kutosha vya virutubisho vyote vinavyohitajika kwa ukuaji wa mimea.
Changamoto kubwa za kudumisha rutuba sahihi ya udongo, ni;
- Matumizi duni ya mbolea zinazofaa na mbinu dhaifu za marekebisho kwa kutumia mbinu hai, kwa mfano, samadi au masalia ya mimea.
- Viwango vya juu vya tindikali (asidi) kutokana na kutumia mbolea za viwandani (hasa, Diammonium Phosphate – DAP), matumizi mabaya ya mbolea, kumwagilia shamba maji yenye chumvi, na mbinu zisizofaa zinazosababisha mmomonyoko wa udongo.
- Ukosefu wa uwezo wa kutambua vizuri hali ya rutuba ya udongo, ambayo inaweza kubainisha vizuizi vikuu kwa uzalishaji wa mazao.
Mbinu za kurekebisha udongo
- Hatua ya kwanza katika kurekebisha na kuboresha rutuba ya udongo ni kujua hali ya udongo. Hii itawezekana kupitia kupima na kuchambua udongo kwenye maabara ili kujua upungufu wake na marekebisho yanayofaa. Tembelea Afisa wa Kilimo katika eneo lako kujua huduma za kupima udongo zinazopatikana karibu na wewe, ziwe za serikali ama za kibinafsi.
- Ikiwa udongo una asidi ya juu (ya pH chini ya 6) basi rekebisha kwa kutumia chokaa (lime). Chokaa hupunguza asidi na kuongeza madini ya kalsiamu na magnesiamu.
Chokaa pia hufanya fosforasi ambayo imeongezwa kwenye udongo kupatikana kwa ukuaji wa mimea, na huongeza upatikanaji wa nitrojeni kwa kuharakisha kuoza kwa vitu vilivyo hai kama masalia ya mimea na kinyesi cha mifugo. Chokaa inapatikana kwa wakala wa pembejeo.
- Ikiwa mkulima hana hela za kununua chokaa madukani, anaweza kutumia jivu kutoka jikoni. Hii inaweza kuchanganywa na kinyesi cha mifugo au wakati wa kutengeneza mbolea mboji.
- Tumia mbinu za kurekebisha tabia ya udongo kwa kuogenza kaboni. Mbinu hizi ni kama matumizi ya mabaki ya mazao na majani ya miti, kinyesi cha mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kuku, kondoo, na kadhalika, na pia mboji. Hii pia, inasaidia mizizi ya mimea kuingia katika udongo kwa urahisi na kunyonya virutubisho.
Kumbuka rutuba ya udongo inajumuisha mwingiliano wa vitu vitatu; madini, muundo wa udongo na uwepo wa virutubishi vya kibiolojia au viumbe hai. Kwa hiyo, ukuaji na nguvu ya mimea, nguvu na mavuno hutegemea upatikanaji wa virutubishi muhimu.
Ikiwa mkulima atazingatia afya ya udongo wake na kuhakikisha analisha udongo, basi udongo pia utalisha mimea na kuleta mavuno yenye tija.
Madini muhimu kwa ukuaji wa mimea
Mmea unaokosa virutubisho muhimu hauwezi kukamilisha mzunguko wake wa ukuaji, yaani mbegu haiwezi kuota, kuwa na mizizi, shina, majani, au kuweka maua vizuri, au usiweze kutoa mbegu kuunda mimea mipya.
Mara nyingi mmea wenyewe unakufa. Lakini, kuwa na virutubisho vingi pia kunaweza kudhuru na hata kuua mimea. Kwa mfano, kuwa na nitrojeni nyingi zaidi husababisha mmea kuwa na majani mengi na matunda machache. Unaweza kuokoa pesa na juhudi
na hata mimea yako ikiwa unajua ni virutubisho gani na kwa kiasi gani mimea yako inahitaji. Mimea itakuwa na afya, na kukupa mavuno mengi ikiwa itarutubishwa kwa viwango vinavyofaa, sio zaidi na sio kwa kiwango cha chini.
Nitrogeni
Inahitajika kwa shughuli ya kutengeneza chakula cha mmea na rangi ya kijani kibichi (chlorophyll) ili kunyonya nguvu kutoka miale ya jua. Ukosefu wa nitrojeni husababisha upotezaji wa nguvu na rangi. Ukuaji unakuwa polepole na majani huanguka, kuanzia chini ya mmea.
Fosforasi
Huchochea ukuaji wa mizizi na maua. Inahusika katika kusafirisha na kuhifadhi nguvu au virutubisho vya nguvu kwa mmea. Inaboresha hali ya jumla ya mmea na huongeza uwezo wa mmea kuhimili hali mbaya ya hali ya hewa. Uhaba wa fosforasi utoaji wa maua, maua huwa chache na hafifu. Pia, matawi ya mmea huwa ya rangi kahawia na iliyokunjana, na mmea huwa hafifu.
Potasiamu
Hutumika kudhibiti maji na usafirishaji wa vitu vya akiba ya mmea. Inaongeza uwezo wa mmea kutengeneza chakula (usanisinuru), inaimarisha tishu za seli, na inaamsha unyonyaji wa nitrogen.
Pia, huchochea utengenezaji wa maua, virutubishi vya nguvu. Inawezesha mmea kuhimili mazingira yasiyofaa kama baridi kali na joto la juu (kunyauka). Ukosefu wake upunguza uwezo wa mmea kuhimili baridi, joto, mashambulizi ya kuvu na vimelea wengine. Hii usababisha ukosefu wa usawa kati ya madini mengine, hasa kalsiamu, magnesiamu, na nitrojeni.
Ukosefu wa Potasiamu unajionyesha kupitia madoadoa meusi kwenye majani.
Kalishamu
Kalishamu husaidia kujenga kuta za tishu za mmea na kutia nguvu kuta za seli. Inachangia uhifadhi wa madini kwenye udongo na usafiri wa madini hayo. Pia, udhibiti wa vitu vyenye sumu kwenye mimea na inachangia ukuaji wa mbegu. Ukosefu wa kalishamu husababisha majani kuwa na sehemu za manjano na udhurungi, na hupunguza ukuaji wa mmea kwa jumla.
Magnesiamu
Magnesiamu ni msingi wa viungo vya majani vinavyotengeneza chakula cha mmea (photosynthesis). Hii inaifanya kuwa kitu cha lazima kwa ukuaji wa mmea. Inakuza ufyonzaji na matumizi ya fosforasi. Inachangia kuhifadhi sukari ndani ya mmea.
Upungufu wa magnesiamu husababisha mabua dhaifu, upotevu wa kijani kibichi katika majani na kuonekana kwa madoa ya manjano na udhurungi, hata mishipa ya majani yakibakia ya kijani.
Salfuri
Salfuri inashiriki katika utengenezaji wa tishu za kutengeneza chakula kutokana na miale ya jua. Ni muhimu katika matumizi ya nitrojeni na huchangia kupunguza ukosefu wake. Inaboresha kinga ya mimea dhidi ya magonjwa na vimelea. Uhaba wa Salfuri unasababisha wepesi wa rangi, mmea unachukua muonekano rangi iliyochakaa (chlorosis), sawawa na ukosefu wa nitrojeni.
Iron
Madini ya chuma (iron) inasaidia katika kupunguza nitrojeni na salfuri, na pia husaidia kutengeneza nguvu katika mmea. Ingawa Iron haitumiki katika usanisi wa rangi ya kijani kibichi katika majani, ni muhimu kwa uundaji wake. Hii ndio sababu, upungufu wa madini ya chuma huonesha ukosefu wa rangi ya kijani kibichi katika majani mapya.
Matawi haya yanakuwa manjano na mishipa ni ya kijani kibichi. Ili kutambua upungufu wa Iron, kwanza angalia mizizi, huonekana imelemaa kwani haichukui virutubisho.
Zinki
Ni kiungo muhimu kinachosaidia utengenezaji wa protini, na huchangia kwa sehemu kubwa michakato mingi kama uzalishaji na ukuzaji wa homoni.
Dalili za upungufu wa zinki ni pamoja na mimea kudumaa, mishipa ya majani kuwa manjano, madoa ya udhurungi kwenye majani ya juu, na majani yaliyopotoka. Bila zinki ya kutosha, nguvu ya mmea na mazao huwa chini.
Manganisi
Inaamsha kazi za seli, hasa utengenezaji wa chakula cha mmea, usanisi nuru. Pia, inaharakisha kuota na kukomaa, na kuongeza upatikanaji wa fosforasi na kalishamu.
Dalili za upungufu wa manganisi, ambazo mara nyingi huonekana kama zile za upungufu wa Iron (chuma), huonekana kama majani machanga kuwa ya manjano na mishipa ya kijani kibichi, madoa yaliyozama, na ukuaji wa mmea kupungua na hivyo kudumaa.
Boroni
Mazao ya Brassica (kauliflawa, kabeji, brokoli) yana mahitaji ya juu ya boroni, na kwa hivyo yanahusika na upungufu wa boroni, ingawa mazao mengine pia yanaweza kuathiriwa. Borini inasaidia utendaji wa seli za mmea, pamoja na utengenezaji wa protini, ukuzaji wa kuta za seli, usafirishaji wa sukari, ukuaji wa matunda na uzalishaji wa mbegu.
Kwa sababu boroni inatumika kwa ukuaji wa seli, dalili za upungufu wa boroni huonekana kwenye sehemu zinazokua kama mizizi na matawi, na kwa jumla ni pamoja na kudumaa, ncha kukunjana na kusababisha ncha kufa, na sehemu ya chini ya matawi kuwa manjano.
Boroni hupungua zaidi katika udongo wenye tindikali (asidi) ya chini 6.5 ph na udongo wenye mchanga mingi na unyevu mdogo.
Shaba
Madini ya Shaba yanahitajika kwa shughuli nyingi za mimea na kwa uundaji wa kijani kibichi (Chlorophyll), na uzalishaji wa mbegu. Upungufu wa shaba unaweza kutokea kwa mazao ya nafaka. Pia, mazao mengine ya mboga kama vitunguu, karoti n.k. yanaathiriwa na upungufu wa madini haya.
Dalili za upungufu wa shaba hutofautiana kwa mazao. Dalili za upungufu huonekana kwanza kwenye tishu na majani machanga ya mmea. Majani machanga zaidi yanaonyesha kubadilika rangi kuwa ya manjano.
Molybdenum
Inahitajika kwa viwango vidogo na husaidia mimea ya vibwetakunde kuweka nitrojeni kwenye udongo ikitumia mizizi yake. Pia, husaidia kupunguza nitrojeni inapokuwa nyingi
au ikiwa katika hali ambayo mimea haiwezi ikatumia. Upungufu wa Molybdenum haidhuru sana ukuaji wa mimea katika maeneo mengi. Molybdenum inahusiana sana na nitrojeni, hivyo, ukosefu wake unaweza kufanana na upungufu wa nitrojeni.
Mimea kufikia madini
Ili kutumiwa na mmea, virutubisho muhimu lazima vivunjwe katika hali yake ya msingi. Mmea hauwezi kutumia misombo ya kikaboni, kama ile iliyo kwenye mbolea au majani yaliyokufa, hadi hapo itakapovunjwavunjwa na kugawanyika katika fomu zao za msingi.
Mimea huchukua karibu virutubishi vyote muhimu kupitia mizizi yake, isipokuwa kaboni, ambayo huchukuliwa kupitia vishimo vidogo vilivyomo kwenye majani (stomata).
Aina ya viumbe vinavyoishi kwenye udongo husaidia mizizi kuchukua virutubisho:
Viumbe vidogo-vidogo huvunja vyanzo hai vya kaboni na kuviweka katika hali inayoweza kuchukuliwa na mmea.
Fangasi huwezesha mimea mingine kuchukua fosforasi kwa kuongeza ukubwa wa mizizi ili kuepenya kwenye udongo na kufikia madini.
Hivyo basi, ni muhimu mkulima kuhakikisha kwamba udongo wake una madini haya muhimu, udongo una viumbe hai, na hii inawezekana ikiwa itatiliwa mboji, mabaki ya mimea, na kinyesi cha mifugo.
Pima udongo wako
Ili kujua ni madini gani unahitaji kuongeza, pima udongo wako kwenye mahabara ili kujua upungufu wake na marekebisho yanayofaa. Tembelea Afisa wa Kilimo katika eneo lako kujua huduma za kupima udongo zinazopatikana karibu na wewe, ziwe za serikali ama za kibinafsi.