- Kuku

Fahamu mikakati rahisi inayoweza kutumika ili kupanua mradi wa ufugaji wa kuku

Sambaza chapisho hili

Ufugaji wa kuku unaweza kumpa mkulima kipato kikubwa. Hii inawezekana ikiwa mfugaji mdogo wa kuku atapanua kiwango na idadi ya kuku anaowafuga.

Kuku ni ndege maarufu na anayefugwa sana nchini Tanzania. Karibu kaya nyingi zinafuga kuku, kwa ajili ya nyama yake yenye ladha nzuri, mayai, pia ni ishara muhimu ya kitamaduni katika baadhi ya jamii. Kwa nini ni vigumu kuongeza kipato kutokana na ndege huyu mwenye  umaarufu mkubwa na bidhaa zake zinathaminiwa na kuhitajika?

Kuna wakati mfugaji anajikuta katika wakati mgumu akiwa na uhitaji wa haraka wa pesa, kuku ndiye mfugo wa kwanza kuuzwa. Wakati mwingine, mgeni muhimu akifika kutembelea familia, mara nyingi kama kuku wapo, huchinjwa na kufanywa kitoweo. Hivyo, idadi ya kuku kwa mfugaji inapungua au kukosa kuongezeka.

Hii inakuwa changamoto katika kukuza ufugaji wa kuku na kufanya biashara yenye tija na kusababisha kukata tamaa. Katika hali kama hii hasa vijijini, inakuwa vigumu kwa mfugaji kutoka kwenye hali ya umaskini.

Fursa katika ufugaji wa kuku Kuna fursa ya kutoka kwenye uzalishaji mdogo na kwenda hatua-kwa-hatua kufikia uzalishaji mkubwa, ambao unaleta pato kubwa na kuhakikisha usalama wa chakula na kujitosheleza kwa chakula. Hii inaweza kufanikiwa ikiwa wafugaji wadogo wa kuku watapanua viwango na idadi ya mifugo yao.

Ongeza idadi ya kuku 

Unahitaji kuongeza idadi ya kuku ili iwe na maana kibiashara. Gharama ya kuwatunza kuku inashuka idadi yao inapopanda. Chagua na kuwatenga kuku wenye hali nzuri wa mbegu, kulalia na kutotoa mayai. Usiuze kundi hili la kuku, badilisha tu jogoo. Wakizeeka au uwezo wao wa kutaga ukishuka, unawauza au kuwabadilisha. Hii inatoa uhakika wa kuwa na mayai ya kutosha kila wakati, na vifaranga wapya kila wakati.

Mara nyingi, wafugaji ambao wanaanza huwa wanatilia mkazo sana makazi ya kuku. Wanajenga nyumba za gharama kubwa, mwishowe, hawana pesa za kununua kuku kuanza ufugaji, au wananunua na kushindwa kuwatunza. Unapoanza zingatia kuongezeka kwa idadi, sio kwenye nyumba za gharama kubwa. Unaboresha makazi pole pole unapojenga kulingana na idadi ya kuku.

Ikiwa una nafasi, unaweza kuweka ua na kutenga sehemu ya kuku kutembea wakati wa mchana. Hii inawapa nafasi ya kula vyakula vyenye kijani kibichi (vitamini) na wadudu (protini), changarawe (nzuri kwa mmeng’enyo wa chakula), na kinyesi chao kinarutubisha udongo. Baadaye, wanarudi kwenye makazi yao ambapo wanapata chakula cha nyongeza kilichotengenezwa nyumbani au kilichonunuliwa madukani.

Chakula kinachozalishwa shambani kinapendekezwa kwa kuku wa asili. Inaweza kuwa mchanganyiko wa nafaka ya mahindi na chanzo cha protini kama soya.

Boresha kila kizazi

Boresha kundi lako kwa kutumia jogoo wa hali ya juu na walioboreshwa, kwa ajili ya kuzaliana na ndege waliochaguliwa kwa uangalifu na ubora. Faida ya kutumia jogoo walioboreshwa ni kwamba utakuwa unaingiza sifa za kukua haraka na mayai makubwa.

Anza na kuku jike wa msingi wenye afya na nguvu.

Weka jogoo mmoja kwa uwiano wa kuku jike kumi. Ukiweka jogoo zaidi basi kuku wako watazidiwa, watafukuzwa kila wakati, watachoka na usumbufu unaathiri kukua kwao na afya kwa ujumla. Kuwa makini kutambua ishara za kupandana kupita kiasi; majeraha, kupoteza manyoya ya nyuma, mabawa, na nyuma ya kichwa. Ukiona haya, punguza idadi ya jogoo.

 Dhibiti Magonjwa 

Kuku hushambuliwa na magonjwa na husababisha hasara kubwa katika ufugaji wa kuku. Ugonjwa wa kutisha zaidi ni Kideri/Mdondo (Newcastle). Punguza uwezakano wa maambuzi ya magonjwa kwa kuwapa kuku lishe bora, weka makazi safi, na kufuata utaratibu wa chanjo. Pia, wape kuku dawa ya miyoo, la sivyo, chakula unachowapa kitakuwa cha kulisha vimelea.

Ikiwa mfumo wa ufugaji huria, wape dawa ya minyoo kila baada ya mwezi moja, na katika mfumo wa nusu huria au ndani wape dawa ya minyoo kila baada ya wiki 6-8. Pia, nyunyiza majivu au chokaa au dawa za kuua wadudu kila mara unapofanya usafi wa banda.

Tenga kuku wapya kutoka nje ya shamba lako kwa angalau wiki mbili. Kwa njia hii, unalinda kuku wako dhidi ya vimelea ambavyo vinaweza kuletwa kutoka shamba lingine.

ANGALIZO: Kukizuka maambukizi ya magonjwa, ondoa na kuchoma au kuzika kuku wote waliokufa. Kuwa na daktari wa mifugo karibu kwa ajili ya ushauri kila wakati unapoona dalili au kushuku kuku wako ni wagonjwa.

Ungana na wafugaji wengine

Pengo moja kubwa katika kukuza sekta ndogo ya kuku nchini ni kutokuwa na vikundi, mashirika na majukwaa ya wafugaji kuku. Mashirika ya wakulima yaliyopo yameundwa vibaya, viongozi ambao hawana maono na uzoefu wa kibishara, na uwezo wa kujenga na kudumisha makundi ya wafugaji.

Ungana na wafugaji wengine ili kuweka mifumo thabiti ya kuzalisha kuku wa hali ya juu. Hii itawawezesha kufikia soko la mbali, kununua chakula cha kuku kwa wingi na kwa bei ya jumla. Mnaweza kutengeneza chakula cha kuku, na kununua malighafi kwa bei ya chini. Pia, kuna nafasi ya biashara ya kuuza chakula cha kuku mlichotengeneza au malighafi kwa wafugaji wengine katika eneo lako na kwingineko. Hii itaongeza njia za kikundi kupata faida.

Wekeza faida

Usiuze kuku mmoja mmoja. Uza kuku wengi mara moja ili upate pesa ya kufanya jambo la maana. Uza wakati bei katika soko iko juu kabisa. Fuatilia soko la kuku ili kujua mfumuko wa bei. Hii itakuwezesha kuepuka hasara. Jambo la muhimu ni kuwekeza sehemu ya faida kwa kuongeza idadi ya kuku, kuboresha malisho, makazi na dawa za chanjo, na matibabu ikiwa magonjwa yatazuka.

Unaweza kutumia mapato kutokana na mauzo ya mayai ili kulipa gharama za kila siku za kuendesha ufugaji, na pesa kutoka kwa mauzo ya kuku kupanua biashara yako ya kuku.

Hakikisha tu, hauli kuku anayetaga yai. Ukifanya hivyo, utakuwa unazika biashara yako.

Chukua hatua

  Je, wewe ni mfugaji wa kuku? Ni mikakati gani unatumia kupanua ufugaji wako na kuongeza mapato? Wasiliana nasi ili tuwashirikishe wafugaji wengine uzoefu wako.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *