- Kilimo

Wakulima Watumia Taarifa za MkM Kuboresha Uzalishaji

Sambaza chapisho hili

Jambo la kufurahisha ni pale unapoona mkulima anajifunza na kutekeleza, hii inatia moyo. Mmoja wa wakulima wanufaika wa jarida la Mkulima Mbunifu ametia fora kwa namna ambavyo amepokea mafunzo ya kilimo ikolojiahai.

Mbinu mbalimbali zilizoandikwa zimejipatia umaarufu mkubwa miongoni mwa wakulima kiasi cha kuanza kutekeleza mara moja, ni pamoja na utunzaji wa udongo, matumizi ya mbolea na madawa ya asili, ufugaji wa kuku, hasa wa kienyeji, ulishaji wa ng’ombe wa maziwa, kilimo cha parachichi, na uzalishaji wa mbogamboga.

Wakulima wanasema kwamba kwa muda mrefu, wamekuwa wakifanya kazi bila ya kuwa na taarifa sahihi zinazohusiana na shughuli zao. Wanaendelea kujipanga, kuunda ama kujiunga na vikundi ili kupokea jarida.

Kilimo mseto kinanipa uhakika wa pesa

Mimi ni Turufaina Simon Lyatuu kutoka kijiji cha Mkalama katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro. Nina jumla ya ekari 11 ambapo nafanya kilimo ikolojia. Mazao ninayolima kwenye eneo hilo ni migomba, mpunga, mahindi, maharage, magimbi, parachichi, papai, minazi, miwa na mbogamboga.

Nimejihusisha na kilimo kwa muda mrefu kwa kuwa nilizaliwa katika familia ambayo shughuli yake kuu ni kilimo. Tumesomeshwa na kukua kupitia kilimo na nilivyoanza kujitegemea tu, nikaendeleza kilimo. Pia, wakati fulani nilijifunza kilimo na ufugaji katika chuo cha Tengeru na kunifanya nikipende kilimo zaidi. Lengo langu kuu ni kupata kipato cha kutosha na cha uhakika.

Kupitia gazeti la Mkulima Mbunifu, nimejifunza mbinu nyingi za kilimo hai. Kwa mfano, matumizi ya mbolea za asili, madawa vya asili, kilimo mseto, matumizi na faida za mbegu za asili.

Katika kutekeleza kilimo hai, changamoto kubwa ni kwamba huwezi kumwachia mtu aandae mbolea au dawa wakati haupo kwa kuwa wenye elimu hii ni wachache, tofauti na madawa ya madukani ambayo yameandikwa kwenye vifungashio vyake namna ya kuzitumia.

Pia, kukosa mbadala wa baadhi ya mimea dawa ambayo siyo ya asili ya maeneo yetu hali iliyonilazimu kutafuta mbegu kutoka sehemu nyingine na kupanda shambani kwangu. Kupanda aina nyingi ya mazao, inaniwezesha kuuza kila wakati, hakuna siku nisiyouza chochote hapa shambani na hii yani inanipa uhakika wa pesa. Zaidi, napata pesa ya kutosha kununua vile ambavyo silimi kwani kila mara kuna mazao yaliyoko tayari shambani.

Nimeweza kupata masoko mapya kwa kushiriki maonyesho mbalimbali kupeleka bidhaa ninazozalisha, mfano kwenye Nane-Nane na maonyesho mengine mengi. Pia, nauza kwa majirani na watu wa maeneo mbalimbali ninaokutana nao kwenye maonyesho na wanapendezwa na bidhaa zangu.

Kilimo hai kimekuwa cheenye manufaa makubwa kwenye shamba langu. Uwezo wa udongo kuzalisha umekua mkubwa, kwa mfano, hata nisipotumia mbolea kabisa misimu mingine, bado navuna vizuri. Unyevu unadumu kwa muda na nimepunguza kumwagilia kila mara. Mwanzoni nilikua namwagilia mara 2 kwa wiki, lakini sasa ni mara moja mpaka siku 10.

Nashauri wakulima wajifunze kilimo ikolojia kwani hakiitaji wewe kutoka nje ya shamba lako, mazao yanategemeana na pia gharama yake ni nafuu. Jarida la Mkulima Mbunifu ndio ngao ya kilimo chenye tija kwa wakulima kama sisi.

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Turufaina Simoni, kwa simu namba 0712921454 Arusha Tanzania.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *