- Kilimo, Kilimo Biashara, Masoko

Unapouza mazao yako zingatia vipimo sahihi

Sambaza chapisho hili

Wakulima walio wengi wamekuwa wakipoteza mamilioni ya shilingi kutokana na uuzaji wa mazao kwa kutumia vipimo visivyokuwa sahihi

Kwa kawaida wakulima wanapoamua kufanya shughuli ya uzalishaji wa mazao huwa na malengo makubwa sana ya kufaidika kutokana na mazao hayo pindi msimu wa mavuno unapofika.

Hii imekuwa ni tofauti kabisa kutokana na wakulima kuishia kupata hasara inayosababishwa na kuuza mazao yao kwa walanguzi kwa kutumia vipimo visivyokuwa sahihi.

Uuzaji wa mazao kiholela na kwa kutumia vipimo visivyokuwa sahihi unasababishwa na ufinyu wa upatikanaji wa soko la mazao hayo, ubovu wa miundo mbinu, ukosaji wa taarifa sahihi za mazao na mambo mengine kadha wa kadha.

Mtindo wa lumbesa ni moja ya aina ya uuzaji wa mazao ambao umekuwa ukimsababishia hasara kubwa mkulima. Mtindo huu humlazimu mkulima badala ya kuuza mazao kwenye gunia la debe 6 kuongeza kilemba kwenye gunia hilo kiasi cha debe 5 huku akiuza kwa bei ile ile ya gunia moja linalochukua debe 6.

Sababu nyingine ya wakulima kupata hasara ni kuuza mazao yao kwa kukadiria yakiwa shambani bila kuwa na uelewa sahihi wa kuthaminisha mazao yao. Wachuuzi na walanguzi hutumia mwanya huo kuwalangua wakulima na wao kupata faida kubwa huku mkulima akipata hasara kutokana na bei finyu anayoipata.

Ili kuondokana na hali hiyo, ni muhimu wakulima wakazingatia na kuepuka mambo yafuatayo:

  • Usikubali kuuza mazao yako kwa mtindo wa lumbesa
  • Usiuze mazao yako kwa kukadiria yakiwa shambani
  • Usiweke mazao yako rehani
  • Usikimbilie kukopesha wachuuzi mazao yako
  • Usikimbilie kuuza mazao bila kufahamu bei halisi ya soko

Ni muhimu wakulima wakaungana kwenye vikundi na kuwa na sauti moja inayopinga uuzwaji wa mazao kwa njia isiyokuwa sahihi. Halikadhalika ni muhimu sana kwa wakulima kuwatumia wakala wa vipimo, ili waweze kuwasaidia kupata njia sahihi ya upimaji wa mazao wanayozalisha kabla ya kufikia muafaka wa kuuza.

Pia ni muhimu kwa wakulima kuhakikisha kuwa wanapata taarifa sahihi za soko la aina ya mazao wanayozalisha, ili kuweza kuuza kwa bei ambayo watapata faida na kusonga mbele bila kukata tamaa kutokana na ufinyu wa kipato unaosababishwa na uuzaji usiosahihi.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *