- Kilimo

Umuhimu wa wataalamu kwa wakulima na wafugaji

Sambaza chapisho hili

Wataalamu wa kilimo na mifugo wamepata mafunzo ili kuendeleza mbinu za kilimo na mifugo kwa lengo la kutoa faida kwa wakulima na wafugaji.

Baadhi ya wataalamu wanaweza kuona upungufu fulani au kuona kuwepo kwa mantiki kwenye baadhi ya mbinu za asili ambazo bado zinatumiwa katika uendeshaji wa kilimo na ufugaji na kuweza kuafikiana na wakulima hao juu ya kuziendeleza au kuziboresha kwa maslahi zaidi.

Kutokana na sababu moja au nyingine, mara nyingi wafugaji hupoteza imani kwa wataalamu na kushindwa kushirikiana nao katika shughuli zao za kilimo na ufugaji. Pamoja na hayo, bado wataalamu kwa kiasi kikubwa sana huwa na mawazo mazuri ambayo huhitajika kufikiriwa na kuona uwezo wake katika kuboresha shughuli za kilimo na mifugo.

Wataalamu wanatoka wapi

Mara nyingi wataalamu wa kilimo na mifugo hupelekwa na serikali kufanya kazi kwa karibu zaidi na wakulima na wafugaji katika vituo mbalimbali vijijini. Lengo ni kuwaendeleza na kuwafanya wakulima kuzalisha kwa ubora unaokidhi viwango na wenye kuleta faida kubwa.

Wakulima na wafugaji wanaojipatia huduma kutoka kwa wataalamu hao mara nyingi wamekuwa wachache kuliko inavyotegemewa. Hawa ni wale wenye uwezo wa kulipia huduma hizo au wale walio tayari kujaribu mbinu mpya.

Aidha, wakulima na wafugaji wameshindwa kujipatia huduma hizo kutokana na ama kutomudu gharama zake, au kutokuwa maarufu kiasi cha kuweza kusaidiwa au pengine eneo fulani kuwa na idadi ndogo ya wataalamu wa aina hiyo ukilinganisha na idadi kubwa ya wakulima na wafugaji wanaostahili kuhudumiwa.

Baadhi ya njia wanazotumia wakulima na wafugaji kupata msaada kutoka kwa wataalamu

Kuwa wepesi wa kukubali na kutumia mbinu mpya za ufugaji zinazotolewa kwao na wataalamu. Wataalamu wengi hutiwa moyo waonapo mbinu mpya wanazofundisha zinakubalika na kutekelezwa.

Katika hali hiyo hawatasita kuwatembelea mara kwa mara wafugaji waliopokea na kutekeleza mbinu hizo. Kwa kawaida mtaalamu anaposita kuwatembelea baadhi ya wafugaji, hafanyi hivyo kwa sababu ya kutopewa malipo au zawadi fulani bali ni kwa sababu hawatekelezi ushauri wanaopata kutoka kwake.

Kama wewe ni mfugaji, unashauriwa kuzungumza na mtaalamu wa mifugo aliye karibu na wewekuhusu shughuli za ufugaji. Hii itasaidia kuonesha kuwa kweli una nia ya kuziendeleza na unataka kupunguza kiwango cha athari kwa kujaribu mbinu mpya hadi kuwa na uhakika kwa kiwango fulani. Kuunda kikundi cha wafugaji au wakulima kisha kuwaalika wataalamu ili kuja kutoa mafunzo mbalimbali na kuzungumza na wanakikundi.

Mara nyingi wataalamu hukosa raha pale kunapokosekana watu wanaowasikiliza na kufuata ushauri wanaotoa huku shughuli wanazowajibika kuweka katika hali nzuri kuenda kombo. Wataalamu hao hawafurahi wanaposhindwa kukidhi haja za wafugaji kwa sababu ya wingi wao na hivyo kunapoundwa kikundi cha wafugaji au wakulima katika eneo fulani huonesha hamu ya wafugaji au wakulima hao kupiga hatua katika shughuli zao na kutekeleza mbinu mpya au kuboresha zile zinazotumika.

Kwa kawaida wataalamu hutafuta vikundi vya aina hiyo kwani huwa ni nafasi nzuri kwao kueneza utaalamu kwa watu wengi zaidi watakaouthamini kwa wakati mmoja. Wataalamu hao watapendelea kukutana na kundi lililokwishaundwa kuliko kujaribu kuwashawishi watu ili waanzishe kundi jipya.

Hali ya kuwa tayari kupokea wageni shambani mwako ni jambo ambalo litawatia moyo wataalamu na kuwafanya walete wageni wengine zaidi. Matokeo ya hali ya namna hiyo ni wataalamu kupenda kuonesha kuwa unapiga hatua katika shughuli zako za kilimo au ufugaji

Kwa nini ni muhimu kuwatumia wataalamu wa kilimo/ufugaji

  • Wakulima hupatiwa mbinu bora na za kisasa zinazotumika katika uzalishaji wa mazao ya kilimo au ufugaji.
  • Wakulima na wafugaji hupata fursa ya kujua na kutumia mbegu bora zinazoshauriwa katika maeneo yao kulingana na hali ya hewa hivyo kuweza kupata uzalishaji mkubwa na wenye ubora.
  • Wataalamu huwafundisha wakulima na wafugaji namna ya kuzalisha kwa viwango pendekezwa kwa ubora ili kulinda afya za walaji au watumiaji wa mazao yaliyozalishwa.
  • Wafugaji na wakulima wataweza mahitaji ya soko la ndani na la nje.
  • Wataalamu pia huwaelimisha wakulima namna ya kufanya uzalishaji ambao hautaathiri mazao na mazingira kwa ujumla.
  • Wakulima na wafugaji hujifunza namna ya kuzalisha na kusindika bidhaa ili kuuza mazao au bidhaa zilizoongezewa thamani badala ya kuuza bidhaa ghafi/malighafi.
  • Wataalamu pia huwafundisha wakulima na wafugaji njia mbalimbali ya kutumia ili kuweza kudhibiti wadudu na magonjwa yanayoshambulia mazao au mifugo yao.
  • Wataalamu pia ni waunganishaji wazuri baina wa wakulima wa eneo moja na jingine kwa kuwashirikisha mbinu mbalimbali wanazotumia wenzao na hata kuweza kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuzalisha kwa mafanikio makubwa.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na mtaalamu wa kilimo na afisa masoko Lucas Rwechoka kwa simu +255754886888.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *