Katika uzalishaji wa mazao kwa misingi ya kilimo hai ambacho ni aina ya kilimo kinachozingatia usalama wa chakula na kuondokana na matumizi ya kemikali za viwandani changamoto ya magonjwa na wadudu pia hutokea, jambo linalohitaji usimamizi mzuri ili kuleta uzalishaji wenye tija.
Faida ya kuzalisha kwa misingi ya kilimo hai hasa katika kukabiliana na magonjwa na wadudu ni kuwa njia zinazotumika katika uzalishaji zinasaidia kupunguza na haziruhusu kuwepo kwa kiasi kikubwa cha wadudu na magonjwa shambulizi kwenye mimea.
Zana za kilimo hai katika udhibiti wa wadudu na magonjwa
Hatua 1: Kilimo kinacholenga usimamizi bora wa mazao
Utendaji huu unalenga katika kujenga mazingira bora ya kukua kwa mimea hivyo kuendeleza afya ya mimea na kuzuia kuingia na kuenea kwa wadudu na magonjwa. Haya yanaweza kufanikishwa kwa kufanya yafuatayo:
- Uchaguzi wa aina stahiki ya mazao yanayofaa kwa eneo husika. Pale inapowezekana, aina za mazao ambazo zinastahimili au zinamudu wadudu na magonjwa zitumike.
- Kutumia mbegu au vichipukizi vilivyo safi. Yaani visivyokuwa na magonjwa au wadudu.
- Kuboresha rutuba ya udongo ili kuhimiza mimea iwe na nguvu na kukua kwa haraka, kwa kutumia mboji, mbolea ya wanyama, mbolea itokanayo na mimea na vitu vingine vya asilia.
- Kilimo mseto na kilimo mzunguko wa mazao ambayo husaidia kupunguza kasi ya ongezeko la wadudu.
- Mbinu nyingine za utendaji zinazohakikisha ukuaji sahihi wa mimea kama kupanda kwa wakati, nafasi sahihi, hifadhi ya maji, kupunguza matawi, kuweka kivuli na kuvuna kwa wakati).
Hatua 2: Hatua za kudhibiti mazingira
Utendaji huu unalenga kukuza kuongezeka kwa viumbe anuwai (pamoja na maadui wa asili) kuzunguka na ndani ya mashamba. Hii inajumuisha:
- Kupanda kwenye uzio spishi za mimea ya asili kuzunguka mashamba ili kuvutia wadudu maadui wa asili. Kuruhusu spishi za mimea zinazotoa maua kukua karibu na mazao ili kutoa nekta na chavua kwa wadudu adui wa wadudu waharibifu.
- Kupanda mimea ambayo inavutia wadudu kwenda kwenye mimea ambayo sio mazao au inayosukuma wadudu kutoka kwenye mazao (kama mkakati wa sukuma/ vuta).
- Usafi wa shamba ikijumuisha kupalilia kwa wakati ili kuondoa mimea mingine inayohifadhi wadudu, mimea na sehemu za mimea iliyoambukizwa, kutokomeza kwa njia sahihi mimea yenye ugonjwa na kusafi sha zana kwa kiuatilifu ambazo zilizotumika kwenye mimea/shamba yenye ugonjwa.
Hatua 3: Udhibiti wa moja kwa moja
Katika mazingira ya mashambulizi makubwa au wadudu na magonjwa yanayoleta uharibifu mkubwa, hatua za moja kwa moja zitahitajika ili kupunguza hasara. Zana hizi zitaweza kufanya kazi vizuri pale tu ambapo hatua nyingine mbili zinapotumika kwa usahihi. Hizi zinajumuisha:
- Viumbe vya udhibiti wa kibiolojia kama vile wadudu adui wanaoshambulia wadudu waharibifu, vimelea vya wadudu, virusi na bakteria.
- Viuatilifu au dawa za kupe zilizoidhinishwa au zilizotengenezwa nyumbani zenye asili ya kibaolojia au madini ikijumuisha maji ya mmea uliokamuliwa, mafuta ya mimea, mafuta ya madini, madini ya kopa na salfa.
- Kama inapatikana, mitego yenye feromoni inayovutia madume inaweza kutumika kuvuruga kuzaliana kwa wadudu.
- Mitego ya mwanga, chambo au rangi inaweza kutumika kunasa wadudu wengi.
- Kuosha mbegu na maji ya moto hupunguza magonjwa yanayoenezwa na mbegu.