Katika kilimo hai kama ilivyo kwa aina nyingine ya kilimo na uzalishaji wa mazao, mara nyingi wadudu na magonjwa vinaweza kuwa moja ya sababu kwa mkulima kukosa mavuno au kupata mavuno hafifu na yasiyokidhi soko lakini pia yasiyokuwa na ubora.
Wadudu na magonjwa visipodhibitiwa, humsababishia mkulima hasara kwa kiasi cha asilimia 20 hadi 80. Kutokana na hali hiyo, ni muhimu kuzuia magonjwa na wadudu kwa kutumia njia mbalimbali kama vile kutoa magugu, kubadili mazao kwa njia ya mzunguko na kutumia madawa ya asili ambayo yanaweza kuwa shambani kwa muda mrefu.
Njia za kuzuia wadudu na magonjwa
Kufanya kilimo cha mzunguko
Kilimo cha mzunguko ni njia ya asili ya kulima mazao kwa kubadili aina ya mazao kila msimu kwenye eneo moja la shamba au kitalu.
Kwa mfano; msimu huu unapanda zao la maharagwe au kunde na msimu unaofuata unalima kabichi, mchicha au matembele. Yaani, unabadilisha aina ya mazao kwa kuangalia zao husika lipo kwenye kundi gani la mazao na kuangalia kama zao unalotaka kulilima linakinzana kitabia na zao lililovunwa.
Kuzuia magonjwa
Kwa kuendelea kuotesha/kupanda zao la aina moja kwa zaidi ya msimu mmoja ni dhahiri kuwa magonjwa mengi huibuka na huwa sugu kuisha na kufanya udhibiti wake kuwa mgumu sana, lakini kwa kufanya kilimo cha mzunguko wa mazao utafanikiwa sana kupunguza/kuondoa kabisa magonjwa hayo.
Kuzuia Wadudu
Wadudu kama minyoo fundo huwa si rahisi sana kufa ama kupote shambani hasa ikiwa unatumia desturi ya kupanda mazao yale yale kwa muda wa zaidi ya msimu mmoja, au kwa kupanda mazao yaliyo kwenye jamii moja hivyo njia ya kudhibiti ni kufanya kilimo cha mzunguko wa mazao.
Nini faida za kilimo cha mzunguko?
- Kuongeza na kuimarisha virutubisho kwenye udongo hasa pale mazao jamii ya mikunde inapopandwa.
- Kupunguza na kuondoa wadudu waharibifu.
- Kupunguza uwezekano wa kuwepo magonjwa shambulizi.
- Rutuba ya udongo hutumika vyema na mazao yatakayo badilishana.