- Kilimo

Sindika machungwa kuepuka hasara na upotevu usio wa lazima

Sambaza chapisho hili
Machungwa huweza kuliwa kama matunda au kusindikwa kupata bidhaa zingine

Machungwa ni moja ya mazao ya matunda ambayo yanalimwa sana kwa wingi katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Mwanza. Zao hili ni la chakula na biashara.

Ikiwa huu ni msimu wa machungwa, wakulima hawana budi kujifunza namna mbalimbali za kusindika zao hili ili kuondokana na upotevu unaotokana na wingi wake na kukosekana kwa soko au kuuzwa kwa bei ndogo sana na ya hasara.

Mkulima anaweza kuchukua hatua za kusindika zao hili na kupata bidhaa mbalimbali kama vile juisi, jamu, mvinyo na mamaledi.

Moja wapo ya bidhaa zinazoweza kutokana na zao hili ni juisi ambayo huwa na virutubisho mbalimbali mwilini na hutumiwa wakati wote pale mtu anapojisikia kutumia.

Namna ya kusindika machungwa kupata juisi

Juisi ya machungwa ni muhimu kwa afya ya binadamu kwani ina vitamini C kwa wingi ambayo hukinga mwili dhidi ya maradhi mbalimbali.

Vifaa

Vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kutengeneza juisi ni pamoja na mizani, mashine ya kukamulia juisi ya umeme, sufuria, jiko, meza safi ya aluminiamu, kisu kisichoshika kutu, lakiri, lebo na chupa za kioo zenye mfuniko.

Malighafi

  • Machungwa safi yaliyokomaa na yasiyooza.
  • Sukari safi nyeupe.
  • Maji safi na salama.

Njia ya kutayarisha

  • Chagua machungwa yaliyokomaa na kuiva vizuri kisha osha kwa maji safi na salama.
  • Menya machungwa kwa kutumia kisu kisichoshika kutu.
  • Kata machungwa na kukamua juisi kwa kutumia mashine ya umeme au ya mkono kisha chuja juisi kwa kutumia chujio safi.
  • Pima ujazo wa juisi kwa kutumia kikombe cha kupima ujazo.
  • Sukari huongezwa kwa kutegemea matakwa. Endapo itatumika, weka sukari isiyozidi ambayo ni sawa na gramu 160 katika kila lita moja ya juisi.
  • Chemsha juisi kwa muda wa dakika 25 hadi 30 katika joto la nyuzi 80 hadi 90.
  • Jaza juisi ikiwa moto katika chupa ambazo zimesafishwa vizuri kisha kuchemshwa na acha nafasi ya milimita 5 toka kingo yam domo wa chupa.
  • Funika vizuri kwa kutumia mifuniko safi na panga chupa kwenye sufuria.
  • Weka maji kwenye sufuria hadi kufikia nusu ya kimo cha chupa na chemsha kwa muda wa dakika 25 hadi 30.
  • Ipua, acha zipoe kisha weka lakiri na lebo. Lakiri huwekwa kwenye mfuniko ili kuzuia hewa isiingie ndani ya bidhaa.
  • Hifadhi sehemu safi tayari kwa matumizi. Kwa kawaida juisi iliyotengenezwa kwa njia hii inaweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi sita bila kuharibika.

Uwekaji wa lebo uonyeshe yafuatayo;

  • Jina la bidhaa na jina na anuani ya mtengenezaji.
  • Tarehe ya kutengeneza na ya kuisha matumizi ya bidhaa hiyo.
  • Ujazo na viamabaupishi vilivyomo.

Matumizi

Juisi ya machungwa hutumika kama kiburudisho cha kukata kiu na ina vitamini C kwa kiasi ambacho hakitofautiani sana na juisi ya machungwa ambayo hayajasindikwa kwani juisi hii haichemshwi kwa kiasi cha kupoteza kirutubisho hicho.

 

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *