Karakara ni zao la matunda ambalo ni muhimu kwa biashara na chakula linalolimwa katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Kigoma, Mbeya, Kilimanjaro na Arusha.
Mara nyingi wakulima huzalisha zao hili kwa wingi sana kwa msimu mmoja na hatimae kushuka kwa soko lake na kufanya kuwepo kwa upotevu na uharibifu wa matunda haya.
Ili kuondokana na uharibifu huu, ni vyema mkulima akajifunza namna ya kusindika matunda haya ili kuweza kupata kipato kinachostahili na kuhifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadaye.
Kuchambua, kusafisha na kupanga madaraja
Kabla ya kujifunza namna ya kusindika, ni vyema mkulima akafahamu namna ya kuchambua, kusafisha na kupanga madaraja ya matunda haya baada ya kuvuna ili kuweza kusafirisha kwenda sokoni ama kuhifadhi.
Kuchambua
Karakara huchambuliwa ili kuondoa zile zilizooza au kuharibika kupita kiasi. Wakati wa kuchambua, ni muhimu sana kuzingatia mambo yafuatayo;
- Karakara zilizooza na zenye wadudu zifukiwe ili kudhibiti kuene kwa wadudu waharibifu na vimele vya magonjwa.
- Matunda yaliyopasuka, kubonyea au kuchubuka kidogo yatumike haraka kwa chakula.
- Matunda mazuri ambayo hayajapata madhara yoyote yatumike kwa kusindika au kuuzwa.
Kusafisha na kuweka nta
Safisha karakara kwa maji safi na salama ili kuondoa uchafu na kisha nyunyizia nta kwenye matunda ili kurefusha muda wa kuhifadhi hadi kufikia kipindi cha wiki tano.
Kupanga madaraja
Panga karakara kwa madaraja kulingana na uhitaji, matumizi ya matunda, ukomaaji, ukubwa, rangi au aina.
Kufungasha
Fungasha karakara kwenye makasha ya mbao, plastiki au karatasi ngumu.
- Karakara za rangi ya zambarau hupangwa nyingi zaidi katika makasha ukilinganisha na yale ya rangi ya manjano ambazo ni kubwa zaidi.
- Tanguliza karatasi laini ndani ya makasha ili kuzuia matunda kuchubuka au kutobolewa.
- Uzito wa kasha usizidi kilo 20 ili kurahisisha ubebaji
- Matunda yapangwe ndani ya kasha kwa kubananisha ili kuzuia yasigongane na kubonyea wakati wa kusafirisha.
Kusafirisha
Unaweza kusafirisha karakara kwa kutumia mikokoteni, baiskeli, magari na matrekta kulingana na uwezo wako mkulima kumudu gharama za usafirishaji pamoja na hali ya barabara.
Kuhifadhi Hifadhi karakara katika sehemu yenye ubaridi upatao nyuzi joto 5 hadi 13 za sentigredi na unyevu wa asilimia 80 hadi 90. Katika hali hiyo matunda ya rangi ya zambarau huweza kuhifadhiwa kwa muda wa wiki nne hadi tano bila kuharibika.
Kusindika karakara kupata juisi
Ili uweze kusindika karakara ni lazima uwe na vifaa, malighafi zinazohitajika na ufahamu njia sahihi za kusindika.
Vifaa
- Visu visivyoshika kutu, jiko, sufuria, chupa au makopo yenye mfuniko, mizani, chujio, mashine ya kukamua juisi, lebo na lakiri, kipima joto, meza safi iliyofunikwa na bati la aluminiamu, kipimo cha sukari (refractometer) na saa.
Malighafi
Malighafi inayohitajika ni karakara zilizoiva vizuri na maji safi na salama.
Namna ya kuandaa
- Chagua matunda yaliyoiva vizuri kisha osha kwa maji safi na salama.
- Pima uzito wa matunda na kata matunda kisha ondoa mbegu na juisi yake.
- Saga juisi pamoja na mbegu za matunda na chuja kwa kutumia kitambaa safia au chujio.
- Chemsha kwenye joto la kawaida (nyuzi joto 80 hadi 90 za sentigredi) kwa muda wa dakika 25 hadi 30.
- Weka juisi ikiwa ya moto katika chupa ambazo zmechemshwa vizuri na acha nafasi ya milimita 5 kutoka kingo ya mdomo wa chupa ili kuruhusu uwazi unaozuia maambukizi ya vimelea.
- Funika chupa kwa mifuko imara na safi kisha panga kwenye sufuria safi.
- Weka maji kwenye sufuria hiyo hadi kufikia nusu ya kimo cha chupa na chemsha tena kwa muda wa dakika 20.
- Weka lebo inayoonesha tarehe ya kusindika, viambaupishi, tarehe ya mwisho ya kutumika na jina la msindikaji.
- Hifadhi kwenye sehemu yenye ubaridi tayari kwa kutumia. Juisi ya karakara iliyotengenezwa kwa njia hii huhifadhika kwa muda wa miezi sita bila kuharibika.
Matumizi
Juisi hii hutumika kama kiburudisho au kikata kiu