Tangawizi ni moja ya mazao ya viungo linalimwa katika mikoa mbalimbali Tanzania kama vile, Tangam Morogoro, Kilimanjaro, Kigoma, Pwani, Iringa, Mbeya na Kagera.
Tangawizi ili iweze kusindikwa kwa ajili ya kupata bidhaa mbalimbali, inahitajika kwanza kuhakikisha umezingatia uvunaji sahihi ikiwa ni pamoja na kuvuna mapema ili kuepuka kukomaa zaidi na kuchipua tena pamoja na ufungashaji na uhifadhi uliozingatia ubora.
Kuvuna Tangawizi
Tangawizi za kukausha, hutakiwa kuvunwa baada ya sehemu ya juu ya shina kukauka. Uvunaji wa tangawizi mbichi kwa ajili ya matumizi ya mboga hufanyika miezi minne hadi mitano baada ya kupanda.
Njia bora ya uvunaji ni kwa kutumia mikono ambapo mashina ya tangawizi huchimbuliwa kwa kutumia jembe uma.
Kusafisha na kuchambua
Tangawizi zinapong’olewa huwa na udongo mwingi, majani na takataka nyingine hivyo ni muhimu kusafisha na kuchambua. Udongo hukung’utwa na majani hukatwa kwa kutumia kisu kikali.
Kusafisha
Osha tangawizi kwa maji safi hadi udongo wote utoke kisha weka juu ya kichanja ili maji yadondoke.
Kuchambua
Ondoa tangawizi zote zilizooza au kuharibika kisha tenganisha tangawizi nzima na zile zilizovunjika.
Kupanga madaraja ya tangawizi mbichi
Tangawizi mbichi zipangwe kwenye madaraja kufuatana na rangi, aina, ubora na ukubwa.
Tangawizi zenye rangi na ukubwa unaolingana ziwekwe pamoja na zile zilizovunjika ziwekwe pia pamoja.
Kufungasha tangawizi mbichi
Kiasi kikubwa cha tangawizi huharibika kutokana na kutumia vifungashio duni kama vile magunia ambayo husababisha tangawizi kuchubuka na kuvunjika wakati wa kupakia na kupakua.
Tangawizi mbichi zinaweza kufungashwa kwa kutumia vifungashio kama vile makasha ya mbao, plastiki na ya karatasi magumu yenye matundu yanayoruhusu mzunguko wa hewa. Ufungashaji kwa kutumia vyombo hivyo hupunguza upotevu wa zao wakati wa kusafirisha na kuhifadhi.
Wakati wa kufungasha, hakikisha kila kasha halizidi kilo 20 ili kurahisisha upakiaji na upakuaji.
Kuhifadhi tangawizi mbichi
Tangawizi mbichi huweza kuhifadhiwa katika hali ya hewa yenye ubaridi upatao nyuzi joto 13 za sentigredi na unyevu wa asilimia 65. Katika hali hiyo tangawizi huweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi sita bila kuharibika.
Tangawizi hizo zinatakiwa kuhifadhiwa kwenye kichanja bora chenye sifa zifuatazo;
- Upana wa kichanja usizidi mita mbili kwa ajili ya kuweka urahisi wa kukagua tangawizi.
- Kichanja kiruhusu mzunguko kidogo wa hewa yenye ubaridi.
- Kichanja kiinuliwe juu sentimita 30 kutoka usawa wa sakafu ili kuruhusu mzunguko wa hewa.
- Tangawizi ziwekwe kwa kutandazwa kwenye kichanja ili kuepuka uwezekano wa kushambuliwa na ugonjwa wa ukungu na kagua mara kwa mara ili kuona kama kuna uharibifu.
Kukausha tangawizi
Tangawizi zinaweza kukaushwa ili kurahisisha ufungashaji wa hifadhi ya muda mrefu. Baada ya kuvuna, tangawizi zisafishwe kwa maji safi ili kuondoa udongo na takataka nyinginezo.
Weka tangawizi kwenye maji yanayochemka kwa lengo la kubabua maganda, kisha menya kwa kutumia kisu au kijiti cha mwanzi chenye makali na kausha kwa kutumia kaushio bora.
Njia nyingine unayoweza kutumia ni kumenya tangawizi safi mbichi kwa kutumia kisu au kijiti cha mwanzi kisha osha kwa maji safi na kausha kwenye kaushio au kichanja bora, mkeka au jamvi. Ukaushaji huu huchukua muda wa siku sita hadi nane kutegemeana na hali ya hewa. Ili kukausha tangawizi vizuri, inashauriwa kukausha hadi kufikia unyevu wa asilimia 10.
Kupanga madaraja ya tangawizi kavu
Tangawizi kavu, safi za aina za aina zote zisizokuwa na ukungu, zenye rangi moja na ukubwa sawa hupangwa na kuwa za daraja la juu.
Tangawizi zilizovunjika nazo ziwekwe katika daraja moja na mar nyingi ziwekwe daraja la chini.
Kufungasha tangawizi kavu
Tangawizi zilizokaushwa hufungashwa kwenye mifuko midogo ya plastiki yenye ujazo wa kilo 5 hadi 10 au kwenye magunia yasiyozidi kilo 50 kwa urahisi wa kubeba. Ufungashaji wa kupita kiasi husababisha tangawizi kuvunjika na hatimaye kushuka ubora.
Kuhifadhi tangawizi kavu
Tangawizi iliyokaushwa huhifadhiwa katika sehemu kavu, safi na isiyo na mwanga mkali. Katika hali hiyo tangawizi inaweza kuhifadhiwa kwa muda wa mwaka mmoja bila kuharibika.
Matumizi ya tangawizi
Tangawizi kama kiungo ina matumizi mengi kama vile kiungo kwenye vyakula mbalimbali, hutumika katika kutengenezea madawa ya magonjwa mbalimbali na pia kutengenezea vinywaji baridi.
Kusindika tangawizi
Kama ambavyo mazao mengine huweza kusindikwa kwa kuongezewa thamani, tangaziwi pia inaweza kusindikwa kupata bidhaa mbalimbali na kusaidia kuweza kufikia lengo la kilimo biashara.
Kusindika tangawizi kupata unga
Vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kusindika tangawizi kupata rojo ni pamoja na mizani, mashine ya kusaga, mishumaa au mashine ya kufungia mifuko, chekeche, vifungashio, lebo na lakiri.
Malighafi inayohitajika ni tangawizi kavu itakayosagwa kwa ajili ya kupata unga.
Jinsi ya kusindika
- Chagua tangawizi zilizokauka vizuri kisha saga kwenye mashine kwa ajili ya kusaga.
- Chekecha vizuri baada ya kusaga ili kupata unga laini.
- Pima unga huo ili kupata uzito unaohitajika na fungasha kwenye vifuko.
- Weka lakiri na lebo kisha hifadhi kwenye sehemu kavu tayari kwa kuuzwa au kutumika.
Kusindika tangawizi mbichi ili kupata rojo
Vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya usindikaji huu ni pamoja na mashine ya kusaga rojo, mizani na maji.
Malighafi
Hizi ni pamoja na tangawizi mbichi, chumvi (hutegemea matakwa), sodiam benzoate na maji asilimia kumi ya tangawizi.
Jinsi ya kusindika
- Chagua tangawizi bora kisha osha kwa maji safi na menya.
- Saga tangawizi kwa kutumia mashine ya kusaga, ongeza maji kidogo ili kupata rojo.
- Pima uzito wa rojo kisha ongeza chumvi kiasi cha gramu 50 kwa kilo moja ya rojo. Iwapo itatumika kwa chai usiweke chumvi.
- Weka sodiamu benzoate (chumvi maalumu), Hii husaidia tangawizi kuhifadhiwa kisha changanya vizuri ili sodiamu benzoate ikolee vizuri.
- Fungasha kwenye chupa, weka lakiri na lebo kisha hifadhi mahali pasipo na mwanha mkali tayari kwa matumizi.
Naomba utaalam kuhusu uchafushaji wa vanilla
Habari, Asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za Mkulima Mbunifu.
Utaalamu wa uchavushaji wa vanila ni mkubwa sana na unahitaji kujifunza moja kwa moja shambani. Kama uko tayari kujifunza kwa njia ya vitendo unaweza kuwasiliana na Penina Mungure (Mama Kipande) kwa simu namba 0787 202946
Karibu sana Mkulima Mbunifu