- Kilimo, Kilimo Biashara, Usindikaji

Namna ya kusindika korosho mara baada ya kuvuna

Sambaza chapisho hili

Korosho ni zao lenye matumizi mengi sana, lakini kubwa kuliko yote ni kwamba kuliwa kama kitafunwa (snacks) wakati wa kunywa chai, juisi, maziwa au kahawa.

Makala hii inakusudia kutoa mafunzo ya namna ya kuandaa korosho kwa matumizi ya nyumbani. Hii itawasaidia wakulima wapya wa mikoa hasa iliyoingia kwenye uzalishaji wa zao hili kwa mara ya kwanza.

Jinsi ya kuandaa korosho

Korosho zinazoandaliwa kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi au kwa kiwango kikubwa maandalizi yake huitaji mashine kwani zinaandaliwa kiasi kikubwa tofauti na maandalizi kwa matumizi ya nyumbani au kwa biashara ndogo ndogo.

Maandalizi

Kukaanga kwenye moto

  • Andaa korosho kavu kiasi cha kilo nne kisha bangua kupata korosho kilo moja.
  • Andaa mafiga kisha washa moto kwa kutumia kuni ndogo ndogo, mibua ya mahindi au mtama.
  • Chukua kipande cha bati chenye urefu unaokaribia mita moja na upana nusu yake, litoboe bati kwa msumari ili kupata matundu ya kuruhusu moto kupenya, matundu yatobolewe kati ya 20 hadi 40.
  • Weka bati jikoni na utie korosho na endelea kukoleza moto ili uwake na baada ya dakika kadhaa korosho zitakuwa zinavujisha mafuta na kufanya moto kuwasha korosho zilizo juu ya bati.
  • Tumia fimbo ya mti ndefu kugeuza geuza korosho hadi ziwe nyeusi, angalia visiungue.
  • Ipua na uzimwage chini na uzime kwa mchanga au kwa maji, endelea kuweka tena bati jikoni na endelea na mchakato hadi ziishe.
  • Baada ya hapo zibangue moja moja kwa kutumia kipande cha mti na kuzigongea juu ya tofali.

Kuchemsha jikoni

Hii ni njia nyingine ya kuandaa korosho kwa kuzichemsha jikoni

  • Chukua sufuria kubwa, weka maji na injika jikoni kisha chukua korosho weka kwenye sufuria kiasi cha robo tatu ya ujazo wa sufuria hiyo.
  • Funika na uendelee kuchochea kuni hadi maji yaanze kuchemka. Baada ya saa moja na nusu hadi masaa mawili korosho zitakuwa tayari kwa kuipuliwa, lengo la kuchemsha ni kufanya ganda gumu la nje liweze kuwa laini na kurahisiha hatua zinazofuata.
  • Korosho zikishaopolewa kutoka jikoni, zimwage kwenye mkeka au tefu na ziwekwe juani kwa siku mzima.
  • Baada ya kuanikwa juani siku inayofuata ni bangua. Andaa tofali au jiwe na uliweke chini, tumia kipande cha mti kwa ajili ya kubangua korosho, hakikisha mikononi umevaa gloves na uzipake majivu ya jikoni, au kama huna gloves basi lowesha majivu na ujipake kwenye viganya na endelea na kubangua

Kumbuka: Wakati wa kubangua maganda ya korosho yanatoa mafuta na ambayo usipochukua tahadhari yaweza kukuchubua mikononi.

  • Baada ya kuzibangua korosho anika juani kwa masaa kadhaa au hata siku mzima, ukishaziondoa juani anza kuzimenya kwa kuandoa ganda laini la ndani na kubakiza korosho ikiwa nyeupe bila kipande cha ganda.

Kuzioka

Baada ya kuzimenye, oka jikoni ili kukamua au kukausha mafuta yaliyobakia kwenye korosho, weka korosho kwenye chombo maalumu au sufuria kisha injika sufuria jikoni na hakikisha unafunika juu na ikiwezekana palia makaa kidogo juu ya mfuniko kama unavyopika wali kwenye jiko la mkaa.

Zingatia kuwa moto hauhitajiki kiasi kikubwa bali ni joto tu na hatua hii ifanyike walau ndani ya dakika 20 hadi 30 tu kisha ipua jikoni.

Kuoka kwa kutumia chumvi

Korosho zikishamenywa hunyunyiziwa maji yenye chunvi na kisha kuwekwa kwenye chombo na kuzioka. Korosho zilizookwa kwa njia hii huwa na ladha ya chumvi na rangi yake ya weupe huwa ni ya kufifia / rangi ya kikahawia.

Kumbuka: Walaji wengi wa korosho hupendelea kupata ladha ya asili na siyo yenye kuchanganyika na chumvi.

Kupanga katika madaraja

  1. Daraja la kwanza korosho kubwa na nzuri
  2. Daraja la pili korosho za ukubwa kwa wastani za zenye kuvunjika kidogo
  3. Daraja la tatu ni korosho vipande vipande vilivyovunjika. Hizi mara nyingi baadhi ya watu wanatumia kwa ajili ya tui kwenye mboga, kulishia kuku, au kutengeneza vitafunwa kama kashata, nk na zile kubwa ni kwa ajili ya biashara, au zawadi, na wakulima walio wengi wanatumia korosho za daraja la pili kwa matumizi ya nyumbani.

Kufungasha

Fungasha korosho kwenye mifuko kwa ujazo mbali mbali ambao ni paketi ya Kilo 1, ya nusu kilo (gram 500) na pengine paketi ya robo kilo ingawa siyo mara nyingi. Weka lebo kwenye pakiti inayoonyesha jina la mwenye mradi, ujazo, nk.

Kumbuka:

Korosho zinazoandaliwa kwa ajili ya kusafirisha mbali na kwa kiasi kikubwa kunahitajika mashine ya kuondoa hewa kwenye paketi ili kuzuia wadudu wasizaane na unyevu nyevu(moulds) na kuharibu bidhaa yako.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *