- Kilimo

Maparachichi yaliyopandikizwa hutoa mavuno bora zaidi

Sambaza chapisho hili

Msukumo wa uhitaji mkubwa wa parachichi kwa wingi na zenye ubora unawasukuma wakulima kutumia teknolojia mpya.

Upandikizaji hujumuisha aina mbili za mimea. Unachukua mmea mmoja ambao unadhani hauna tija nzuri, na sehemu ya mmea mwingine ambao una ubora zaidi na kupandikiza kwa kukata na kufunga pamoja ili kupata mbegu bora zaidi.

Utaratibu wa kupandikiza hivi sasa umekuwa silaha ya wakulima kuwakomboa dhidi ya wadudu pamoja na magonjwa, na hili kwa sasa halifanyiki tena maabara kama ilivyokuwa awali na hii inadhibitishwa na yale tuliyojionea Njombe tulipotembelea wakulima. Kwenye shamba la bwana Bosco Kidenya, ana kitalu chenye zaidi ya miche 1200 ya miparachichi, baadhi ikiwa tayari imeshapandikizwa na mingine ikiwa inasubiri kufikia wakati wa kupandikiza.

Huyu ni mmoja kati ya wakulima walio wengi wanaofanya kazi kwa karibu na CARITAS Njombe, kuboresha uzalishaji wa parachichi, pamoja na kuboresha kipato cha wakulima ambao wanazalisha matunda na mboga mboga.

Bw. Bosco akionyesha mche wa parachichi uliopandikizwa

Mbinu wanayotumia

Wakulima hukusanya kokwa za parachichi kutoka maeneo ya sokoni; wanachofanya ni kuhakikisha tu kuwa mbegu hiyo ni safi, haijaathiriwa na magonjwa na itaota. Baada ya hapo huchagua zile zenye muundo mzuri na kuzipanda kwenye boksi au kwenye sehemu ya kitalu. Baada ya kuota huziotesha kwenye makopo, au kwenye viriba kisha kuendelea kumwagilia maji mpaka zinapokuwa na umbo usawa wa penseli.

Upandikizaji ni lazima ufanyike wakati mmea umefikisha unene wa penseli. Kupandikiza kwa kutumia chipukizi lililolingana na mche unaopandikizia ni njia yenye mafanikio zaidi. Upandikizaji ni lazima ufanyike wakati ambao mizizi bado ni laini. Pandikizi litakalotumika wakati wa kupandikiza ni lazima lisiwe katika hatua ya ukuaji kwa wakati huo, na ni lazima umbo liwiane na mti linapopandikizwa. Funga vizuri kwa kutumia nailoni ili kuzuia maji yasipotee na kusababisha pandikizi kukauka.

Mapandikizi ni lazima yatokane na aina ya parachichi ambazo zimeboreshwa kama vile hass, fuerte au pueblo. Kwa wale wakulima ambao wana mkataba na Africado, watahitaji kupata mapandikizi kutoka kwenye miti ya hass. Hii ina maanisha kuwa mkulima anayetaka kuanzisha kitalu kwa ajili ya kupandikiza ni lazima apande walau miti 5 ya parachichi aina ya hass ili kupata mapandikizi.

Njia ya kupandikiza ina ufanisi zaidi na ni rahisi kuliko kupanda miche upya, kwa kupandikiza inagharimu chini ya asilimia 75, kuliko kupanda miche upya na kuweza kupata aina ambayo inastahimili magonjwa. Wakulima pia wamekuwa na rikodi nzuri ya ongezeko la mavuno kutokana na mimea waliyopandikiza, pamoja na upungufu wa matumizi ya madawa.

Wakulima ambao wanafanya kazi zao chini ya CARITAS Njombe sasa wanaona faida kubwa inayotokana na kupandikiza, wameamua kuwekeza kwenye utaalamu huu na kuwa na miche mingi kwenye vitalu vyao. Hii ni mbinu ya kilimo ambayo ina faida kubwa kwa mkulima, huku akiwa amewekeza kwa kiasi kidogo sana katika kukabiliana na wadudu na magonjwa na kuepuka kuwa na mazao yenye ubora wa chini.

Taarifa hii imeandaliwa kutokana na tuliyojionea tulipomtembelea shamba la bwana Bosco Kidenya kutoka Njombe, ambaye ni msomaji mzuri wa jarida la Mkulima Mbunifu. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 753431117.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

4 maoni juu ya “Maparachichi yaliyopandikizwa hutoa mavuno bora zaidi

    1. Hbari, Karibu saa Mkulima Mbunifu. Ni rahisi sana kwani utafuata taratibu hizohizo za kupandikiza parachichi kuanzia kutafuta kikonyo kwenye mti unaopenda na wenye sifa zote za kuzalisha halafu utapandikiza kwenye mlimao.

  1. Habari za leo
    Nilibebesha miparachichi yangu kama 102 hii lakini ajabu ni kwmaba hakuna hata mmoja uliochipua. Niliibebesha tarehe 27 Feburuari 2022 mpaka muda huu ninaandika email hii yote imekauka imebaki kamam mimme tu ambayo inaubichiubichi nayo ninasubiria kuona kama itachipua au la.

    Nilipanda makokwa nilyookota sokoni harafu vikonyo niliagiziwa na mtu kutoka iringa, sijui nilikosea wapi katika kubebesha maana kabla ya hapo nilienda iringa kujifunza jinsi ya kubebebsha na nilifuata hatua zilezile nilizofundishwa.

    Ninatanguliza shukrani 0754838585 au 0655113388

    1. Habari Eliphas

      Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa swali lako lakini pia pole sana kwa changamoto hii.

      Kabla sisi hatujakushauri ni vyema ungwasiliana na wale waliokupa mafunzo ya ubebeshaji wa miche huenda kuna kitu umekosea katika kupandikiza.

      Lakini pia kama hujakosea, huenda ulipokea vikonyo ambavyo tayari vimeshaanza kukauka labda kutokana na umbali wa kusafirisha na siku iliyovunwa au katika utunzaji hukumwagilia miche yako kupata maji ya kutosha.

      Lakini pia huenda ulifunga sana miche ikapelekea kukauka.

      Hivyo, ni muhimu kufanya tathmini ya awali kwa kuwasiliana na wale waliokufundisha namna ya kubebesha.

      Karibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *