- Kilimo, Udongo

Maandalizi ya udongo kwa ajili ya kusia mbegu

Sambaza chapisho hili

Wakulima wengi hawaelewi ubora na umuhimu wa kuandaa udongo maalumu kwa ajili ya kusia mbegu za mazao mbalimbali kabla ya kuzipeleka shambani hasa mazao ya bustani.

Si kila udongo unafaa kwa ajili ya kusia mbegu. Kuna udongo maalumu unaostahili kutumika kwa ajili ya kusia mbegu, ambao mkulima yeyote anaweza kuutafuta na kuandaa mwenyewe kwa ajili ya matumizi hayo.

Bila kutumia udongo ulioandaliwa vizuri na maalumu kwa ajili ya kusia mbegu, ubora wa miche tarajiwa pamoja na uotaji unakuwa hafifu na hata miche ikipelekwa shambani, itakuwa imepoteza ubora wake na uzalishaji wa mazao utakuwa wa kiwango cha chini.

Huu ni udongo wa aina gani

Udongo mzuri ambao unafaa kwa ajili ya kusia miche na unapatikana kwa urahisi ni kutoka msituni au kutoka chini ya miti mikubwa, ambao umetokana na mazalia ya majani na vijiti vilivyo oza na kuwa udongo, ikiwemo vinyesi vya ndege.

Kwa maana hiyo, mkulima anapokuwa tayari kusia mbegu, ni lazima ahakikishe anatafuta udongo wa aina hii mahali unapopatikana tayari kwa ajili ya kusia mbegu.

Namna ya kuandaa udongo

Pamoja na kuwa udongo huu una ubora unaostahili kwa ajili ya kusia mbegu, lakini kuna namna inatakiwa uandaliwe ili kuua baadhi ya vijidudu ambavyo huenda vikawa na madhara kwa mbegu au miche, lakini pia kuufanya udongo uwe na ubora zaidi.

Vifaa na vitu vinavyohitajika kwa ajili ya kuandaa

Mchanga mwekundu, mfuko wa sulfate, sufuria au pipa, maji, ndoo/debe la lita ishirini (kwa ajili ya kupimia), jiko na beleshi/shepe.

Hatua za kuuandaa ni kama zifuatazo;

  • Pima udongo kiasi cha debe moja na pima mchanga mwekundu kiasi cha beleshi moja (kilogramu mbili).
  • Changanya vizuri udongo na mchanga huku ukiondoa takataka ngumu kama vile miti na mawe ikiwa udongo wako una taka hizo.
  • Udongo ukishachanganyika vizuri, na taka zote ngumu zikiwa zimetoka, weka kwenye mfuko wa sulfate na funga vizuri.
  • Chukua sufuria kubwa au pipa kisha jaza maji na injika jikoni, na uchemshe vizuri mpaka yaanze kufoka.
  • Maji yakiwa tayari, gawa nusu ili kuwepo na nafasi ya kuweza kutumbukiza mfuko bila maji kumwagika.
  • Chukua udongo uliouandaa na tumbukiza kwenye maji yaliyoko kwenye sufuria au pipa kwa kusimamisha mdomo wa mfuko ukiangalia juu, na fungua mfuko huo huku ukishikilia udongo usimwagikie kwenye maji.
  • Chukua yale maji uliyoyagawa, na anza kutilia kwenye mfuko taratibu huku ukihakikisha hayajai kwenye sufuria au pipa na kuanza kumwagika.
  • Ukiona maji yamefika juu kabisa mwa sufuria, acha na funga mfuko wa udongo vizuri ukiwa bado kwenye pipa/sufuria kisha weka sufuria hiyo sehemu patulivu penye kivuli na acha kwa siku mbili hadi tatu mpaka utakapoona udongo umenyonya maji yote.
  • Baada ya siku ya tatu, chukua na fungua mfuko kuangalia kama udongo bado una tope sana, na kama umekauka maji lakini kuna kaubichi kidogo, basi udongo wako uko tayari kwa ajili ya kutumia kusia mbegu.
  • Udongo huo unaweza kutumika siku yeyote ama ata ukahifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye maadamu tayari umeshatengenezwa kwa hatua hizo.

Namna bora ya kusia mbegu kwa kutumia udongo huu

Ili udongo huu uweze kuonyesha ubora zaidi katika usiaji wa mbegu na ukuzaji wa miche, mkulima hana budi kutumia trei maalumu zinazotumika kwa ajili ya kukuzia miche. Trei za kukuzia miche ziko za aina nyingi na zimetofautiana kulingana na idadi ya matundu ama idadi ya miche inayoweza kuchukuliwa na trei hiyo

Namna ya kuandaa trei kwa ajili ya kutumia kusia mbegu

Vifaa

Maji, trei zenyewe na sabuni ya unga.

Hatua

Weka maji katika chombo kikubwa chenye uwezo wa kutumbukiza trei kama vile beseni kubwa, kisha changanya na sabuni ya unga kiasi kidogo. Chukua trei zote unazotegemea kuzitumia kusia mbegu, moja baada ya nyingine na kisha tumbukiza kwenye maji hayo, huku ukihakikisha trei lote na tundu zote zinapata maji kisha toa na weka pembeni.

Kutumbukiza trei kwenye maji yenye sabuni husaidia kuua vimelea ambavyo si rafiki kwa mbegu au miche.

Namna ya kuweka udongo kwenye trei

Chukua turubai au mfuko kubwa wa nailoni na tandaza, kisha mimina udongo wako uliouandaa kwenye upande mmoja wa turubai na anza kujaza udongo kwenye matundu ya kila trei.

Hakikisha unapoweka udongo kwenye trei, udongo huo unajaa kwenye kila tundu lakini bila kushindiliwa kwani ukishindilia utakuwa mgumu, na itakuwa kazi kupandikiza mbegu na hata kupitisha maji wakati wa kumwagilia mbegu hizo au miche yako hapo baadaye.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *