- Kilimo

Lima Giligilani kukuza uchumi kwa haraka

Sambaza chapisho hili

Kilimo cha Giligilani (Coriander) ni mradi mkubwa unaojitosheleza kukuza maisha ya mkulima kutokana na sababu kuwa zao hili la biashara huchukua muda mfupi toka kuotesha hadi kuvuna.

Zao hili linalotumika kama kiungo cha chakula katika mapishi ya vyakula mbalimbali kama nyama, supu au mchuzi linafaa kulimwa wakati wowote na katika maeneo mengi ya Tanzania hususani mikoa ya Mbeya na Iringa.

Uhitaji mkubwa wa walaji pamoja na urahisi wa kuzalisha zao hili katika maeneo mbalimbali nchini, umewezesha wakulima kupata soko zuri na kujiongezea kipato kwa urahisi zaidi.

Aina za Giligilani.

Kuna aina kuu mbili za giligilani ambazo ni:  Giligilani fupi na ndefu. Aina zote hizi zinatumika kwa wingi na zinauzika katika masoko yote.

Giligilani fupi: Aina hii ni nzuri kwa mkulima yeyote anayetaka kulima kwa lengo la kuvuna mbegu. Hii ni kutokana na sababu kuwa inatoa maua ikiwa fupi na  inakomaa kwa haraka na mbegu zake huwa nyingi. Aina hii si nzuri sana kwa kilimo cha kuvuna majani.

Giligilani ndefu: Hii ni aina ya giligilani ambayo ni bora kwa ajili ya kilimo cha kuvuna majani lakini pia mbegu zake hufaa kwa viungo. Aina hii hurefuka zaidi kabla ya kutoa maua na mbegu zake ni chache.

Hali ya hewa

Giligilani hustawi katika maeneo yote ya Tanzania, yenye joto lisilozidi nyuzi 20C hadi 25C, kiasi cha mita 1000 hadi 1800 kutoka usawa wa bahari. Pia hustawi katika maeneo yenye nyuzi joto zaidi ya 25C kwa kulima wakati wa mvua ambapo joto huwa limepungua. Hata hivyo, mikoa ya Mbeya na Iringa ni maeneo mazuri zaidi kulima zao hili kulingana na hali ya hewa ya ubaridi katika msimu wote wa mwaka.

Udongo

Zao hili linastawi katika udongo wa aina yoyote lakini hustawi vizuri zaidi katika udongo tifutifu (Loam soil) na udongo wa kichanga (Sand soil).

Utayarishaji wa shamba

Hakikisha shamba lako limelimwa vizuri, limenyeshewa vizuri na lina mbolea ya kutosha kabla ya kupanda.

Mbolea

Mboji inafaa zaidi kwa ajili ya kurutubisha udongo na kuongeza mavuno. Baada ya siku mbili toka kumwagiliwa, tifua tena kwa kutumia rato, kisha sawazisha vizuri kuondoa mabonde na kisha sia mbegu za giligilani.

Uoteshaji

Uoteshaji wa giligilani hutegemea umekusudia kuvuna nini au ni aina gani ya giligilani unaotesha. Mfano, mkulima anaweza kuwa anakusudia kuzalisha mbegu au kuvuna giligilani ikiwa majani kwa ajili ya kutumika kama kiungo.

Unaweza kuotesha giligilani kwa kusia shambani moja kwa moja.

Uoteshaji kwa ajili ya kiungo

Endapo unakusudia kuzalisha giligilani kwa ajili ya kuvuna majani ambayo hutumika kama kiungo kwenye chakula, ni lazima uoteshe giligilani ndefu na unatakiwa kusia kama unavyosia mbegu za mchicha ila hakikisha mbegu hizo hazitarundikana mahali pamoja.

Uoteshaji kwa ajili ya mbegu

Endapo unakusudia kuvuna mbegu kwa ajili ya kiungo, unatakiwa kuotesha giliglani fupi ambayo mbegu zake hupandwa kwenye mashimo.

Nafasi

Umbali wa shimo hadi shimo liwe sentimita 10-15 na umbali kati ya mstari na mstari iwe ni sentimita 20.

Kuota

Giligilani huanza kuchipua kuanzia siku ya 8 hadi 15 toka kuoteshwa. Hakikisha katika siku 12 za mwanzo unamwagilia kila baada ya siku mbili, na baada ya hapo unaanza kumwagilia kila wiki mara mbili au tatu. Ikiwa mvua zinanyesha, hakuna haja ya kumwagilia.

Kukomaa na kuvuna

Giligilani hukomaa vizuri baada ya siku arobaini (mwezi na siku kumi) na hapo huwa tayari kwa kuvunwa.

Kama unakusudia kuvuna majani, hakikisha unaanza kuvuna kabla ya kuanza kutoa maua au mara baada ya kufikia urefu wa sentimeta 20. Hakikisha unang’oa wakati wa asubuhi kwa kung’oa mche pamoja na mizizi yake kisha kuziosha ili kuondoa udongo wote. Baada ya hapo, funga kulingana na soko husika.

Ikiwa unakusudia kuvuna mbegu, hakikisha mbegu zimekomaa kwa kubadilika rangi na kuwa kahawia. Ng’oa miche na rundika mahali pasipokuwa na maji au unyevu kwa muda wa siku saba, kisha zipige polepole hadi mbegu zote zitoke katika majani, pepeta na paki tayari kwa kuuza.

Magonjwa na udhibiti

Giligilani tofauti na mazao mengine mara nyingi halisumbuliwi na magonjwa kabisa. Mara chache sana zao hili hushambuliwa na ukungu ambao husababishwa na wingi wa maji shambani hasa linapooteshwa wakati wa mvua kubwa na wakati wa baridi kali.

Hakikisha unamwagilia kwa kiwango cha wastani huku ukiepuka kuotesha wakati wa mvua nyingi na wakati wa baridi kali.

Kwa mawasiliano zaidi unaweza kuwasiliana na Bw.Jonas Sabaya kwa simu namba +255767647846

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

4 maoni juu ya “Lima Giligilani kukuza uchumi kwa haraka

      1. Habari,
        Karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa kufuatilia na kusoma makala zetu. Unaweza ukaanza kulima kwa kufuata hatua za msingi tulizoainisha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *