- Kilimo

Jarida la Mkulima Mbunifu ni darasa tosha la kilimo hai

Sambaza chapisho hili

“Mimi nilipata jarida la Mkulima Mbunifu mwaka 2017 Disemba kwenye maonyesho ya wakulima lakini mara baada ya kufika nyumbani sikulisoma nikaliweka kabatini wala sikufikiri kama linaweza kunisaidia kwa lolote, nilipokea kama kipeperushi tu”.

Hayo ni maneno ya Bi. Magreth Leandry kutoka Kijiji cha Slahamo ambaye ni mfugaji lakini pia mkulima wa mazao mbalimbali kwa misingi ya kilimo hai.

Bi. Magreth ni mmoja wa wadau wa kilimo hai ambaye anajishughulisha na kilimo cha migomba, mbogamboga pamoja na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kuku.

Kabla ya kufikiwa na elimu hii, Bi. Magreth anasema, alikuwa akizalisha kwa njia za kienyeji/asili lakini hakuwa akipata mavuno mengi kwani alilima mazao mengi katika eneo moja kwa kuchanganya bila mpangilio hivyo mimea kuzidiana katika utafutaji chakula na mwishowe kukosa mavuno katika mazao mengine au kupata mavuno haba.

Alijifunza nini kupitia Mkulima Mbunifu

“Katika shughuli zangu za kilimo na ufugaji, nilikuwa nikitegemea kuuliza kila kitu toka kwa wataalamu na wakati mwingine kukwama au kupata hasara hasa pale ambapo mtaalamu hapatikani kwa wakati.

Nilishikwa butwaa pale nilipofungua jarida la Mkulima Mbunifu nikakuta taarifa nilizokuwa nazihitaji za kilimo na ufugaji zipo tena zimeandikwa kwa lugha rahisi kiasi kwamba ukifuata maelezo hayo huitaji tena kuwa na mtaalamu.”

Bi. Magreth anasema kuwa, katika jarida moja tu la disemba 2017, alikuta kuna taarifa juu ya ufugaji wa kuku yaani namna na mifumo ya ufugaji, faida zake na hasara hivyo ni rahisi sana kwa mfugaji kuchagua mfumo atakaotumia lakini pia kufanya ufugaji wenye tija.

Bi. Magreth aliongeza kuwa, pamoja na taarifa zingine nyingi kulikuwa na taarifa juu ya malisho ya glirisidia na namna ya kusindika ili kupata chakula mbadala cha kulishia kuku na tayari ameotesha mti wa gliricidia.

Mama huyu anasema kuwa, kama jarida moja tu, limeweza kusheheni mambo lukuki, je, ukiwa unapata jarida la kila mwezi si zaidi?

Nini anazalisha katika kilimo hai

Bi. Magreth anasema kuwa, kupitia elimu ya kilimohai ameweza kujifunza namna ya kuzalisha mazao mbalimbali kama ifuatavyo;

  • Kuzalisha mahindi na kupata mavuno mengi pamoja na chakula kwa ajili ya ng’ombe na mbuzi.
  • Kuanza uzalishaji wa mbogamboga kwa kutengeneza bustani ya jikoni.
  • Kuotesha malisho aina ya glirisidia kwa ajili ya kulisha kuku na ng’ombe.
  • Kuanza ufugaji wa kuku na mbuzi.
  • Kupanua mradi wa ufugaji wa ng’ombe mpaka kufikia ng’ombe 8.
  • Uzalishaji wa miti kwenye vitalu kwa kupandikiza mbegu kisha kuuza miche.
  • Uzalishaji wa mazao kwa kutumia umwagiliaji wa matone.

Faida za kilimohai

Bi. Magreth anaeleza kuwa, faida kubwa anayoipata kupitia kilimo hai ni kuzalisha mazao ya aina mbalimbali katika eneo moja kwa mpangilio kwa njia ya kilimo.

Pili, kupata mazao salama yasiyokuwa na sumu kwani malighafi zinazotumika ni za asili na salama kwa afya ya mwanadamu, mimea, wanyama na mazingira kwa ujumla.

Bi Magreth akionyesha baadhi ya makopo anayotumia kwa ajili ya kukuzia miche ya miti

Aidha, anaongeza kuwa, badala ya kununua mbogamboga toka sokoni na ambayo hana uhakika nayo kama ni salama, sasa anazalisha mboga mwenyewe kwa kutumia bustani ya jikoni na pia anapata nyama na mayai kutokana na kuku anaowafuga.

Bi. Magreth anaongeza kuwa, kupitia kilimo hai, ameendelea kuzalisha na kupata malisho kwa ajili ya mifugo yake kutokana na migomba, mahindi, maharage lakini pia kwa kuotesha miti ya sesbania na glirisidia.

Wito kwa wakulima

‘’Mimi ningewashauri tu wakulima wenzangu, jarida la Mkulima Mbunifu pekee linaweza kukufanya ukawa tajiri mkubwa sana bila kutumia gharama kutafuta huduma lakini pia elimu inayotolewa ni ya kumsaidia mkulima wa chini kuzalisha kwa gharama nafu hivyo kila mkulima ahakikishe anapata nakala yake kila mwezi” alisema

Bi Magreth akiwa katika eneo lake la bustani ya jikoni analoandaa kwa ajili ya kuotesha mbogamboga

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *