- Kilimo

Fahamu kuhusu mazao funika (Cover Crops) na faida zake katika kilimo

Sambaza chapisho hili

Mazao funika ni aina ya mazao ambayo huoteshwa ili kufunika udongo na kwa lengo la kuongeza rutuba ya udongo na kuzalisha chakula na malisho.

Mazao funika huoteshwa wakati wa kiangazi au huoteshwa pamoja na zao kuu wakati wa msimu wa kulima.

Mazao haya huweza kuachwa kuendelea kuota katika msimu wote wa mazao mseto au yanaweza kungolewa na kuachwa juu ya ardhi kama matandazo.

Kuna aina nyingi za mazao funika yanayopatikana katika Afrika. Aina zote hizo zimegawanywa na kuwekwa katika makundi manne, ambayo ni mazao funika jamii ya mikunde, vichaka, nyasi na mengineyo.

Mkulima atahitajika kuchagua aina ya mazao funika yanayosadifu wingi na ubora wa matandazo yatakayotoa.

Baadhi ya wakulima pia huotesha pamoja maharagwe na mahindi, ambapo maharagwe huwa kama moja ya mazao funika kwa kipindi fulani cha mwaka.

Namna sahihi ya kuchagua mazao funika

Wakulima wadogo walio wengi wanapendelea zaidi mazao funika ambayo huzingatia mfumo wao wa sikuzote wa kilimo ambao unalenga mambo mengi kama vile; kurutubisha udongo, malisho ya wanyama, dawa, mbegu na mbogamboga, mahitaji kwa ajili ya uzio, kupunguza palizi.

Ili kuotesha mazao funika sahihi mkulima anahitajika kuangalia mambo yafuatayo;

  • Aina gani ya mazao funika huota vizuri katika eneo lako: Hii hutegemeana zaidi na aina ya udongo, mvua, joto na mwinuko kutoka usawa wa bahari. Endapo mkulima anaishi katika eneo lenye mvua kidogo basi utahitajika kuchagua aina ya zao funika ambalo huota kwa muda mfupi sana kama vile desmodium, labalab, lucerne, mucuna, pigionpea na cowpea.
  • Kujua zao funika ulilochagua linahitajia uangalizi kiasi gani: Hii ni kuanzia maandalizi ya shamba kabla ya kuotesha, palizi, uzalishaji na uvunaji. Aina zile zenye maganda na nafaka kubwa/nene kama vile pigeonpea na mukuna ni rahisi sana kutunza kuliko zile zenye maganda madogo kama vile nyasi. Wakulima walio wengi hupendelea zaidi mazao funika yenye yanayofunika udongo kwa haraka na moja kwa moja na yanayoweza kutumika kama chakula na malisho kwa wakati mmoja.
  • Hakikisha zao funika utakalootesha halitasumbuana na zao kuu. Kwa mfano, ni muhimu kuhakikisha huoteshi zao funika ambalo litaweka kivuli kwenye zao kuu. Aidha, ili kuondokana na zao kuu kusumbuliwa na zao funika, unaweza kuotesha zao funikizi baada ya kupita muda kidogo kuotesha zao kuu.
  • Ikiwa huhitaji mifugo kuingilia katika shamba lako, basi ni muhimu pia kuhakikisha unaotesha zao funika ambalo mifugo hawatapenda kulila kama vile Jackbean (Canavalia).

Baadhi ya mazao funikizi huoza haraka sana kuliko mengine mara yanapokufa. Aidha, mikunde hutengeneza mbolea haraka kuliko nyasi, hivyo ni rahisi sana kwa mmea utakaofuata kuoteshwa kupata virutubisho kama vile naitrojeni kwa haraka zaidi.

Mchanganyiko wa mikunde na nyasi ni njia nzuri zaidi ya kutengeneza udongo wenye rutuba ya kudumu.

Ni wakati gani sahihi kuotesha mazao funika

Mazao funika huweza kuoteshwa kwa njia mbalimbali kama zifuatazo;

Kilimo mseto

Unaweza kuotesha mazao funika kama zao kuu. Njia hii ni rahisi sana kwani husaidia kupata mazao yote kwa pamoja (zao funika na wakati huohuo zao kuu), na hufanya vizuri katika eneo lenye baridi au baridi kiasi. Aidha, huwezi kuotesha zao funika kwa mtindo huu kama tayari umeshachanganya nafaka (kwa mfano mahindi na maharagwe).

Kuotesha kwa kufuatanisha

Unaweza kuotesha zao funika mara baada tu ya kupalilia zao kuu, na njia hii hufanya vizuri pia katika eneo lenye baridi au baridi kidogo.

Katika kuotesha zao funika mara tu baada ya palizi mara nyingi hufanyika kati ya wiki ya nne toka kuotesha kwa zao kuu. Na ikiwa umechanganya mahindi na maharage, basi zao funika unaweza kuliotesha mara tu baada ya kuvuna maharage.

Kufuata kilimo cha mzunguko

Aidha, katika maeneo yenye ukame, unaweza kuotesha zao funika mara tu baada ya kuvuna zao kuu, hii itasaidia kuzuia zao funika kushindania unyevu pamoja na zao kuu. Unaweza pia kutumia zao funika kupata matandao ya ziada ama chakula cha mifugo.

Kwa wakulima wanaoishi katika maeneo ya nusu jangwa ambapo wana msimu mmoja tu wa kulima, basi wanaweza kuotesha zao funika linalohimili ukame kama vile lablab kwa kupanda katika ya mistari ya mahindi.

Mara baada ya kuvuna mahindi, acha zao funika liendelee shambani hivyo kusaidia kufunika udongo na kuzuia magugu. Kabla ya msimu wa pili wa mvua, fyeka ama ondoa kabisa kisha yaweke kama matandazo.

Namna ya kuotesha mazao funika

  • Kama ilivyobainishwa hapo juu, unaweza kuotesha mazao funika kwa namna moja wapo utakayochagua kuendana pia na hali halisi ya eneo ulilopo.
  • Kwa zao funika lenye mbegu kubwa, otesha kwa kutumia jembe la mkono au jembe la kukokota na wanyama.
  • Kwa zao funika lenye mbegu ndogondogo unaweza kusia moja kwa moja kwenye udongo ikiwa tu udongo si mwepesi sana. Na ikiwa udongo utakuwa mwepesi, basi sia mbegu kwa kuweka kwenye mistari kwa kutumia mikono au tumia chombo cha kusia mbegu.

Nafasi na idadi ya mbegu hutegemeana na sababu mbalimbali.

  • Tumia nafasi nyembamba kwa zao funika lenyewe na nafasi pana katika mfumo wa kilimo mseto.
  • Tumia nafasi pana katika maeneo kame ili kuzuia mimea kupambana katika kushindania unyevu.
  • Idadi ya mbegu katika shimo hutegemeana sana na kiasi cha unyevu kilichopo; weka mbegu chache katika eneo kame na mbegu nyingi katika eneo lenye ubichi, kwa ujumla unaweza kuweka mbegu 2 hadi 4 katika shimo.

Je, mazao funika yanahitaji palizi?

Kama yalivyo mazao mengine, mkulima pia anahitajika kupalilia mazao funika mara tu yanapoanza kukua na mara tu yanapoanza kufunika udongo, zao funika litazuia lenyewe magugu kuota.

Ikiwa utaotesha mazao funika kwa wakati mmoja au kwa kufuatanisha na mahindi, basi huna budi kupalilia mara tu zao kuu (mahindi) linapohitaji kupaliliwa. Hakikisha zao funika halitafungamana/songamana na zao kuu.

Kudhibiti wadudu na magonjwa

Kwa maeneo mengi nchini, wakulima wengi huotesha lablab kama zao funika. Aidha, kwa baadhi ya vijiji, maeneo mengi yametawaliwa na zao la aina moja, na kwa maana hiyo wakulima hawa huweza kuwa hatarini kwa kuvamiwa na ugonjwa unaoweza kuharibu mazao funika.

Namna ya kuondokana na hatari ya magonjwa na wadudu

  • Fanya kilimo mzunguko kwa aina ya mazao unayootesha yaani mazao ya chakula, mazao funika, na mazao ya biashara.
  • Chagua mazao funika ambayo ni kinzani kushambuliwa na wadudu.
  • Otesha aina mbalimbali ya mazao funika katika shamba lako.
  • Tumia dawa za asili kunyunyizia katika mazao yako funika.

Uvunaji na uhifadhi wa mbegu

Vuna mbegu zilizokomaa kabla hujafyema mazao funika kwa ajili ya kufanya matandazo. Uvunaji wa mbegu hufanyika kwasababu kuu mbili; Moja ni kwa ajili ya kuotesha kwa msimu ujao wa kilimo kama chakula au malisho na pili kuvuna mbegu kwa ajili kuuza kwa wakulima wengine.

Namna ya kutunza mbegu za mazao funika

  • Kusanya mbegu kutoka katika mimea tofauti ili uweze kuwa na aina mbalimbali za mbegu.
  • Kausha mbegu na weka dawa ya kuhifadhia, na kama mbegu hutumika kama chakula basi hakikisha dawa utakayoweka haiwezi kuleta madhara.
  • Mbegu kwa ajili ya kuotesha ziwekwe katika mifuko yenye mdomo wa kufungua na kuwekwa katika stoo yenye hewa ya kutosha.
  • Hakikisha unatoa mbegu nje kila baada ya muda fulani na kukausha tena kisha kutoa mbegu zozote utakazoona zina tatizo.

Mazao funika yanayolimwa Tanzania na faida zake

Lablab

  • Lablab sifa yake kubwa huota haraka na kufunika udongo na kuzuia kuota kwa magugu.
  • Ni rahisi kutunza na humudu sana ukame.
  • Hutoa malisho kwa wanyama na pia soko zuri na la uhakika.

Mucuna

  • Huota haraka sana hivyo pia kufunika udongo na kuzuia uotaji wa magugu.
  • Ni rahisi sana kutunza na kwa kuwa huteketea wakati wa kiangazi basi mkulima hana budi kuziteketeza mapema kabla ya kuotesha zao lingine.
  • Ni malisho kwa ajili ya mifugo.
  • Huzalisha mbegu nyingi ambazo ni rahisi pia katika kukusanya.
  • Wakulima wengine hutwanga mbegu zake na kuchanganya na makapi ya mahindi kisha kulisha maksai.

Pigeonpea

  • Kwanza ni zao la kibiashara na ni zao la chakula.
  • Huzuia ardhi kuharibika kutokana na malisho na lina soko hata nje.
  • Mbegu zake zinapatikana kwa urahisi lakini pia shina lake hutumika kama kuni.

Pumpkins

  • Ni zao la chakula la asili linaloweza kuoteshwa pamoja na mahindi.
  • Hufunika udongo na kuzuia kuota kwa magugu.
  • Mbegu zinapatikana kwa wingi na kwa gharama nafuu.
Zao funika aina ya maboga ni nzuri sana kwani hurutubisha ardhi na ni chakula pia

Kutumia zao funika kwa chakula na malisho

Kilimo cha mazao funikizi ni kigeni sana hasa kwa wakulima wanafanya kilimo hifadhi. Aidha, baadhi ya mazao funika kama vile Canavalia huhitaji kwa kukaushwa kabla ya kulisha mifugo. Jinsi wakulima wengi wanapohamia na kufanya kilimo hifadhi basi  ni rahisi pia kuwauzia mbegu za mazao funika aidha majirani zako au hata kwa kupeleka sokoni.

Baadhi ya mazao funika hutumika kama chakula na malisho pia.

Aidha, mifugo huweza kulisha malisho kutokana na mazao funika moja kwa moja bila kukausha japo kuna baadhi ambayo ni muhimu sana kuyakausha kwanza kama vile jackbean.

Mbegu zitokanazo na labalab, lucerne, pigeopea, na cowpeas huweza kupikwa na kutumiwa kama chakula ikiwa ni sehemu mojawapo ya lishe kwa binadamu.

Changamoto katika kufunika udongo

Kuna baadhi ya changamoto zilizopo katika ufunikaji wa udongo lakini pia kuna namna ya kukabiliana nazo.

Maeneo yenye mvua kidogo

Katika maeneo yenye mvua kidogo ambapo mara nyingi hunyesha kwa msimu mmoja tu, kutekeleza mbinu ya zao funika ni ngumu kwa kiasi fulani.

Hii ni kutokana na sababu kuwa, mazao, miti na hata vichaka hubakiza masalia machache sana na ambayo wakulima hutumia kwa ajili ya kulishia mifugo na hata kujengea nyumba huku mazao funika yakihitaji maji.

Kwa maana hiyo, ni ngumu sana kufunika udongo kwa mwaka mzima hivyo ni lazima kujikita zaidi katika masalia ya mazao au kupruni miti na vichaka kisha kutumia kama moja ya njia ya kufunika udongo.

Magonjwa na wadudu

Aidha, magonjwa na wadudu huweza kushambulia zao funika hivyo kuhitaji uangalizi wa hali ya juu. Wakulima walio wengi hutumia moto kuteketeza wadudu na magonjwa jambo ambalo huharibu udongo kwa kuua viumbe hai wanaohitajika katika udongo.

Panya

Mazao funika mazito huhamasisha uwepo wa panya kwa wingi kitu ambacho hupelekea kuharibu mazao.

Jambo la msingi ni kupunguza mazao funika yanayokaribiana sana na ardhi kabla ya kuotesha zao kuu. Ni vizuri pia kama utaweza kuwatega panya kwa kutumia sumu.

Aidha, kufanya kilimo cha mzunguko pia husaidia kufukuza panya kwa njia hii husaidia sana kuharibu upatikanaji wa chakula chao lakini pia huharibu mfumo wao wa maisha.

Mchwa

Wakulima walio wengi huogopa kuwa mazao funika huweza kuvutia mchwa shambani.

Aidha, mchwa ni muhimu sana kwani hutumika wakati mwingine kuvunjavunja mabaki ya mimea juu ya uso wa ardhi na hata kupeleka ndani ya udongo ambapo huongeza viumbe hai. Pia, husaidia kulainisha udongo na kufanya maji kupenya ardhini kwa urahisi.

Aina nyingi za mchwa zina faida sana, ni baadhi tu ndiyo ambao huathiri mimea ambapo wanaweza kula mashina au kuharibu nafaka nah ii mara nyingi hutokea katika msimu wa mavuno.

Hata hivyo kwa kuacha mabaki ya mazao funikiza juu ya ardhi itasaidia sana mchwa kula kuliko kuharibu zao kuu. Mazao yanaweza pia kuvunwa kabla mchwa hawajaanza kufanya uharibifu.

Moto

Uchomaji mbaya mashambani au kwenye mashamba yanayopakana huweza kusambaa na kuingia katika eneo linalofanywa kilimo hifadhi na kuharibu udongo uliofunikwa.

Kama wakulima wengi wakifanya kilimo hifadhi, basi uchomaji utakuwa mdogo sana.

Kwa maelezo zaidi kuhusiana na makala hii ya mazao funika unaweza kuwasiliana na mtaalamu wa kilimo Bi. Lucy Mvungi kwa simu +255755 565 621

 

 

 

 

 

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *