- Kilimo, Kilimo Biashara

Ahamasika kufanya kilimo hai baada ya kusoma jarida la MkM

Sambaza chapisho hili

‘’Nimejifunza mambo mengi toka jarida la Mkulima Mbunifu hasa kuzalisha kwa misingi ya kilimo hai na nimeweza kutekeleza kwa vitendo ili wengine wajifunze kutoka kwangu”.

Hayo ni maneno ya Bw. Kastuli Paulo toka kijiji cha Tumati, Wilaya ya Mbulu (Arusha), mkulima wa kilimo hai ambaye anajishughulisha na uzalishaji wa mazao mbalimbali kama vile viazi mviringo, mboga za majani ikiwamo chainizi, sukuma wiki, kilimo cha migomba, ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kuku.

Bw. Kastuli anasema kuwa, kupitia jarida la Mkulima Mbunifu amehamasika sana kufanya uzalishaji kwa misingi ya kilimo hai hususan kutokana na faida alizojifunza kupitia jarida hili.

Maisha kabla ya kilimo hai

Bw. Kastuli anasema kuwa, huko nyuma kabla ya kupata jarida la Mkulima Mbunifu alikuwa akizalisha kwa kutumia kemikali za viandani ikiwa ni pamoja na sumu kupambana na wadudu, magonjwa pamoja na mbolea za kukuia mimea.

‘’Nilifanya uzalishaji kwa misingi hii kwa muda mrefu lakini sikuwa nikipata mavuno mengi na ikiwa nitapata mavuno mengi basi gharama niliyotumia lazima ilikuwa kubwa kwani pembejeo za kilimo ziliuzwa kwa bei kubwa lakini ilitakiwa nitumia kiasi kikubwa ili niweze kunufaika’’.

Alianzaje kilimo hai

‘’Nilianza kupokea majarida ya Mkulima Mbunifu mwaka 2020 kupitia MVIWAMA. Niliposoma baadhi ya makala nilihamasika kuanza kufanya uzalishaji kwa misingi ya kilimo hai hasa pale nilipogundua madhara yatokanayo na kemikali za viwandani hivyo nikaanza moja kwa moja kulima mbogamboga na viazi vikuu’’alisema.

‘’Niligundua kuwa kilimo hai si tu kinasaidia kukwepa madhara yatokanayo na kemikali za viwandani lakini inasaidia katika utunzaji wa mazingira, utunzaji rahisi na salama wa mifugo, uzalishaji kwa gharama nafuu, pamoja na upatikanaji wa soko la kuaminika wa mazao wakati wote’’aliongeza.

Anazalisha mazao gani

Bw. Kastulia anasema kuwa anazalisha mazao mbalimbali kama vile mahindi, maharage, kitunguu, viazi mviringo, mbogamboga lakini zaidi anazalisha mbogamboga na viazi mviringo kwa wingi jambo analolifurahia kwani soko lipo na ana uhakika wa chakula salama kwa ajili ya familia yake mwaka mzima.

Anazalishaje kwa misingi ya kilimo hai

Bw. Kastuli anasema kuwa, kwa kiasi kikubwa anatumia mbegu za asili hasa za mahindi na maharage lakini pia kwa mazao kama vile viazi, mbogamboga ananunua katika maduka ya pembejeo za kilimo yaliyosaliwa na serikali kisha kuyazalisha kwa njia za kilimo hai.

Anasema kuwa, anatumia mbolea za asili hasa baiyoslari inayotokana na kinyesi cha mifugo baada ya kuchakatwa ili kupata moto lakini pia anatumia mboji.

Aidha, anatumia dawa za asili alizojifunza kupitia jarida la Mkulima Mbunifu kutibu magonjwa na wadudu waharibufu wa mazao.

Soko la mazao ya kilimo hai likoje

‘’Soko la mazao ninayoyazalisha kwa misingi ya kilimo hai linapatikana na mbaya Zaidi nashindwa kumudu wateja kwani huwa wengi kiasi kwamba nakosa cha kuwauzia’’.

‘’Wateja wakubwa ni wanakijiji ambao mara baada ya kuwaelezea kuhusu mazao yaliyozalishwa kwa misingi ya kilimo hai na baada yaw engine kuanza kutumia wamekuwa wakimiminika kila siku kwa ajili ya kununua hasa mbogamboga jambo linalopelekea kutokufikisha mazao sokoni mara kwa mara kwani huisha nyumbani’’.

Bw. Kastuli anaongeza kuwa hata akipandisha bei mara nyingi si rahisi kwa wateja kuulizia ni kwanini au kughahiri kununua jambo linalomtia hamasa ya kuzalisha kwa wingi.

Changamoto

Bw. Kastuli anasema kuwa changamoto kubwa anayoipata ni ukosefu wa mbegu za asili kwa mazao mengine pamoja na wadudu waharibifu wa mazao wa ardhini lakini anashukuru kuwa Mkulima Mbunifu imeweza kujitahidi kwa kiasi kikubwa kuelekeza namna ya kukabilia nao kwa njia rafiki.

Wito kwa Mkulima Mbunifu

‘’Nawaomba Mkulima Mbunifu kuendelea kusambaza majarida haya kwa wingi kwa wakulima wengine pamoja na kutoa elimu juu ya umuhimu wa majarida hayo’’.

Wito kwa wakulima

‘’Nashauri wakulima wajikite katika uzalishaji kwa njia ya kilimo hai kwani kina faida hasa katika kulinda afya ya mlaji, wanyama, mimea na kudumisha rutuba ya udongo huku ukizalisha kwa gharama nafuu na kupata pato kubwa’’.

 

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *