- Binadamu, Mimea, Usindikaji

Sindika togwa kwa matumizi ya muda mrefu

Sambaza chapisho hili

Togwa ni kinywaji cha asili kinachonyweka kwenye maeneo mengi Tanzania pamoja na nchi zingine lakini ikitumika zaidi katika maeneo ya wakulima.

Kinywaji hiki chenye asili ya ubaridi kinatengenezwa kwa kutumia nafaka kama vile mahindi, ulezi, mtama (isipokuwa ngano) japo inasadikika pia kuwa kuna maeneo mengine wanatengeneza kwa kutumia matunda.

Asili ya togwa hapa nchini inasadikika kuwa imetokana na wanajamii wa kibantu ambao kwa miaka ya nyuma walikuwa wakijishughulisha na kilimo.

Togwa hutumika wapi

Kinywaji hiki cha baridi ambacho hunywewa na wa watu wa rika zote hutumika kama kiburudisho wakati wa kulima/kuvuna, kwenye sherehe za kijamii/kiasili/kikabila na hata wakati wa kazi zingine mbalimbali za kijamii.

Usindikaji wa togwa

Togwa inayotokana na ulezi pamoja na mtama, inaweza kusindikwa na kuhifadhiwa kwenye vyombo au chupa maalumu kisha kuuzwa kama bidhaa zingine sokoni.

 

Malighafi

Katika usindikaji huu, malighafi inayohitajika ni ulezi, mtama, maji, kimea pamoja na kilinda chakula (preservatives).

Vifaa

Hivi ni pamoja na sufuria, jiko, majaba, chupa maalumu za kuhifadhia, pamoja na karatasi/nailoni maalumu ya kufungashia chupa kwa ajili ya kupelekea sokoni.

Hatua za usindikaji

Kabla ya kuanza usindikaji wa togwa, ni muhimu sana kwa msindikaji kuhakikisha kwanza kuwa anafikiria kuhusu soko na mara nyingi soko linaanzia nyumbani kwa watu waliokuzunguka.

Usindikaji unafanyika kama ifuatavyo;

  • Hakikisha unakuwa na mtama na ulezi uliokauka vizuri (ulezi ni kwa ajili ya kutengeneza kimea).
  • Chambua mtama na ulezi vizuri kwa kutoa uchafu ama taka.
  • Baada ya kuchambua, safisha kwa kutumia maji safi salama ili kuondoa udongo na vumbi.
  • Anika juani sehemu safi na salama ili ukauke tena.
  • Saga mtama ili kupata unga.
  • Bandika sufuria jikoni kisha weka maji na ongeza unga tayari kwa kupika uji.
  • Chemsha mpaka uji uive vizuri (uji usiwe mzito wala mwepesi).
  • Epua na acha pembeni upoe kisha ongeza kimea (kinachotokana na ulezi).
  • Baada ya saa saba iko tayari kutumika kwa kunywa.
  • Ili kuhifadhi kwa ajili ya kupeleka sokoni na matumizi ya muda mrefu mara baada ya kuepua acha kwa siku tatu.
  • Rudisha tena jikoni na pasha ili kupata moto kidogo kisha ongeza kilinda chakula (preservative).
  • Paki ikiwa bado ya moto kwenye chupa maalumu kulingana na ujazo unaopendelewa sokoni.
  • Panga chupa kwenye karatasi maalumu ya kufungashia kisha bana karatasi kwa kuchoma kwa kifaa maalumu ya kuchomea kisha peleka sokoni.

Namna ya kutengeneza kimea

Chukua ulezi mkavu, uoshe na uweke kwenye chombo kikavu alafu ufunike kwa muda wa siku 2.

Ukifunua utakuta umeanza kuota (kimea). Chukua ulezi huu kisha saga kidogo ili kubakia na chenga chenga.

Mimina zile chenga chenga za kimea kwenye ule uji na ongeza sukari kidogo.

Faida za kunywa togwa

Kinywaji cha togwa kinasadikika kuongeza nguvu, ina madini ya kalsiamu, ina bakteria wazuri wanaohitajika katika mmeng’enyo wa chakula mwilini na kinywaji hiki pia kinaongeza protini mwilini.

Kuhusu usindikaji wa togwa tafadhali wasiliana na Charles Shauri wa GoMillet kwa simu namba 0767 691071

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *