Mara nyingi nimesikia na kuona MkM Mkisisitiza wakulima na wafugaji kujiunga kwenye vikundi, je kuna umuhimu gani, na ni hatua zipi za kisheria tunazopaswa kufuata ili vikundi vyetu vitambuliwe na kuwa rasmi?-Bakari Buhari, Msomaji MkM Handeni.
Kikundi ni muunganiko wa watu wenye nia/lengo moja katika kutekeleza jambo fulani walilolikusudia kwa faida ya hao walioamua kuwa pamoja. Lengo kuu la kuwa na kikundi ni kutaka kufanya au kutatua tatizo kwa pamoja.
Maamuzi ya kikundi kiwenje ikiwa na maana ya ni kikundi cha aina gani na wahusika watakua wangapi hutegemea na lengo kuu la kuunda umoja huo.
Kikundi kinaweza kuundwa na watu ambao wanafanya shughuli moja mfano kikundi cha wafuga nyuki, wakulima wa kahawa, wafugaji wa kuku n.k.
Pia kikundi kinaweza kuudwa na watu wanao fanya shughuli zisizofanana lakini wakatambulika kwa jina moja. Hivyo ni lengo kuu ambalo litawaunganisha hawa mfano wanataka kufahamika, kupata soko, elimu, kufikiwa kirahisi na wadau n.k.
Wazo la kuunda kikundi hutokana na mchakato wa mawazo ya wahusika wenyewe ili kuunda kikundi imara. Ili kuwa kikundi thabiti inabidi mambo yafuatayo yazingatiwe:
- Watu wa eneo moja.
- Mnafahamiana vyema.
- Muwe na nia ya dhati kuleta mabadiliko.
MUHIMU: Inashauriwa angalau kikundi kianzie na watu watano na kiwe na idadi ya wajumbe ambao haigawiki kwa mbili (namba tasa) hii itasaidia kipindi cha kuchagua viongozi na pia katika kupitisha ajenda za kikundi.
Aina za vikundi
Kuna makundi mawili ya vikundi ambayo hutofautiana kulingana na lengo kuu ambayo ni:
Kikundi cha shughuli za kijasiliamali
Hivi ni vikundi ambavyo lengo lake kuu ni kuzalisha kwa ajili ya biashara ama kupata faida.
Kikundi cha shughuli za kijamii
Hivi ni vikundi ambavyo vimeanzishwa kwa lengo la kusaidiana katika kipindi cha matatizo mfano, misiba, kuuguza /kuumwa. Kipindi cha furaha mfano sherehe na pia vikundi vya ulinzi. Ijapokua katika aina hii wanakikundi hunufaika kwa kukopeshana fedha ambalo huwa lengo dogo.
Makundi haya yote mawili huwa yakifanana japo hutofautiana katika lengo kuu.
Usajili wa kikundi
Ili kikundi kifanye mambo yake kwa uhuru na kwa upana zaidi ni vema kikapata usajiri. Usajiri upo katika hatua mbili za msingi ambazo ni
- Usajili katika serikali ya sehemu kilipo
Huu ni utambulisho wa kikundi katika serikali ya sehemu husika mfano kwa afisa mtendaji kwa kueleza ni nini mnafanya, kwa nini, viongozi wenu ni akina nani na mnafanyia sehemu gani.
Hii ni hatua ya awali ambayo huweza kufanyika kipindi cha awali ambapo kikundi kinaanzishwa au kama kikundi bado hakijakamilika.
- Kupitia kwa msajili wa vikundi na ushirika
Hii ni ngazi nyingine ya usajili ambayo ni kubwa ambayo hufanyika wilayani. Katika usajili huu kikundi chaweza kuwa kinaanza au kilikwisha anza. Hivyo unapokwenda kuomba usajili huu kuna vitu vya msingi ambavyo ni lazima uwe navyo ambavyo ni
- Katiba
- Barua ya maombi kutoka ofisi ya kata unayotoka au kwa afisa maendeleo
- Mukhutasari ambao unaonesha ni lini kikundi kilikaa na kupitisha azimio la makubaliano ya kufanya usajiri
- Huwa kuna gharama mfano gharama ya fomu ya maombi, ada na gharama ya usajili. Gharama hizi hutofautiana kutoka wilaya moja hadi nyingine.
Mfumo huu wa kuungana umeweza kuwa na mchango mkubwa kwa mashirika binafsi na serikali katika kuwasaidia wakulima kwa
- Kutoa elimu na vitendea kazi, serikali na mashirika binafsi wameweza kuwafikia watu wengi kwa njia hii kwa mfano uanzishwaji wa mashamba darasa
- Kuwadhamini
- Kuwatafutia masoko ya bidhaa mnazozalisha
- Kuwatambua, hii huwasaidia kujua ni nini na akinanani wanafanya kitu gani.