- Binadamu, Mazingira

Madhara ya kiafya kutokana na viuatilifu

Sambaza chapisho hili

Wakulima wengi wamejisababishia madhara ya kiafya kutokana na matumizi ya viuatilifu. Hii ni kutokana na kutokua na maarifa sahihi na kutokutumia hatua zinazostahili za kinga au kutekeleza mbinu sahihi za udhibiti.

Viuatilifu vya kiwandani na zana zake kwa kawaida huhifadhiwa majumbani ambako kuna hatari ya kugusana na chakula na watoto. Pia mazao yaliyopuliziwa dawa wakati mwingine huvunwa bila ya kuzingatia muda maalumu unaotakiwa upite kabla ya kuvuna, hivyo kuhatarisha afya za walaji.

Ni muhimu kwa mkulima kutambua madhara ya viuatilifu kiafya

Viuatilifu ni nini

Viuatilifu ni wingi wa Kiuatilifu. Kiuatilifu ni sumu ambayo hutumika kuua, kuangamiza, kufukuza, au kuzuia visumbufu katika mimea. Visumbufu vya mimea vinaweza kuwa wadudu, kuvu (fungus), magugu pamoja na baadhi ya wanyama na ndege.

Kilimo ndio zao kuu la biashara, nchini Tanzania asilimia kubwa ya mazao ya chakula, hufanywa na wakulima wadogo ambao kipato chao ni kidogo. Ili mkulima huyu aweze kuongeza kipato kwa haraka, anajikuta akitafuta njia mbadala ya kupambana na changamoto za uzalishaji wa mazao.

Imekua ni imani kwa wakulima wengi ya kwamba viuatilifu vinasaidia katika kutatua matatizo ya visumbufu vya mimea. Wakulima wengi wametumia kama njia mbadala kuondoa visumbufu hivyo, ili waweze kukuza mazao yao kwa haraka na kupata kipato.

Hata hivyo viuatilifu hivi vimegundulika kuwa na madhara kwa mimea, wanadamu, wanyama na mazingira pia. Tafiti nyingi za wataaluma zimeonyesha kuna madhara  kwa kutumia viuatilifu katika mazao ya chakula.

Madhara ya viuatilifu kwa binadamu

Mhadhiri Mshauri wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS), anasema viuatilifu vinaweza kuwa na madhara kwa binadamu na mazingira kwa kiwango tofauti na wakati mwingine vinaweza kusababisha vifo kwa binadamu na viumbe kila mwaka. Kuna mifumo mingi ya kikemikali inayoendelea ndani ya miili yetu.

Mimea ina uwezo wa kubadili kemikali kama hewa ukaa (kabonidioksaidi), maji na madini kutoka kwenye udongo kujenga nyingine za hali ya juu zaidi, kama vile sukari, protini na mafuta.

Mimea na wanyama hutengeneza kuvunja kemikali mfululizo ambapo hutumia kemikali kutuma ujumbe kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Viuatilifu vinaingiaje mwilini? (kinywa, ngozi, pumzi)
Inaelezwa kuwa unaweza kula kwa bahati mbaya au kwa makusudi, vyakula vyenye chembechembe za viuatilifu, kuvuta hewa yenye viuatilifu, kupitia kwenye ngozi  na macho iwapo utashindwa kutumia vifaa vya kujikinga wakati wa kuchanganya na kunyunyizia katika kilimo au hata kupitia mfuko wa uzazi wa mama mjamzito kwenda kwa mtoto aliye tumboni. Uvaaji wa vifaa vya kinga visivyokidhi mahitaji au uvaaji usio sahihi unaweza pia kusababisha viuatilifu kuingia mwilini. Uhifadhi wa viuatilifu ndani ya nyumba watu au wanyama wanamoishi unaweza kusababisha kuvuta hewa nyenye viuatilifu hata kama harufu haisikiki.

Pia viuatilifu vinaweza kuingia mwilini kupitia maji yaliyochafuliwa na kiuatilifu ambapo si lazima rangi na ladha ya maji viwe vimebadilika. Vile vile, matumizi ya viwekeo vitupu vya viuatilifu kwa kuhifadhia maji, maziwa, nafaka na vyakula vingine inaweza kikasababisha viuatilifu hivyo kuingia mwilini.

Sumu ya viuatilifu inayoingia mwilini mwa binadamu inaweza kuwa na athari za papo kwa hapo au athari za muda mrefu. Inaweza pia kuleta mlundikano wa kemikali ndani ya mwili.

Dalili za madhara ya viuatilifu

Katika mwili wa mwanadamu na mtu aliyedhurika na viuatilifu huwa na dalili zifuatazo;

  • Maumivu ya tumbo,
  • Kizunguzungu,
  • Maumivu ya kichwa,
  • Kutapika,
  • kukosa hewa,
  • kukohoa,
  • Kuwapo kwa matatizo ya ngozi na macho.

Madhara ya muda mrefu

Madhara ya muda mrefu ni kama vile;

  • Kupata saratani,
  • madhara ya kinga ya mwili,
  • Kupata msongo wa mawazo,
  • Kupata matatizo ya mfumo wa neva,
  • kusitisha mfumo wa tezi ndani au homoni unaoweza kusababisha upungufu wa nguvu za kike na kiume, watoto wa kiume kuota matiti, wanawake kuwa na shida wakati wa hedhi au kutokupata ujauzito
  • Mimba kutoka na hata kuwepo kwa upungufu wa viungo vya watoto
  • Kuzaa watoto walemavu au wenye mtindio wa ubongo

Madhara yanayotokea baada ya muda mrefu kama kuwa msahaulifu au kupoteza kumbukumbu, kutetemeka mikono, kushindwa kuzingatia jambo, kuonekana mzee kuliko umri halisi, kupooza na kukosa fahamu.

Viuatilifu vinaingiaje katika mazingira?

  • Inakadiriwa asilimia 10 hufikia sehemu iliyolengwa huku asilimia 90 ya kemikali hizo zinaishia kwenye mazingira.
  • Viuatilifu vinapoharibiwa kwa njia zisizo sahihi baada ya kwisha muda wake vinaweza kuchangia kuharibu mazingira.
  • Vifungashio vilivyokwishatumika vikitupwa ovyo husababisha uchafuzi wa mazingira kwani havikosi masalia ya viuatilifu

Athari zilizowahi kutokea kutokana na kemikali hizo kuingia katika mazingira ni pamoja na baadhi ya mayai ya kuku wa kienyeji katika eneo mojawapo lililokuwa na viuatilifu chakavu kukutwa na masalia ya viuatilifu ndani yake.

Nyuki wanaohitajika kuchavua mimea kama vile mahindi ili mazao yawe mengi wanaathirika na viuatilifu katika mazingira hivyo kupunguza uzalishaji. Vile vile, asali izalishwayo na nyuki walio kwenye maeneo yaliyochafuliwa na viuatilifu hukosa soko la nje kwani hukutwa na masalia ya viuatilifu.

Pia baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa viuatilifu chakavu hadi sasa mimea haiwezi kuota tena kutokana na kiwango cha viuatilifu kuwapo katika mazingira.

Hata hivyo viuatilifu vikitumika kwa wingi mno huathiri uwezo wa udongo kushika maji na virutubisho, hudhuru hata wanyama waishio ardhini na ndani ya maji. Minyoo ardhini iliyokuwa inasaidia kutengeneza rutuba ardhini wamepotea kwa sababu ya viuatilifu kuchafua mazingira.

Ushauri

Inashauriwa kuepuka matumizi ya kemikali kwa wakulima na kutumia mbinu mbadala ili kupunguza matumizi ya viuatilifu. Ikibidi kutumia viuatilifu vitumike vile vyenye usumu usio mkali na visivyolundikana katika mazingira.

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *