Katika toleo lililopita la juni tulianza kuangazia madhara yasababishwayo na viatilifu na katika toleo hili tumalizia mada hii kwa kuangalia njia ambazo sumu huingia mwilini. Mara nyingi wakulima hutumia kemikali kwa matumizi tofaut, bila kufahamu kuwa wao pia wanaathiriwa na madawa hayo. Dawa hizo huingia mwilini kwa njia mbalimbali.
Kwa sababu kuna aina nyingi za dawa, sumu inaweza kutofautiana sana. Uwezekano wa kuwa mgonjwa kutokana na kuathiriwa na viuatilifu hutegemea mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na:
- Aina ya dawa (baadhi ya dawa ni hatari zaidi kuliko zingine);
- Kiasi cha dawa uliyogusana nayo au uliyovuta (kiasi gani),
- Kiwango cha dawa katika mchanganyiko (kiasi kikubwa/kipimo),
- Muda dawa ilivyogusana/kuvutwa (muda/muda gani),
- Njia ya kuingia ndani ya mwili (ngozi, kumeza, au kuvuta pumzi), na
- Kemikali nyingine katika bidhaa ya dawa.
Kwa ujumla, hatari kwa mtumiaji huongezeka kutegemeana na kiwango na nguvu ya dawa inayotumika na muda (urefu) wa mgusano na dawa unavyoongezeka.
Je, watu wanaweza kuwa na mzio wa viuatilifu?
Baadhi ya viatilifu husababisha mzio (allergy) kwa watumiaji. Dalili za mzio hasa katika ngozi hujumuisha uvimbe, ngozi kuvia, kuwasha, maumivu, na malengelenge. Dalili za mzio katika kupumua zinaweza kujumuisha ugumu wa kupumua, kubana kwa kifua, kukohoa n.k. Katika baadhi ya matukio ya mzio katika kupumua huweza kusababisha shambulio kali la pumu.
Madawa yenye nguvu ni hatari zaidi
Unapaswa kuchukua tahadhari kubwa ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi ya madawa yenye nguvu. Ni muhimu sana kukinga mwili
mzima (hasa mikono na uso) yasigusane kabisa na mwili wako. Ni rahisi sana kupata madhara yanayotokana na madawa ya kemikali wakati wa;
• Kufungua chupa au pakiti zenye madawa ya kuangamiza wadudu, Kumimina, Kupima, Kukoroga
• Kutumia madawa ambayo yanapendekezwa kwa kiwango kidogo
• Kusafisha dawa iliyomwagika chini
• Kutupa ovyo pakiti ambazo zilikuwa na dawa za kuwaangamiza wadudu
Ni muhimu kujiepusha na matumizi ya dawa hizo au kuhakikisha unavaa vifaa vya kujikinga hasa mikono na miguu ili kupunguza hatari ya kumwagikiwa na dawa. Inapotokea kuwa katika mazingira inazotumika dawa hizo ni muhimu kufunika kichwa, uso na mabega.
Ni muhimu kuzingatia kanuni za usafi
Katika mazingira yanapotumika madawa ya kuangamiza wadudu, ni muhimu sana kuzingatia kanuni za usafi kwa umakini hasa kwenye sehemu za mwili zinazoachwa wazi kazi zinapomalizika na kabla ya kula chochote.
Kama ilivyo desturi hakikisha kuwa mavazi na vifaa vyote vilivyotumika au kuwa katika mazingira zilipotumika dawa, vinasafishwa au kuhifadhiwa katika sehemu ambayo haviwezi kusababisha madhara kwa afya ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira.