Ndugu msomaji wa jarida la Mkulima Mbunifu, ni furaha yetu kuwa umeendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali zinazochapishwa kwenye jarida hili. Pia tunashukuru wewe uliefatilia na kutaka kufahamu kwa undani kwa kuuliza maswali pale ambapo hujaelewa ama umekwama. Pia tunashukuru kwa mchango wako katika kutekeleza kilimo hai.
Katika makala hii ni baadhi tu ya maswali yaliyoulizwa na wakulima wasomaji wa jarida hili kwa njia ya simu. Mkulima Mbunifu inatoa majibu kupitia ukurasa huu kwani inawezekana pia ulikua na swali kama hilo.
Swali toka 0755 056611: Samahani naomba kujua dawa ya kutibu ugonjwa wa kunyauka bamia ikiwa bado ni miche.
Jibu toka MkM; Habari, Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za jarida hili. Asante pia kwa swali lako. Kuhusu ugonjwa wa mnyauko kwenye bamia, unaweza kutumia unga wa mlonge uliochanganywa na mkojo wa mifugo.
Chukua majani ya mlonge kisha anika juani mpaka yakauke na mara baada ya kukauka, twanga ili kupata unga unga. Pima unga wa mlonge kiasi cha lita 20, changanya na majivu kiasi cha sado moja yaani kilo 4 kisha weka mkojo wa mifugo mfano ngombe kiasi cha lita 5.
Changanya vizuri kuhakikisha malighafi zote zimechanganyika kisha peleka moja kwa moja shambani na weka katika kila mmea kwa kuuzungushia kidogo kidogo.
Swali toka 0655 547787; Mimi ni mfugaji wa kuku wa asili, kuku wangu wana shida ya kutaga. Ninawafuga kwa mfumo wa nusu huria, nimejaribu watibu minyoo na magonjwa mengine lakini bado.
Jibu toka Mkulima Mbunifu; Habari, Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za jarida hili. Kuku kutokutaga husababishwa na kutokupata chakula chenye madini sahihi yatakayomwezesha kuweza kutengeneza na kutaga mayai.
Kuku wa asili au wa kienyeji ili aweze kutaga mayai wakati wote, hakikisha unawapa chakula chenye mjumuisho kama ufuatao; mahindi, pumba za mahindi, soya, mashudu ya alizeti/mashudu ya pamba, dagaa iliyokaushwa, damu, mifupa iliyosagwa, chokaa, chumvi na vitamini.
Mchanganyiko huu ni, mahindi kilogramu 40, pumba ya mahindi kilogramu 25, mtama kilogramu 5, mashudu ya alizeti kilogramu 10, dagaa kilogramu 4, damu kilogramu 5, mifupa iliyosagwa kilogramu 4.50, chokaa kilogramu 4, vitamini kilogramu 2, na chumvi kilogramu 0.50. auDagaa kilogramu 4.5, soya kilogramu 18, mahindi kilogramu 50, pumba ya mahindi kilogramu 15, mashudu ya pamba kilogramu 5, mifupa iliyosagwa kilogramu 3, vitamini kilogramu 2, chumvi nusu kilogramu (0.5) na chokaa kilogramu 2. Yote jumla kilogramu 100.
Changanya vizuri na wapatie kuku kila siku. Angalia pia unaweza kukuta kuku wanataga nje hivyo si rahisi kuona kama wametaga.
Swali toka 0626 685754; Naomba kuelimishwa jinsi ya kuandaa almond ili nizitumie kama karanga.
Jibu toka Mkulima Mbunifu; Habari, Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za jarida hili. Kuhusu mbegu za almond kama karanga, unaweza ukatafuna hivyo hivyo zilivyo mara baada ya kubanguliwa.
Lakini pia kama hutaki kutumia na maganda yake, unaweza kuchemsha kwa dakika 5 kisha weka kwenye maji baridi na acha kwa dakika chache kisha anza kutoa maganda na utabakiwa na karanga nyeupe. Waweza kula hivyo ilivyo ama kupasha kidogo kwenye moto.
Swali toka 0762 256368; Matunda (makarakara) yangu yananyauka na kudondoka nifanye nini? Nguruwe anachukua mda gani kuzaa?
Jibu toka Mkulima Mbunifu; Habari, Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za jarida hili. Kuhusu karakara kudondosha maua huweza kusababishwa na mabadiliko ya hali joto kuwa juu sana au chini zaidi, uchavushaji duni, mvua nyingi, au kuwepo kwa hali ya hewa yenye ukungu kwa muda mrefu pamoja na kuweka mbolea nyingi ya naitrojeni hivyo angalia kwanza kujua chanzo ni nini ili uweze kujua njia ya kutatua.
Kuhusu nguruwe kuzaa, mara nyingi anaweza kuanza kuzaa mara afikapo miezi mitano au sita.