Ni jambo jema kufahamu kama mayai yanayoatamiwa na kuku yataanguliwa yote au mangapi hayataanguliwa. Na kwa wanaototolesha vifaranga ni muhimu zaidi kwao kujua hali ya mayai inavyoendelea ndani ya kiangulio na kufahamu kama kuna tatizo linaweza kusababisha kifaranga ndani ya yai kufa.
Pia kujua kama kuna mayai ambayo hayatapelekea kutotoa kifaranga na kuyaondoa. Hii yote hufanyika kwa kuyachunguza mayai yanayototolewa kila siku.
Makala hii inalenga kukujuza namna ya kuchunguza mayai na kujua kama (a) yana kifaranga hai (b) kifaranga kimekufa (yai viza) na (c) kama yai halina kifaranga. Kuku anaweza kutaga mayai kukiwepo na jogoo au bila hata kuwepo na jogoo.
Kazi ya jogoo ni kurutubisha mayai ili yaweza kuwa na kifaranga ndani. Hivyo yale yatakayorutubishwa na jogoo yatakuwa na kifaranga ndani wakati yale ambayo hayajarutubishwa na jogoo hayatakuwa na kifaranga.
Kutotolesha mayai kwa njia ya asili (kuku)
Mayai yanayototolewa na kuku hayana vitu vingi vya kuzingatia maana ni kuku mwenyewe anayeyapatia joto mayai ili yaweze kuangua vifaranga. Unaweza kuchagua kuku mwenye uwezo mzuri wa kutamia na kukupatia vifaranga na akaatamia mayai ya wale kuku wasio na uwezo wa kuatamia.
Lakini kuku huyu pia awe na sifa nyingine ya kulea vifaranga mara baada ya kuangua. Kuku wa aina hii watakuwa kama mashine ya kuangua vifaranga ndani ya shamba lako. Hivyo watahitaji matunzo ikiwa ni pamoja na viota vizuri vya kuangulia, yaani sehemu salama kwa kuku kuatamia mayai kwa siku 21.
Kuku anayeatamia vizuri atakaa kwenye mayai usiku na mchana, akitoka nje mara moja kula au kutafuta chakula, kunywa maji na kunya kinyesi. Ukitaka kumtoa kwenye mayai bila ridhaa yake huwa mkali na anaweza kukufukuza kwa hasira.
Kiota chake kikiwekwa mahali tulivu, kuku huyu atageuza mayai mara 12 hadi 14 kutoka upande yalipolalia kwenye kiota. Mara kadha atakuwa akiyatawanya manyoya yake ya kifua ili joto lake la mwili liyafikie mayai na kuyafanya yabaki kuwa ya joto lile linalohitajika (nyuzi joto 37 za sentigredi). Lakini pia manyoya ya kuku hukifanya kiota chote kiendelee kuwa na joto.
Kutotolesha mayai kwa njia ya mashine (Incubator)
Utotoleshaji wa mayai kwa njia ya mashine unafuata kanuni zinazotumiwa na njia ya asili (kuku). Mashine imetengenezwa kufuata mahitaji yanayotolewa na kuku anayeatamia. Kuku ataatamia mayai kwa siku 21, atageuza mayai mara kwa mara, atayapa mayai joto (nyuzi joto 37 digirii za sentigredi) na unyevu nyevu. Hivyo hivi vyote lazima mashine itemize yaani igeuze mayai, joto stahiki liwepo, unyevunyevu, na mayai yakae kwa siku 21.
Mayai yanayowekwa kwenye mashine ya kutotolesha lazima yawe masafi na ambayo hayajapasuka.
Hivyo kama kuna mayai machafu, yamechafuliwa na kinyesi cha kuku yasafishwe vizuri kwa kitambaa/spongi safi. Kuepuka mayai kuchafuliwa na kinyesi ni bora ukusanye mayai mapema. Unaweza kukusanya mayai mara mbili kwa siku.
Uchunguzaji wa mayai yanayoatamiwa au yaliyopo kwenye mashine ya kuangulia vifaranga
Kuchunguza maendeleo ya mayai yanayoatamiwa au yaliyopo kwenye mashine ni muhimu sana. Hii itakusaidia kubaini kama mayai yako yana vifaranga, hayana vifaranga au vifaranga vimekufa. Hivyo utaondoa mayai yale ambayo hayataanguliwa.
Njia inayotumika inajulikana kama candling (yaani kuchunguza mayai kwa kutumia mwanga wa mshumaa). Wagunduzi wa mwanzo walitumia mshumaa lakini sasa vipo vifaa vingi kuanzia vile vya kisasa hadi vile vya kawaida ambavyo vinapatikana mazingira yetu kirahisi mfano tochi.
Utofauti uliopo ni kuwa vile vya kisasa mionzi yake inakusanywa pamoja kumulika eneo moja inayopenya kirahisi kuona ndani ya yai wakati mwanga kama wa tochi unatawanyika.
Kwa nini ufanye candling ya mayai?
Candling ni sehemu muhimu sana katika ufugaji wa kuku hasa unapofanya uchunguzi wa ukuaji wa kifaranga ndani ya yai. Hivyo candling inakusaidia kuona nini kinaendelea ndani ya yai katika kila hatua ya ukuaji wa kifaranga. Mwanga unaotumika kumulika yai kwenye eneo lenye giza unakusaidia kuona baadhi ya vitu ndani ya yai.
Nini utaona wakati wa kumulika mayai (candling)
Kwa yai hai lililorutubishwa utaona mishipa ya damu, kifaranga kikichezacheza na uwazi upande ule mkubwa.
Kwa yai ambalo kifaranga kimekufa (yai viza) huwezi kuona mishipa ya damu, utaona kifaranga ila hakichezichezi na huwezi kuona uwazi wa hewa upande mkubwa wa yai.
Kwa yai ambalo halikurutubishwa huwezi kuona chochote (mishipa ya damu, kifaranga).
Candling inatakiwa ifanyike kila siku hasa kwa wanaotumia mashine ili kubaini kama kuna tatizo lolote linalotokana na mashine na kulirekebisha. Chunguza yai moja baada ya jingine na hakikisha yai halikai nje ya incubeta zaidi ya nusu saa.