- Kilimo

Unaweza kuuwa wdudu waharibifu kwa kutumia muarobaini

Sambaza chapisho hili

Muarobaini ni moja kati ya miti ya asili, ambayo kwa karne nyingi umekuwa ukitumika kama dawa kwa binadamu, wanyama na mimea.

Tunapozungumzia mwarobaini katika kuua wadudu kwenye mazao, tunazungumzia mafuta yaliyomo katika mmea huu. Hii ni dawa ambayo ina uwezo wa kuua wadudu wa aina mbalimbali. Mafuta ya mwarobaini yana dawa inayojulikana kitaalamu kama “AZADIRACHTIN”. Hii ni kemikali isiyo ya kawaida kwani ina homoni zinazopatikana kwa wadudu, hivyo huwachanganya wadudu na kuwafanya waone kama ni homoni zao.

Wadudu wanapokula homoni hizo zilizopo kwenye muarobaini, zinazuia homoni zao kufanya kazi, hata wanapotaga mayai hayaanguliwi kwani yanakuwa hayana uhai.

Muarobaini unaweza kutumika kutibu udongo, kwani udongo uliowekwa muarobaini, hauruhusu wadudu kuzaliana. Muarobaini pia hutumika kama kifukuza wadudu (repellant) na huweza kuwafanya wadudu wenye miili laini kukosa hewa, hivyo kufa kwa haraka.

Inashauriwa kutumia muarobaini nyakati za jioni maana wadudu wenye faida hufanya kazi mchana , hivyo ukitumia muarobaini muda wa mchana utaua hata wadudu rafiki.

Pamoja na hayo, wadudu rafiki huwa hawali majani, na muarobaini humdhuru mdudu anaekula majani, hii ina maana kuwa muarobaini hautamdhuru mdudu rafiki.

Kwa kuwa muarobaini ni kiuatilifu hai, tunapotumia tunapunguza wadudu, kuhifadhi mazingira, na pia kupunguza hatari ya wadudu kuwa sugu kutokana na matumizi ya muda mrefu ya madawa.

Hawa ni baadhi ya wadudu wanaodhibitiwa kwa kutumia muarobaini: Minyoo fundo, panzi, kimamba, inzi weupe (wakubwa), utitiri, chawa, thiripi, dumuzi, viwavi na wengineo.

Namna ya kutengeneza mchanganyiko

Unaweza kutengeneza mchanganyiko wa mwarobaini kulingana na mahitaji yako, na ukubwa wa shamba pia. Hapa tuchukulie mfano wa utengenezaji wa mchanganyiko wa lita ishirini (20):

Mahitaji

  • Gramu 700 za mbegu ya muarobaini (Unatupatia wastani wa mililita 200 za mafuta ya muarobaini)
  • Mililita 20 za sabuni ya maji
  • Lita 20 za maji ya uvuguvugu

Kwa mahitaji zaidi zidisha kiasi hiki kulingana na mahitaji yako. Endapo unapata tabu kuyeyusha, ongeza sabuni ya maji.

Maandalizi

  • Twanga mbegu za muarobaini na kupata mafuta
  • Chuja mafuta kwa kutumia kipande cha blanketi
  • Tumia maji ya uvuguvugu, changanya na sabuni, kisha ongeza mafuta huku ukikoroga kwa nguvu.

Mchanganyiko huo unaweza kuhifadhiwa kwenye chombo cha plastiki kilichofungwa vizuri.

Ni vyema kuandaa mchanganyiko utakaotumika wiki moja ili kuzuia kupoteza uwezo wake. Mashudu yaliyobaki yanaweza kuweka shambani ili kusaidia kudhibiti wadudu kwenye udongo.

Matumizi

Tumia mililita 10 za mafuta ya muarobaini kwa lita moja ya maji. Nyunyiza kila baada ya siku 4-7 kulingana na kiwango cha wadudu shambani. Kwa kunyunyiza kwenye udongo,  tumia kiwango mara nne ya kiwango cha kawaida, kwa kuchanganya kwenye maji ya umwagiliaji tumia lita 8-10 kwa hekta.

Mazao

Muarobaini unaweza kutumika kwenye mazao yote, lakini inashauriwa  kujaribu kwenye eneo dogo kuona kama kuna athari kwenye mimea. Kunyunyizia shamba lote kwa mara moja, kunaweza kuathiri mazao yako.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *