- Kilimo

Canavalia hurutubisha udongo kwa kiwango kikubwa

Sambaza chapisho hili

Katika toleo lililopita tuliona ni kwa namna gani mkulima Bi. Edvesta Yambazi alivyofanikiwa katika kulima canavalia. Katika toleo hili tutaangalia kwa undani zao la canavalia ni zao gani na linalimwaje.

Canavalia ni zao jamii ya mikunde ambayo hujulikana kwa majina mengine kama Jackbean au swordbean. Kitaalamu au kisayansi hujulikana kama Canavalia Ensiformis.

Zao la canavalia ni moja ya mazao funikizi na huwa katika mwonekano wa aina tofauti wakati unapoota.

Hii ni kwa sababu kuna zinazolalia ardhi na kuna zinazopanda kwenye miti au juu ya kingo za shamba.

Kazi ya canavalia ardhini

Mmea huu ni maarufu kwa ajili ya kurutubisha udongo, lakini watu wengine hulima kwa lengo la kuimarisha makingo na hata huoteshwa kama ua majumbani.

Utafiti uliofanywa na Roland Bunch na kuandika kwenye kitabu chake cha (Restoring the soil) umebaini kuwa mmea huu huongeza naitrojeni katika udongo kwa kiwango cha mpaka kilogramu 240 kwa ekari moja.

Tafiti katika maeneo mbalimbali zimeonesha kuwa urutubishaji huu katika udongo ni sawa na kuweka mbolea ya viwandani aina ya yurea mifuko 10.

Aidha, kiwango cha urutubishaji ambayo canavalia hutoa katika kurutubisha udongo ni mara sita ya urutubishaji unaofanywa na mimea mingine ya kurutubisha ardhi jamii ya mikunde.

 

Jinsi ya kulima canavalia

Zao hili hulimwa kama vile inavyolimwa mazao mengine aina ya mikunde.

Ni vyema kuotesha mwanzoni mwa msimu wa mvua ambapo ardhi ina unyevuunyevu wa kutosha na unaweza kuotesha sehemu yoyote kama porini au shambani, na unaweza kulima lenyewe au kuchanganya na mimea mingine.

Zao hili hupendelea zaidi sehemu yenye mwanga wa kutosha hivyo likioteshwa katika eneo wazi pia hufanya vizuri zaidi.

Utunzaji

Utunzaji wa canavalia ni rahisi sana. Hii ni kwa sababu yenyewe ikishaota haihitaji matunzo mengi zaidi ya kufanya palizi mara moja tu kwani yenyewe huzuia magugu yasiote.

Sifa za canavalia

  • Canavalia huota katika maeneo yenye ukame na hata katika tindiga.
  • Zao hili lina uwezo wa kukusanya na kuchukua naitrojeni kutoka hewani na kupeleka moja kwa moja kwenye udongo.
  • Haina gharama nyingi za uzalishaji wala utunzaji.
  • Huweza kuoteshwa kwa kuchanganya na mazao mengine ya chakula kama mahindi, kahawa au kuoteshwa peke yake shambani.
  • Hupendezesha nyumba pale linapolimwa au kuoteshwa kama maua.

Faida za canavalia

  • Huongeza naitrojeni katika udongo ndani ya mwaka mmoja katika eneo lililopoteza rutuba kwa kipindi kirefu.
  • Hufunika ardhi na kufanya udongo kuwa na unyevu au kutokukauka na kupoteza maji kwa wingi.
  • Husaidia katika kipindi cha kulima au kufanya maandalizi kwa ajili ya kilimo cha mazao mengine, udongo usiwe wazi sana na kupitisha jua ardhini.
  • Ni zao la kibiashara kwani hununuliwa na wakulima wengine kwa ajili ya kuotesha na kurutubisha ardhi yao lakini pia hulimwa wakati wowote.
  • Baadhi ya wakulima waliolima zao hili wamethibitisha kuwa hauliwi na wanyama pori au wa kufugwa hivyo ni faida kwa kuweka ulinzi shambani.
  • Wakulima wameshuhudia kuwa ni dawa kwa mtu aliyeng’atwa na nyoka. Maharagwe yake husagwa na kisha unga kuwekwa kwenye kidonda kwa ajili ya kutoa sumu ya nyoka.

Kuvuna

Canavalia huanza kuvunwa miezi sita hadi tisa. Zao hili huweza kuvunwa kwa kipindi kirefu sana na kwa vipindi tofauti endapo mkulima hataling’oa mapema shambani kwake.

Katika kilogramu 2 za canavalia unaweza kuvuna mpaka kilo 500 kutegemea na kipindi cha uvunaji.

Soko

Soko lipo na wakulima wengi wameanza kutafuta mbegu za canavalia lakini elimu zaidi bado inahitajika kwa wananchi ili kuweza kulipa kipaumbele zao hili kwa faida ya udongo na biashara.

Ushauri

Utakapolima au kuotesha canavalia, hakikisha mara baada ya mavuno unaling’oa na kupumzisha ardhi kisha kuotesha mazao mengine kama kawaida. Yaani ni vyema kufanya kilimo cha mzunguko.

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *