Tofauti na ilivyo kwa watu wazima, watoto wanahitaji kupata lishe bora kila siku ili kuweza kujenga miili yao, na kukua katika kiwango kinachotakiwa na hatimae kuwa watu wazima. Ni muhimu kufahamu lishe inayotakiwa kwa watoto.
Lishe bora ni nini?
Lishe bora ni mlo unaojumuisha uwiano unaotakiwa wa virutubisho vyote muhimu vinavyotakiwa kutoka katika makundi makubwa ya vyakula. Miili yetu huhitaji virutubisho muhimu ili kuendelea kuwa na afya na kujilinda na magonjwa. Kuna baadhi ya virutubisho vinaweza kutengenezwa mwilini, lakini vingine lazima vipatikane kutoka kwenye chakula.
Hatuwezi kuongelea lishe bora bila kuongelea mafungu sita muhimu ya vyakula nayo ni Wanga, mafuta, protini, madini, vitamin na maji.
Umuhimu wa lishe bora kwa afya ya mtoto
Lishe bora ni muhimu katika maendeleo ya afya ya kila mtoto. Misingi ya lishe bora kwa mtoto ni rahisi. Watoto wanahitaji chakula bora kutoka katika makundi makuu ya chakula, ikiwa ni pamoja na nafaka, mbogamboga, mahindi, maziwa na nyama.
Watoto pia wanahitaji aina tofauti za vyakula katika ngazi, na hatua tofauti za ukuaji. Jamii tofauti zinaweza kuwa na aina zinazotofautiana za vyakula na namna ya ulishaji.
Gharama za vyakula zinaweza kuwa kikwazo kwa baadhi ya familia. Aina ya tamaduni na mila zinaweza kulazimu familia kutumia aina ya fulani za vyakula, na pia baadhi ya watoto wana uzito unaotokana matumizi ya aina fulani za vyakula.
Unapaswa kufanya nini?
Ni muhimu kujifunza juu ya lishe ya watoto kulingana na makundi na umri ili kuweza kutambua iwapo mtoto anakula vizuri na kuweza kumsaidia kutokana na hali halisi ya wakati husika katika ukuwaji wake.
Taarifa za lishe kwa jamii husika hupatikana kupitia kwa waelimishaji wa afya walio katika eneo husika, maandiko au majarida ya afya na lishe, au mtandao. Ni muhimu kuwekea mkazo katika lishe ya familia.
Dini na tamaduni huwa na nafasi kubwa katika uchaguzi wa vyakula kwa Watoto. Kuwa na uelewa juu ya gharama za chakula, kwani familia haiwezi kuendelea kuwa na aina za vyakula wasivyoweza kugharamia.
Lishe bora kwa mtoto ni ipi?
Muhimu sana, mtoto anashauriwa kunyonya maziwa ya mama tu kwa muda wa miezi sita(6) tangu alipozaliwa.
Baada ya miezi 6 watoto wanahitaji aina nyingine ya vyakula pamoja na maziwa ya mama ili kuwafanya kuendelea kukua vyema. Aina mbali mbali za vyakula vitamsaidia mtoto wako katika njia mbali mbali. Wape watoto wako mchanganyiko wa vyakula hivi mbali mbali kila siku. Vyakula hivi vinaweza kupikwa kulingana na mahitaji.
MUHIMU: Zingatia usafi wakati wa uandaaji wa vyakula vya mtoto
Maharagwe, dengu, nyama, kuku, samaki, na kiiniyai husaidia kujenga mwili wa mtoto wako.
Wali, viazi, ugali, mahindi, mtama, na matoke humpa mtoto wako nguvu.
Matunda na mboga kama vile mboga za majani, karoti, malenge, machungwa, maembe, na mapapai, yatamkinga mtoto wako dhidi ya maradhi.
Jinsi ya kumlisha mtoto
Mtengee mtoto kijiko na kisahani cha kutumiwa na yeye tu. Mtayarishie uji ambao ni mzito kiasi cha kuweza kukaa kwenye kijiko. Kila mara, mlishe mtoto uji pamoja na vyakula vingine. Watoto ambao hawatakula vizuri wakati huu huenda wakawa na afya mbaya na wapungufu katika werevu maisha yao yote.
Mtoto wako anapoendelea kuwa mkubwa, endelea kuongeza kiasi cha chakula unachompatia.
Akiwa na umri wa miezi 6, anza kumpa mtoto wako aina nyingine ya vyakula pamoja na kumnyonyesha. Endelea kumnyonyesha hadi atakapotimu umri wa miaka miwil
Tabia ya ulaji wa watoto wanapokua
Kwa kawaida, watoto huangalia ni nini watu wazima wanakula, na mara zote hulinganisha kile wanachosema kwa kile wanachotenda.
Kuzisaidia jamii kuboresha uwezo wao wa chakula ni jambo muhimu na tunaweza kulifanya katika kusaidia familia kutoa lishe bora kwa watoto wao kila siku. Hii inaweza kuwa ni pamoja na:
- Kuboresha mgawanyiko wa chakula, hasa kwa familia zisizoweza kujinunulia vyakula vya gharama.
- Kuelimisha watu kuhusu umuhimu wa lishe bora.
- Kuwasaidia watu wa eneo husika kulima na kuzalisha aina tofauti za mazao ya chakula.
- Kufahamu ni njia gani nyingine zinaweza kutumika kujiandaa vizuri ili kuzisaidia jamii na familia kuwalisha watoto chakula bora kila siku.
- Ni rasilimali zipi nyingine zinazoweza kutumika au kushirikishwa ili kusaidia jamii kuboresha uwezo wao wa chakula.
- Kuhakikisha Watoto wanapata mahitaji ya msingi katika maisha ya kila siku.
Ni muhimu kila mwanajamii kuhakikisha kuwa anazingatia afya ya familia iko salama, na hasa kwa ukuaji bora wa watoto kwani afya bora ndiyo msingi wa kuwa na jamii bora.