- Mifugo

Unawezaje kutambua mnyama mwenye afya nzuri na mwenye matatizo ya kiafya?

Sambaza chapisho hili

Afya ya mifugo ni tatizo kubwa linalowakabili wafugaji walio wengi katika sehemu mbalimbali za nchi. Wapo wataalamu mbalimbali katika maeneo na mikoa yote ya nchi wanaotoa huduma ya mifugo lakini, bado kuna changamoto nyingi zinazowakumba wafugaji.

Katika sehemu ambazo mawasiliano ikijumuisha pia miundo mbinu kuwa duni, wafugaji wamekuwa wakipoteza mifugo hasa kutokana na sababu kuwa mara ugonjwa unapoikumba inakuwa si rahisi kufikiwa na mtaalamu kwa wakati hivyo kupeleka mifugo kufa.

Huduma za kisasa za kitabibu huenda pia kuonekana ni aghali katika maeneo machache hivyo wafugaji wengi kuonekana kutozitegemea kwa asilimia 100 na kuendelea kupoteza mifugo yao.

Mnyama mwenye matatizo ya kiafya

Mnyama mwenye shida ya kiafya hukosa hamu ya kula na kunywa maji, mwili kunyong’onyea na kuonekana mchovu na hutembea pole pole na kwa taabu na mara nyingi hujitenga na wenzake.

Pia, pua zake na midomo huonekana kukauka na kupunguka kwa kiwango cha uzalishaji kama vile maziwa. Kwa madume huzubaa na kuinamisha shingo chini na kukosa hamu ya kuwapanda majike wanaoingia kwenye joto.

Dume anayeumwa hunyong’onyea na kukosa uchangamfu

Mnyama mwenye afya nzuri

Mara nyingi mnyama mwenye afya nzuri huwa mchangamfu wakati wote, macho maang’avu huku mkia na masikio vikimsaidia kufukuza inzi na pia hula na kucheua, kunywa maji vizuri kila siku.

Mnyama huonyesha ushirikiano na kutembea pamoja kwenye kundi huku akitembea vizuri, anashtuka na kukimbia anaposhtuliwa na mnyama hatari anapomkaribia kamaa vile mbwa mwitu, fisi, chui, simba.

Mwili wa mnyama mweye afya nzuri una uwezo mkubwa wa kukibadili chakula anachokula kutoa mazao ya kutosha kama vile maziwa na anaonekana mwenye nguvu na kwa wale wanaoendelea kukua wanaongezeka uzito kwa muda mfupi.

Kwa mnyama anayekamuliwa mara kwa mara kupiga kelele za kumtafuta mtoto wake, kiwele huwa kimejaa maziwa, chuchu huwa wakati mwingine zimetanuka upande kwa ajili ya kujaa maziwa.

Aidha, ngozi ya mnyama husisimka mara kwa mara wadudu wapomtambaa, ngozi kuwa na ulaini unaotakiwa na manyoya hung’aa  na pua na midomo huwa na unyevu unyevu wakati wote.

Kwa madume, huwa wana hamu ya kuwapanda majike wanaoingia kwenye joto, miili yao hujengeka vizuri. Pumbu hujengeka na kukaa vizuri kwenye nafasi yake (yaani katikati ya miguu).

Kwa kawaida unapo mkaribia mnyama mweye afya njema na asiye na tatizo lolote la viungo endapo atakuwa amekaa chini ni lazima atanyanyuka na ikiwa amesimama ataanza kusogea sogea kuangalia unataka kufanya nini.

Mnyama mwenye afya nzuri kwa muonekano huwa mchangamfu
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *