Hupunguza uchafuzi wa mazingira
Kila siku watumiaji wa vyombo vya usafiri hubadilisha matairi. Mbali na kuwa matairi hutumika kutengeneza vitu kama viatu, mipini ya mapanga n.k, pia matairi yanaweza kutumiwa katika kilimo cha mbogamboga na matunda badala ya kuchoma matairi na kuzalisha kemikali zenye sumu kwa binadamu.

Ni rahisi kutumia
Ukilinganisha na kulima kwa kutengeneza matuta ya mbao au mawe, kutumia matairi hakuhitaji ujenzi wowote.Unachukua tairi, unaweka bustanini, unajaza udongo, kisha unapanda, basi!
Huleta joto na kukausha udongo kwa haraka
Kwa maeneo yenye udongo wa mfinyanzi unaotuamisha maji na kuzuia kusambaa kwa mizizi ya mazao kama karoti, bustani ya matairi ni suluhisho. Pamoja na tairi kuleta joto kwenye udongo kwa ajili ya mazao kama nyanya na viazi kukua, pia hukausha udongo hivyo kufanya maji yasituame na kuharibu mmea.
Huruhusu kupanda mapema
Kutumia matairi kupanda huruhusu kupanda mazao mapema kuliko sehemu nyingine katika bustani yako. Huna haja ya kuwa na hofu kulima wakati wa mvua kubwa kwa sababu udongo utalindwa na tairi usikutane na changamoto ya maji mengi au baridi kali pia.
Matunzo kidogo
Kazi kubwa ukilima kwa kutumia matairi itakuwa kumwagilia na kuweka mbolea tu. Kwa sababu mazao hayajapandwa chini hautapata kazi ya kupalilia mara kwa mara kama ilivyo desturi kwenye bustani za kawaida. Pia hii ni njia nzuri ya kutumia eneo dogo kwa kilimo mjini.




