Imekuwa ni kawaida kwa wakulima walio wengi kufanya shughuli zao bila kufanya maandalizi thabiti, na bila kuwa na mipango endelevu.
Jambo hili ni hatari sana kwa maendeleo, hii ni kwa sababu hautaweza kufanya kazi zako kwa malengo. Utakuwa mtu wa kuchukua kila linalokuja mbele yako, na mwishowe unajikuta haujaweza kufanya jambo la maendeleo na kutokufikia malengo pia.
Mwaka umeanza, endapo haukufanikiwa kujipanga na kuweka mipango thabiti kabla ya mwaka jana kwisha, bado hujachelewa sana. Kuna msemo usemao tunajifunza kutokana na makosa, hilo lilikuwa ni kosa la kutokupanga, lakini sasa unaweza kuibua mipango yako na ukapata mafanikio mazuri katika mwaka huu wa 2025.
Ni vyema sasa kujipanga na kufanya maandalizi: kuwa ni kilimo cha namna gani utafanya kwa mwaka huu, ni ufugaji wa namna gani unaotaka kufanya, na ni nini malengo yako? Mkulima Mbunifu liko nyuma ya mipango yako katika kuhakikisha kuwa linakusaidia kupata taarifa muhimu kwa kile ambacho umekusudia kufanya, iwe ni kilimo au ni ufugaji, pamoja na kukuhimiza kuingia katika usindikaji wa mazao utakayozalisha.
Endapo hauna wazo kuwa unataka kufanya nini basi soma yaliyomo kwenye jarida hili na bila shaka utapata pa kuanzia, ila kumbuka kuwa mbunifu ili kupata mafanikio zaidi.