- Binadamu, Kilimo, Kilimo Biashara, Kutuhusu, Masoko, Mazingira, Mifugo, Mimea, Redio, Shuhuda, Udongo, Usindikaji

Mwelekeo wa mvua za vuli (Oktoba – Disemba) na nini wakulima wafanye (Taarifa na TMA)

Sambaza chapisho hili

Uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli kipindi cha Oktoba – Disemba 2024, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya pamoja na menejimenti za maafa. Utabiri huu ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma). Kwa muhtasari, mwelekeo huo na athari

zake unaonesha kuwa:

  1. a) Mvua za Vuli, 2024
  2. Mvua zinatarajiwa kuwa za Chini ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuanza kwa kusuasua na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha.
  3. Mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2024 katika ukanda wa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2024. Mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2024.
  4. Mvua za Vuli zinatarajiwa kuongezeka kidogo mwezi Disemba, 2024.
  5. Vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu wa Vuli.
  6. Uwepo wa La-Niña hafifu unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu wa Vuli, 2024.

b) Athari zinazotarajiwa

  1. Upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi na hivyo kuathiri shughuli za kilimo.
  2. Kina cha maji katika mito na mabwawa vinatarajiwa kupungua.
  3. Kujitokeza kwa magonjwa ya mlipuko, kutokana na upungufu wa maji safi na salama.

Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki:

Katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro: Mvua za Chini ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki. Mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2024.

Kilimo na Usalama wa Chakula

Kipindi cha msimu wa mvua za Vuli, upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi yanayopata mvua za Vuli hususan maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa pwani ya kaskazini. Hali hii inatarajiwa kuathiri ukuaji wa mazao. Aidha, wadudu na magonjwa ya mazao yanatarajiwa kuongezeka katika msimu hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao. Vilevile, upatikanaji wa mazao ya misitu kama vile asali unatarajiwa kuathirika kutokana na uhaba wa maji na maua. Wakulima wanashauriwa kutumia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo.

Aidha, wanashauriwa kuandaa mashamba kwa wakati, kupanda mbegu na mazao yanayoweza kukomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame. Pia, wakulima wanashauriwa kupanda mazao tofauti tofauti yanayostahimili ukame ili kupunguza madhara yatakayoweza kujitokeza endapo zao moja litaathirika. Halikadhalika, mamlaka husika zinashauriwa kutoa elimu na uelewa kwa wakulima juu ya njia bora na namna ya kutumia kiwango kidogo cha mvua kinachotarajiwa pamoja na matumizi mazuri ya akiba ya chakula kilichopo. Wakulima pia wanahimizwa kupata ushauri kutoka kwa maafisa ugani kuhusu namna bora ya kuendesha shughuli za kilimo.

Mifugo na Uvuvi

Mvua chache zinazotarajiwa katika msimu zinaweza kuathiri upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo na chakula kwa ajili ya samaki. Hali hii inatarajiwa kuathiri uzalishaji wa mifugo, mazao ya mifugo na samaki. Katika msimu huu, magonjwa kwa mifugo yanayoenezwa na kupe pamoja na wadudu warukao yanatarajiwa kupungua. Halikadhalika, kutokana na upungufu wa malisho na maji kuna uwezekano wa migogoro kujitokeza baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Vile vile, uzalishaji wa zao la mwani unaweza kuathirika kutokana na vipindi virefu vya ukavu na joto vinavyotarajiwa. Jamii inashauriwa kuweka mpango mzuri wa matumizi na uhifadhi wa maji na malisho. Aidha, wafugaji na wavuvi wanashauriwa watumie taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani.

Tafadhali bonyeza hapa kwa taarifa zaidi

https://www.meteo.go.tz/uploads/publications/sw1724321444-Mwelekeo%20wa%20Mvua%20za%20Vuli%202024.pdf

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *