Boga lishe ni miongoni mwa vyakula vilivyopo katika kundi la mimea ya Cucurbitaceae au familia ya squash. Boga hili huwa na umbo la kibuyu na rangi yake huwa ni ya kijani mpauko kabla ya kukomaa na likikomaa huwa na rangi ya chungwa kwa nje na ndani.
Kwa sehemu ya nje, gamba lake huwa ngumu lakini likipikwa hulainika. Ndani ya mboga kuna mbegu ambazo pamoja na nyama ya ndani yake huliwa.
Kipande cha gramu 80 cha boga (lililochemshwa) huwa na gramu 0.5 za protini, gramu 0.2 za mafuta, gramu 1.5 za nafaka, gramu 1.4 za sukari, gramu 1.2 za faiba (nyuzinyuzi), miligramu 67 za potasiam, miligramu 764 za carotene na miligramu 6 za vitamini C.
Faida zigine za kula boga lishe ni pamoja na, kuboresha afya ya ngozi, kuboresha afya ya macho, kusaidia mfumo wa kinga ya mwili, kujenga mifupa na kusaidia kuzuia saratani.
Namna ya kusindika boga lishe
Boga lishe huweza kusindikwa na kupata unga ambao utatumika kupikia uji, ugali, supu na hata kuongeza kwenye mbogamboga kama kiambaupishi.
Hatua za usindikaji
- Chukua kiasi cha maboga unayohitaji kwa ajili ya kusindika.
- Osha maboga yote kwa maji safi na salama na hakikisha hakuna sehemu yeyote ya mboga yenye uchafu.
- Bila kumenya wala kutoa mbegu yake ya ndani, pasua kwa kutumia kisu kikali kisha kata maboga yote vipande vyembamba vidogovidogo kwa uwiano sawa.
- Vipangilie vipande vyote kimojakimoja kwenye kaushio la jua bila kuweka kipande juu ya kingine.
- Acha vikauke kiasi cha kuweza kusaga kupata unga. Yaweza kuchukua siku 5 au Zaidi kutegemeana na ukataji pamoja na hali ya hewa.
- Mara baada ya kukauka, saga vipande hivyo kupata unga kisha hifadhi kwenye mifuko maalumu ya kuhifadhia unga tayari kwa matumizi au kupeleka sokoni.
Muhimu: Unaweza pia kuchanganya na majani yake wakati wa kukausha.
Hii ni kwa kuchuma majani yalio laini, kuyamenya, kuosha na kisha kukata na kukausha pamoja kwenye kaushio la jua.