Tunapozungumzia lishe tunamaanisha kupata kiasi na ubora wa chakula na maji kwa vipindi vinavyofaa ili kuruhusu mwili kufanya kazi vizuri “balanced diet” yaani mlo kamili.
Mahitaji ya lishe hutofautiana kulingana na jinsia, umri, shughuli za kila siku, ujauzito/kunyonyesha na hali ya afya ya mtu binafsi.
Chakula kinapovunjwa, hutoa nishati ya kujenga mwili na kuupa kinga. Nishati hupimwa kwa kilokari au kilojuli. Vyakula tofauti hutoa kiasi tofauti cha nishati (kilokari) kwa gramu inayotumiwa. Nishati hii huupa mwili joto na hutumika kuruhusu seli za mwili kufanya kazi.
Chakula
Kula ni kitendo cha kiumbe hai kuingiza chakula ndani ya mwili wake kupitia mdomo wake. Kula humfanya kiumbe hai kuwa na nguvu. Viumbe hai wanahitaji kula ili miili yao iendelee kufanya kazi. Matatizo mbalimbali ya kiafya yanaweza kutokea kiumbe asipopata mlo kamili.
Vyakula vyenye afya kama vile mboga za majani, matunda, karanga na nafaka zisizokobolewa huwa na wingi wa lishe bora, vitamini, madini, nyuzinyuzi, protini na mafuta ya omega ni muhimu sana kwa miwli wa mwanadamu kwani unahitaji virutubisho hivi ili kufanya kazi.
Chakula hutupatia nishati na malighafi ya kufanya kazi muhimu za mwili kama vile kuondoa taka, kuzuia magonjwa na kudumisha mapigo ya moyo wako.
Sahani ya mlo unaofaa
Sahani ya Mlo unaofaa, ambayo imebuniwa na wataalamu wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Afya ya Jamii, Harvard na kuhaririwa na wataalamu kutoka Harvard, ni muongozo wa mlo kamili unaofaa kwa afya, ikiwa utatumiwa kwenye sahani ya mlo.
- Sehemu kubwa ya mlo wako uwe mbogamboga na matunda (½ ya sahani)
Hakikisha unaweka aina mbalimbali zenye rangi tofauti. Viazi mbatata havihesabiwi kama mbogamboga katika sahani ya mlo unaofaaa kwa sababu ya madhara yake kwenye kiwango cha sukari mwilini.
- Tumia vyakula vya nafaka isiyokobolewa (¼ ya sahani)
Vyakula vinavyotokana na nafaka isiyokobolewa kama vile ulezi, mtama, mchele wa brown vinaathari kidogo katika kiwango cha sukari mwilini na utengenezaji wa insulini kuliko vyakula vinavyotokana na nafaka iliyokobolewa.
- Nguvu itokanayo na protini (¼ ya sahani)
Samaki, Kuku, maharagwe, njugu, vyote ni vyakula vinavyoleta afya kutokana na protini vinaweza kuchanganywa na kachumbari. Punguza matumizi ya nyama nyekundu na epuka nyama za kusindikwa kama bacon na soseji.
- Mafuta yatokanayo na mimea kwa kiasi
Chagua mafuta yanayofaa ambayo yanatokana na mimea kama vile mizeituni, soya, mahindi, alizeti, karanga na mengineyo na epuka kutumia mafuta ambayo yameganda. Kumbuka kuwa alama ya “low fat” kwenye makopo ya mafuta haimaanishi “mafuta yafaayo kwa afya”
- Kunywa maji, kahawa au chai
Epuka vinywaji vyenye sukari, punguza matumizi ya maziwa na vyakula vitokanavyo na maziwa mpaka mara moja au mbili kwa siku, punguza matumizi ya juisi mpaka glass ndogo moja kwa siku.
Chakula salama na vihatarishi
Chakula salama ni uhakika kuwa chakula kikitayarishwa na kuliwa kama kilivyokusudiwa hakitaleta madhara kwa mlaji.
Vihatarishi na vyanzo vyake
Vihatarishi vya usalama wa chakula ni vile ambavyo kwa njia moja au nyingine vinaweza kufanya chakula kisiwe salama kwa matumizi ya binadamu.
Vihatarishi vya Kibailojia (biological hazards)
Vihatarishi hivi vinajumuisha vimelea vya magonjwa kama bakteria, virusi, minyoo (parasites) na prion (aina yap rotini ambayo huweza kuharibu protini ya kawaida kwenye ubongo na kukufanya kutokuwa sawa). Mara nyingi vinaingia katika chakula kupitia malighafi zinazotumika viwandani, mazingira ambayo chakula uandaliwa, binadamu au wanyama.
Wingi wa vimelea hivi hupunguzwa au kuondolewa kabisa wakati wa kupika au kusindika na pia kwa kudhibiti mfumo mzima wa uzalishaji, usindikaji na uhifadhi wa chakula (usafi, joto na muda).”
Kundi la pili vihatarishi vya Kikemikali (k).
- Hivi vinaweza kupatikana ndani ya chakula chenyewe au kuingia wakati wa uhifadhi au usindikaji. Sumu hizi zinakuwepo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa kinga dhidi ya uharibifu. Sumu zinazotumika kama kinga ni kama vile cyanide katika muhogo.
- Uchafuzi wa kemikali za sumu katika mazao ya chakula mfano sumukuvu.
- Vikolezo katika vyakula ambavyo husaidia katika usindikaji ikiwa vitaongezwa katika kiwango kisichokubalika na mabaki ya kemikali ambayo hutokana na kemikali zilizotumika kwenye kilimo, mifugo, au usafi wa sehemu za uzalishaji.
- Uchafuzi wa kemikali zilizopo kwenye kitu chochote kinachogusana na chakula (food contact materials), mfano vifungashio, vifaa vya majumbani vinavyotumika kuandaa chakula (sufuria, sahani, n.k).
Athari zitokanazo na chakula kisichokuwa salama
Athari za kiafya
Hizi huweza kujitokeza ndani ya muda mfupi (food poisoning) mfano; kuumwa tumbo, kutapika, kuhara na kuhara damu au baada ya muda mrefu mfano; kansa, upungufu wa kingamwili na udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano (5).
Athari za kibiashara
Kunaweza kutokea kukataliwa kwa bidhaa za chakula zisizo na viwango vinavyokubalika katika soko na hivyo kukosa mapato.
Athari za uhaba wa chakula
- Chakula kilichochafuliwa zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa hakifai kwa matumizi ya binadamu hivyo hutakiwa kuharibiwa.
- Athari za kuongezeka kwa gharama za matibabu na kupungua kwa nguvu kazi
- Uzalishaji mali hupungua kutokana na watu wengi kuwa wanaumwa na ndugu wa karibu kutumia muda mwingi kuwahudumia.
Nini kifanyike ili chakula kiwe salama
- Ili kuwa na chakula salama, unatakiwa mfumo thabiti wa usimamizi na udhibiti wa uzalishaji, usindikaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula.
- Lengo kuu la kuwa na mfumo imara wa chakula salama ni kujenga mazingira ambayo yatatoa uhakika wa uzalishaji chakula ambacho ni salama ili kulinda afya ya mlaji na kukuza biashara.
- Misingi imara ya usimamizi wa usalama inahusisha mambo yafuatayo; uwepo wa sheria, muundo wa kitaasisi (usimamizi), mfumo wa ukaguzi na ufuatiliaji, huduma za maabara na elimu kwa umma.
Mifumo endelevu ya chakula
Ni mfumo wa chakula unaotoa usalama wa chakula na lishe kwa wote kwa njia ambayo misingi ya kiuchumi, kijamii na kimazingira katika uzalishaji hauwezi kuathiri usalama wa chakula na lishe kwa vizazi vijavyo.
Kimazingira: Ni mfumo unaolinda viumbe hai, rutuba ya udongo, wanyama na mimea.
Kijamii: Ni mfumo unaolinda haki ya mwanadamu, afya na lishe. Unajali usawa wa kijinsia, tamaduni na makundi yote katika jamii.
Kiuchumi: Ni mfumo unaolinda uzalishaji wenye tija, na wenye kutoa ajira endelevu.
Kwa ujumla wake, mfumo huu hupelekea kupatikana kwa vyakula vinavyokubalika kitamaduni, kiuchumi vikiwa vya bei rafiki kwa wote, vyakula salama, na vyenye afya kwa njia ambayo inatoa usawa kwa mazingira na ustawi wa jamii.
Kwanini kubadili mifumo yetu ya sasa ya chakula
Kuna sababu kadhaa za kushindwa kwa mifumo yetu ya chakula kwa sasa;
- Mifumo yetu ya sasa ya chakula kutokuwa na uwezo wa kuzalisha kiasi kikubwa cha chakula ili kulisha idadi kubwa ya watu duniani inayoongezeka siku kwa siku.
- Mifumo yetu ya sasa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya lishe
- Mifumo yetu ya chakula kutokuwa na uwezo wa kumnufaisha kila mtu kwa usawa.
- Kuongezeka kwa athari hasi za mifumo ya chakula kwa mazingira na maliasili.
Jumla ya yote ni mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyozidi kuathiri mifumo ya chakula na wakati mifumo yenyewe inaendelea kuchangia kuwepo kwa mabadiliko haya.
Inakadiriwa kuwa, kati ya mwaka 2017-2019 watanzania takribani milioni 13 hawakua na chakula cha kutosha (Severely food insecure (WFP 2021) na asilimia 49% ya watanzania wanaishi chini ya dola 1.90 kwa siku (World Bank 2019).
Tunabadilisha mifumo yetu ya chakula ili;
- Kuwa na uhakika wa chakula, afya na lishe.
- Kubadili hali ya maisha kwa wakulima. Kilimo kinaajiri watu wengi hivyo ni lazima kujali hali zao za kimaisha.
- Kuzuia uharibifu mkubwa wa mazingira, viumbe hai na baiyoanuai.
Tufanye nini ili kubadili mifumo ya chakula
- Tunahitaji mbinu jumuishi ya mifumo ya chakula.
- Tunahitaji kufikiria zaidi ya mavuno ili kufahamu
Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Ayesiga Buberwa (Meneja miradi kutoka shirika la Iles De paix- IDP) kwa simu namba 0762 542 253