Mwaka umeanza ukiwa na baraka tele na habari njema kwa wakulima na wasomaji kwa ujumla. Kuanzia mwezi huu jarida lako ulipendalo la Mkulima Mbunifu (MkM) litakuwa likichapishwa na kuletwa kwako kila baada ya miezi miwili.
Tangu jarida hili lilipozinduliwa mwezi Julai 2011, limekuwa likichapishwa na kusambazwa kwa wakulima kila baada ya miezi miwili. Hata hivyo sababu ilikua ni kujenga msingi imara wa utoaji elimu na taarifa kwa wakulima.
Tangu mwaka 2014 hadi mwaka jana 2022, kipindi cha miaka nane, Jarida lilikua likichapichwa mara moja kwa kila mwezi na tumekua na wasomaji wengi ingawa kumekua na changamoto ya kutopata mrejesho na baadhi ya wasomaji kutopokea kwa wakati.
Kwa kuzingatia hilo, jarida litatolewa mara moja kila baada ya miezi miwili na litawafikia wakulima ambao tunataarifa zao kamili. Hii itatusaidia kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na wasomaji wa jarida.
Pia, tumeongeza kurasa nne ili kutoa nafasi ya waandishi kupambanua taarifa zaidi. Wakulima wanashauriwa kufuatilia katika masanduku yao ya posta, vikundi, taasisi zilizopo chini ya kanisa, mashirika ya kijamii, na taasisi zisizo za kiserikali ambazo huwa zinasambaza majarida haya, ili kuhakikisha kuwa hawakosi nakala kila toleo. Lakini, ukikosa nakala iliyochapishwa, usikate tama, unaweza kupata nakala yako kupitia kwenye tovuti yetu.
Endapo wewe ni mmoja wa wakulima na wafugaji wanaokua na kufanya shughuli zao kwa ufanisi, tutafurahi kusikia kutoka kwako ili tuweze kuwashirikisha wakulima wengine, nao waweze kupiga hatua kwa kujifunza kutoka kwako. Tunaamini kuwa wakulima wanaposhirikishana uzoefu, ni njia rahisi ya kila mmoja kujifunza kutoka kwa mwingine.
Somo ambalo umeweza kujifunza kutoka katika shughuli zako za kilimo na ufugaji, ni njia nzuri ya kuwasaidia wengine kutatua matatizo yanayowakabili katika shughuli zao.
Hivyo, itawasaidia kusonga mbele. Kwa pamoja, tuwasaidie wengine, usiwe mchoyo, wasiliana nasi ili tukutembelee na kuwapatia wengine yale uliyo nayo.
Napenda kujifunza ufugaji
Karibu Mkulima Mbunifu na fuatilia na soma makala zetu mbalimbali zilizopita na zinazoendelea kuchapishwa kupitia hapa hapa kwenye tovuti nawe utajifunza mengi.