Vijana wanaweza kujikwamua kiuchumi kwa kusindika mazao kutumia malighafi za hapa nchini.
Mvinyo ni neno linalotokana na neno la kireno vinho, ni kinywaji kinacho tengenezwa kutokana na majimaji ya matunda mbalimbali. Kuna aina nyingi za mvinyo kufuatana na matunda yaliotumika.
Katika Makala hii Mkulima Mbunifu inaangazia Kijana wa kike kutoka mkoani Mbeya alivyoamua kujitoa kimasomaso katika kusindika matunda kupata mvinyo aliouita SUITOR’S Sweet Red Wine (Mvinyo mwekundu).
Fursa katika kilimo hazikosekani mbali na kuzalisha mazao usindikaji wa mazao unafaida lukuki ikiwa jitihada zitazingatiwa. Hata hivyo ubunifu katika usindikaji ni muhimu ili kupata bidhaa yenye ushindani katika soko la ndani na pia nje.
Liliani aliamua kujifunza namna ya usindikaji wa matunda mbalimbali ili kupata mvinyo. Alipata mafunzo hayo kutoka SIDO (Small Industries Development Organisation). Aliamua kujiajiri ambapo alianza mwaka 2018 kwa kusindika lita 50-70 za mvinyo na sasa anauwezo wa kutengeneza lita 250- 300 kwa mwezi.
Anasema “Nilipata msukumo wa kuamua kutengeneza mvinyo huu baada ya kufanya utafiti na kugundua kuwa bidhaa nyingi za mvinyo zinazotumika Tanzania zinatoka nje ya nchi. Pamoja na kwamba malighafi za utengenezaji wa mvinyo yaani matunda yanapatikana Tanzania kwa wingi”.
Jinsi ya kusindika mvinyo kwa matunda mbalimbali:
Mahitaji.
- Sukari, zabibu, nanasi, rozela, machungwa, limao, maji na amira mama
- Kuandaa vifaa muhimu kama:- Refractometer, mzani wa digitali, kipima joto, vifaa vya kupikia, kuchuja na kuchanganyia.
Namna ya kuchanganya
- Chemsha mchanganyiko wa matunda rozela, zabibu na nanasi kwa vipimo maalum kulingana na kiasi cha mvinyo unao hitaji
- Tengeneza Amira mama kwa nia ya kuhifadhi chakula kwa njia ya asili bila kemikali kwa kutumia limao na chungwa.
- Chukua mchanganyiko wa matunda ulio chemka vizuri kisha kupoozwa kufikia joto la digrii 28, uchuje, weka sukari kwa kulingana na wingi wa mvinyo unao tengeneza kisha changanya na amira mama.
- Paki kwenye madumu maalum ya kufanyia fermantation na kuacha mchanganyiko huo kwa siku 30 – 90.
- Baada ya Mchakato wa kuvundika (fermentation) kuisha mvinyo utakuwa tayari hivyo unatakiwa kuchuja tena kwa umakini na kupaki kwenye vifungashio kwa usafi.
Faida gani ambazo Lilian amezipata toka aanze kutengeneza mvinyo?
Kama mjasiriamali mdogo ameweza kujiongezea kipato, kuendesha maisha ya familia yake, kupata fursa za kutambulisha bidhaa zake katika masoko ndani ya nchi pamoja na kupata nafasi ya kushiriki kwenye maonyesho mbalimbali ya kilimo na ufugaji (nanenane) mwaka 2020, yaliyofanyika kitaifa Mkoani Simiyu.
- 5. Changamoto anazokabiliana nazo katika kutekeleza kazi yake.
Kila penye mafanikio hapakosi changamoto, Bi Lilian anaelezea changamoto zinazomkabili katika utekelezaji wa kazi yake;
- Ufinyu wa vitendea kazi na vifaa vya usindikaji kuwa na uwezo wa kuzalisha kwa kiwango kidogo inapelekea kushindwa kuzalisha bidhaa kwa wingi na kushindana na wazalishaji wakubwa na kushika masoko kwa kasi kulingana na uhitaji.
- Ukosefu wa eneo la kudumu la kufanyia usindikaji wa bidhaa.
- Uhaba katika upatikanaji wa vifungashio kama chupa kulingana na saizi zinazo hitajika sokoni. vifuniko na madumu maalumu ya kufanyia fermentation.
- Gharama za uzalishaji kuwa kubwa kutokana na uwekezaji wa vifaa, vifungashio na mashine za uzalishaji kuwa juu.
- Kupata masoko kwa kuwa hajaweza kufikia maeneo engi kutokana na gharama za usafirishaji kuwa kubwa.
Kwa maelezo zaidi juu ya usindikaji wa matunda mchanganyiko, unaweza kuwasiliana na Lilian Rutenge kwa simu namba +255 717 557404.