- Kilimo, Mimea

Nimefanikiwa katika kilimo na ufugaji kupitia Jarida la Mkulima Mbunifu

Sambaza chapisho hili

Mimi ni msomaji wa jarida la Mkulima Mbunifu (MkM) toka mwaka 2011, na nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza shughuli zangu za kilimo na ufugaji kwa ufanisi kutokana na elimu inayotolewa na jarida hili.

Hayo ni maneno ya Bw. Silvester Gideon Mbulla (63), mkazi wa Kongwa (Hogoro), mkoani Dodoma, ambaye hakusita kuonyesha furaha yake mara tu alipokutana na mwandishi wa jarida hili katika mkutano wa Farm Radio International jijini Dodoma.

Alianzaje kupata jarida la MkM?

Bw. Mbulla anasema kuwa alisikia kuhusu jarida la Mkulima Mbunifu kupitia kipindi cha radio mwaka 2011, ambapo kulikuwa na taarifa kuhusu jarida hili na namna ya kulipata.  Hivyo,akajiandikisha na kutuma taarifa zake ili kuwa miongoni mwa wasomaji na wanufaika wa jarida hili.

“Niliposikia kuhusu jarida la MkM na namna ya kulipata, nilijiandikisha mapema kisha nikatuma taarifa zangu japo kwa wakati huo sikuwa na kikundi chochote. Nikaamua kuunda kikundi cha wakulima wenzangu kwa haraka tukiwa watano na tukatuma maombi yetu.

Mara tu baada ya wao kupokea taarifa zetu, walitupigia simu na wakaanza kututumia jarida mwezi uliofuata na mpaka sasa kikundi chetu cha Penpal chenye wanachama 15, kipo hai na bado kinapokea majarida ya Mkulima Mbunifu”.

Jarida la Mkulima Mbunifu lilimsaidaje katika uzalishaji?

Kabla ya kupata jarida la Mkulima Mbunifu, Bw. Mbulla anasema kwamba walikuwa wakijishughulisha na uzalishaji wa mazao mbalimbali kama ilivyo desturi ya wanajamii wengi nchini lakini siyo kwa utaalamu.

Aidha, mara baada ya kupata jarida hili, walianza kulima kitaalamu na kufanikiwa kupata ongezeko kwenye mavuno yao. Pia, wakajifunza juu ya mnyororo wa thamani na kuweza kuzalisha kwa tija.

Mbali na mazao ya kilimo, anasema kuwa wameweza kufanya ufugaji hasa wa kuku na nguruwe jambo ambalo hapo mwanzo walikuwa hawafanyi.

Wakulima wengine wameanza kujihusisha na usindikaji wa bidhaa mbalimbali.

“Kupitia kitabu cha kuku, na cha nguruwe, nimehamasika kufanya uzalishaji wa kuku na ufugaji wa nguruwe, kitu ambacho sikuwa nacho huko mwanzo lakini kupitia jarida hili nimejifunza na nikafanya kwa vitedo”.

Aidha, ameongeza kuwa ameweza pia kuhamasika kufanya kilimo cha mahindi, karanga, alizeti na mbogamboga kwa tija. Hivyo, kwake jarida hili ni zaidi ya kusoma kwani kile anachokisoma kinatekelezeka kwa vitendo na faida yake inaonekana.

Mafanikio

  • Kupitia kusoma jarida hili amefanikiwa kuongeza kipato chake na kuweza kumudu mahitaji ya kifamilia kama chakula na mavazi.
  • Anaongeza kuwa, ameweza kufanya kilimo chenye tija ambacho kimemuwezesha kupata fedha na kusomesha watoto kwenye ngazi mbalimbali za elimu.
  • Kubwa zaidi, ni elimu ya uzalishaji ambayo anajivunia kwani hazalishi tena kwa mazoea bali kitaalamu, hivyo kuongeza uzalishaji.

Changamoto

Bw. Mbulla anasema changamoto wanayopata kama kikundi cha Penpal na wasomaji wa jarida hili ni kutokuwa na sanduku la posta la kwao binafsi. Wakati mwingine majarida yanachelewa kuwafikia kwani wanatumia sanduku la posta la kijiji chao.

Wito kwa wakulima

“Nawashauri wakulima ikiwezekana wahakikishe wanalipata jarida hili kila mwezi kisha kulisoma na kufanya kwa vitendo yale yaliyoandikwa ili waweze kufanya kilimo chenye tija.

Kama wana maswali yoyote kuhusiana na kilimo na ufugaji, wasisite kutuma kwa Mkulima Mbunifu kwani yatajibiwa kwa wakati. Sisi ni mashuhuda tumekuwa tukituma maswali na kupata utatuzi”, anasema.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Nimefanikiwa katika kilimo na ufugaji kupitia Jarida la Mkulima Mbunifu

    1. Habari, Karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala zetu. Ungependa kufahamu nini kwenye kilimo cha ndizi? Na unaposema kuku cross unamaanisha kuku wa aina gani?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *