Kuna njia kadhaa za kuongeza idadi ya kuku kama vile kununua kuku wakubwa, kununua vifaranga kutoka kwa wafugaji wengine, kuzalisha vifaranga kutokana na kuku waliokomaa au kutotoa kwa kutumia mashine ya inkubeta. Mbinu inategemea uwezo na uzoefu wa mfugaji.
Kila mfugaji angependa kupanua kiasi ya ufugaji wa kuku na kujiongezea kipato. kutokana na mauzo ya kuku au mayai. Kufuga kuku wengi wenye umri moja ni njia ya haraka na uhakika ya kufikia lengo.
Wafugaji wengi ambao wana lengo hili la kufuga kuku wengi wa umri mmoja na kupata mayai mengi au kuweze kuuza kuku wengi kwa wakati mmoja inabidi awe na vifaranga wengi wa umri mmoja. Hii inaambatana na uangalifu mkubwa katika kuwalea vifaranga ili kupunguza maafa zinazotokana na usimamizi usiofaa na unaoleta magonjwa au afya dhaifu.
Vifaranga wengi
Kuna manufaa ya kuwalea vifaranga wengi kwa wakati mmoja, ikiwa ni pamoja na;
- Kupunguza gharama za ufugaji kwa mfano chakula, chanjo na tiba.
- Kutunza kuku kitaalamu kwa urahisi
- Kupata mayai mengi kwa wakati mmoja
- Kuuza kuku wengi kwa wakati mmoja
- Kuwapa uhakika wateja wako, kwamba utatimiza kiasi wanachotaka.
Kuna njia kuu mbili za upatikanaji wa vifaranga wengi kwa wakati mmoja nazo ni;
- Kwa kuhatamiza kuku wengi kwa wakati mmoja
- Kwa njia ya mashine ya kuangulia inkubeta
Njia zote mbili huweza kutoa vifaranga bora bali uchaguzi wa njia ipi itumike utatokana na mtaji wa mfugaji na mahali alipo.
Kwa kuhatamiza kuku wenyewe
Wafugaji wadogo wote hutumia njia ya kiasili kuhatamisha na kuangua mayai. Hii ni njia ya kutumia kuku au ndege mwingine ambaye hupewa mayai na kuyahatamia hadi kuanguliwa. Kuku wa kienyeji ni wazuri sana wanapotumiwa kwa ajili ya uzalishaji wa vifaranga. Hata hivyo, kwa uzalishaji mzuri ni lazima mfugaji ahakikishe kuwa kuku anapewa mayai yenye uwezekano mkubwa wa kuanguliwa. Haya ni mayai ambayo hayajakaa sana na yaliyohifadhiwa vizuri.
Kuchagua mayai
Mbinu moja wapo ambayo mfugaji anaweza kuitumia kutambua mayai yenye uwezekano mkubwa wa kuanguliwa ni kwa kumulika kwa kutumia mshumaa. Mayai yanaweza kuwekwa kwenye mwanga mkali ambao utakuwezesha kuona ndani ya yai.
Kifaa rahisi cha kumulika mayai kinaweza kutengenezwa kutokana na kuweka balbu ndani ya boksi dogo. Unakata tundu dogo kuruhusu mwanga. Hakikisha linakuwa na ukubwa wa kuweza kuruhusu yai kukaa juu yake. Shika yai kwa kulisimamisha kwa kutumia vidole vyako viwili, kisha liweke kwenye mwanga wa tochi au balbu. Zoezi hili linakupa uhakika kuwa mayai yenye uwezekano wa kuanguliwa ndiyo pekee yanayochaguliwa.
Sifa za mayai ya kuhatamisha
- Mayai ya siku ya mwisho kutagwa ndio yawe ya kwanza kuwekwa yafuatiwe na ya siku zinazofuata yasizidi wiki mbili tangu kutagwa
- Lisiwe kubwa sana au la duara, lisiwe na uvimbe
- Yasiwe machafu wala yasiwe na nyufa
Sifa za tetea wa kuhatamia
- Kuku mwenye umbo kubwa
- Mwenye uwezo na historia nzuri ya kuhatamia na hatimaye kutotoa vifaranga
Sifa za kiota na chumba cha kuhatamia
- Kuku wanaohatamia watengwe katika chumba ili kuondoa tatizo la kutagiana.
- Mlango na dirisha viwekwe wavu ili muda wa mchana mwanga na hewa uweze kuingia ndani.
- Chumba kiwe na nafasi ya kutosha kuweka viota, chakula na maji.
- Ili kutumia eneo vizuri viota vinaweza kutengenezwa ukutani kama mashelfu.
- Viota viundwe vizuri kwa nyasi, maranda makavu ya mbao, au nguo ya pamba lakini isiyo tetroni.
- Viota visiwe sehemu yenye unyevunyevu.
- Idadi ya viota vilingane na idadi ya matetea walio chaguliwa kuatamia
- Vinyunyiziwe dawa ya kuuwa wadudu kama utitiri kwani hawa ni wadudu wasumbufu ambao husababaisha kuku kutokatoka nje, hivyo kupunguza uwezekano wa mayai kuanguliwa yote.
Chakula, vitamini na maji
Kuku wanaohatamia wapewe chakula cha kuku wakubwa wanaotaga (layers mash) cha kutosha muda wote kiwemo kwa kua kuku hawa hutoka wakati tofauti pia majani, mboga-mboga na maji ya kunywa ni muhimu sana.
Vyote hivi viwekwe kwenye chumba ambacho kuku wanahatamia ili kumfanya kuku asiende umbali mrefu kutafuta chakula pia kuyaacha mayai kwa muda mrefu.