Mkulima Mbunifu imekua ikitembelea wakulima mbali mbali nchini Tanzania ili kuchukua shuhuda mbalimbali za wanufaika na kuzichapisha ziwe chachu kwa wasomaji wengine kujifunza na kufanya kwa vitendo. Je wewe umejifunza nini kutoka Mkulima Mbunifu? Tafadhali tuandikie kupitia mawasiliano yaliyo katika jarida hili.
Katherini Samweli Palanjo, Kijiji cha Sura-Meru, Arusha
Mimi ni mkulima wa kilimo hai, ninajishughulisha na kilimo cha mboga mboga, mahindi, karoti na viazi lishe. Pia ni mfugaji wa kuku wa kienyeji na nina mizingga ya nyuki ambayo ninapata asali ya kuuza na matumizi ya nyumbani kama dawa. Mimi ni kiongozi na muwezeshaji wa kikundi cha wakulima katika eneo langu. Nimekua nikipokea jarida la Mkulima Mbunifu tangu mwaka 2015, kila jioni baada ya shughuli za shambani hupitia jarida hili ambalo limenisaidia kujifunza mambo mengi hasa kuhusu kilimo hai. Nimefanya kwa vitendo na natumia uzoefu huo kuwafunza wana vikundi wenzangu kupitia shamba langu.
Kilimo kimenisaidia niweze kujikwamua kiuchumi kwani ninasomesha watoto wangu na kupata mahitaji ya nyumbani ya kila siku.
Wito kwa kina mama: Wakina mama tujifunge viuno tujishughulishe na shughuli za kilimo na ufugaji kwani bidii huzaa matunda.
Bw. Seth Zacharia, Meru-Arusha
Mimi ni mfanyakazi katika dayosisi ya Meru, katika mradi wa Afya na Maendeleo. Mradi huu unavipengele vitatu ambavyo ni uhakika na usalama wa chakula (Food Security), elimu kuhusu maambukizi ya VVU na pia ushawishi na utetezi wa haki za binadamu.
Tuna jumla ya wakulima 4500 katika wilaya ya meru ambao huwatembelea na kuwapatia elimu juu ya kilimo bora. Tulianza kupokea majarida ya Mkulima Mbunifu mwaka 2014 mpaka sasa, sisi hutumia majarida haya kufundishia wakulima kulingana na hitaji la mkulima mwenyewe. Tumekua tukichukua maarifa kutoka kwenye jarida na kujibu maswali mbalimbali yanayohusu changamoto za kilimo kwa wakulima wetu. Majarida haya yamekua yakisambazwa kwa wakulima pindi tuyapokeapo.
Wito kwa Mkulima Mbunifu: Tumekua tukipata maswali kwa wakulima juu ya masoko ya bidhaa zao kwani kipindi cha mavuno inakua ni changamoto kujua mahali pa kuuza bidhaa hizo. Hivyo wakulima wanashauri kama kunauwezekano jarida litoe taarifa juu ya masoko mbalimbali ya bidhaa ili mkulima aweze kufuatilia.
Evarina Peter, Mkulima kutoka Babati
Mimi ni mkulima wa nyanya kutoka wilaya ya Babati Mkoani Manyara. Mimi ni mlemavu wa miguu. Nina watoto wanne ambao wananitegemea, kilimo ndio tegemeo langu kiuchumi. Jirani yangu hupokea jarida la Mkulima Mbunifu, ambapo huniletea nisome. Mimi na walemavu wenzangu tunakikundi chetu ila hatujawai kupokea jarida. Kwa kua ulemavu sio kulemaa, ninaomba Mkulima Mbunifu watutumie jarida na sisi tuweze kufaidika na elimu hii ya kilimo endelevu.
Nimeona wenzangu wakifanya kilimo biashara na kufaidika kwa kufuata kanuni za kilimo endelevu, bila kutumiwa kemikali yoyote, kwasasa nimeanza kuandaa mbolea ya mboji kwaajili ya zao la nyanya. Nimejifunza kutengeneza mboji kutoka kwa mnufaika wa jarida la Mkulima Mbunifu.
Wito kwa walemavu: Ninawashauri watu wenye ulemavu kutafuta mbinu za kujishughulisha kufuatana na uwezo ulionao ili kujikwamua kiuchumi kwani ulemavu sio kulemaa.