Mara nyingi wakulima na wafugaji wamekua wakipata shida kwenye shughuli zao za kila siku kutokana na ukosefu wa maji. Maji yamekua ni moja ya sababu inayofanya wafugaji kuhama eneo moja kwenda lingine sambamba na wakulima kuhamia maeneo ambayo watapata uhakika wa uzalishaji wa mazao yao. Madhara ya mafuriko na ukame yanaweza kuongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya hew ana hivyo kupelekea wastani wa watu karibu 45,000 kuathirika kwa mafuriko kila mwaka nchini Tanzania.
Ni ukweli usiofichika kuwa kipindi cha mvua maji mengi hupotea kutokana na kukosekana kwa mbinu rahisi ya kuyavuna na kuyahifadhi maji hayo yanayotiririka ambayo yangeweza kusaidia jamii nyingi hasa kipindi cha ukame. Mojawapo wa Mbinu rahisi ya kuvuna maji ya mvua ni kwa kutumia Silanga (water reservoir).
Silanga ni muundo wa bwawa la wazi linaloweza kutumika kuvuna maji ya mvua kwa njia ya paa za nyumba na kuyahifadhi kwa matumizi ya baadae kama vile umwagiliaji, kunyeshea mifugo, matumizi ya nyumbani, au katika matumizi ya utunzaji wa mazingira. Silanga ni mbinu yenye mchango mkubwa katika kuhakikisha inapunguza upotevu wa maji kipindi cha msimu wa mvua na hivyo ni moja ya mbinu bora kutumika kwa jamii ya Kitanzania hususani vijijini ambapo uhaba wa maji ni moja ya kikwazo katika kufanikisha shughuli za kila siku.
Namna ya kutengeneza silanga
Utengenezaji wa muundo wa uvunaji wa maji ya mvua kwa kutumia Silanga kwa kaya ni vyema ukazingatia yafuatayo; utaalamu wa kuandaa shimo la kukusanya maji kwa kuzingatia vipimo linganifu, hali ya kipato cha kaya kwa maana baadhi ya vifaa kama nailoni ngumu nyeusi ya bwawa huwa na gharama (dam liner), uwepo wa uzio wa silanga kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.
Mahitaji muhimu katika kuaandaa silanga ni yafuatayo
- Shimo lililochimbwa kwa kuzingatia marefu na mapana kulingana na kiasi cha maji kinachotarajiwa kuvunwa mfano shimo la kuvuna maji lita elfu 50 linatakiwa kuwa na vipimo vya urefu mita 7.5 upana mita 5.5 na kina kwenda chini mita 1.5
- Nailoni ngumu nyeusi yenye upana mita 8 na urefu mita 13 itakayotumika kufunika shimo lote
- Uzio kuzunguka shimo kwa ajili ya usalama na kuzuia uharibifu unaoweza kutokea kutokana na mifugo kama ng,ombe, mbuzi kuingia
- Uwepo wa Neti kufunika Silanga kwa juu (Shade Net) kwa ajili ya kukinga upotevu wa maji kwa njia ya mvuke na kuleta usafi na usalama wa maji yaliyopo kwenye silanga
Faida za kuvuna maji kwa kutumia silanga
- Uvunaji wa maji ya mvua kwa kutumia silanga linaweza kusaidia uhitaji wa maji kwa matumizi ya binadamu au shughuli mbalimbali hasa kwenye maeneo yenye uhaba wa maji.
- Uvunaji wa maji ya mvua kwa kutumia silanga huweza kudhibiti mmonyoko wa udongo, mafuriko na uchafuzi wa mazingira unaotokana na mtitirriko wa maji. Hili linasaidia kulinda mazingira na rasilimali zinginezo muhimu katika ardhi kama vile rutuba, bioanuai na ubora wa maji
- Uvunaji wa maji ya mvua kwa kutumia silanga huongeza upatikanaji na uhakika wa maji kwa mifugo na kufanya uboreshaji wa afya ya mifugo, bidhaa bora na ongezeko la mifugo.
- Uvunaji wa maji kwa kutumia silanga huweza kuongeza kipato kwa kaya kupitia uanzilishi wa miradi ya ufugaji wa samaki na uzalishaji wa miche ya mazao ambayo kaya inaweza kuuza na kujipatia kipato cha ziada.
Shirika la IDP lilipo Arusha Tanzania limekua na mchango mkubwa katika kubadili maisha ya wakulima wadogo wawanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi wa Kilimo Endelevu katika wilaya za Karatu na Arusha ambapo takribani wakulima wapatao 1,600 kutoka Karatu na 680 kutoka wilaya ya Arusha watanufaika kwa kwenye Mradi huu. Mpaka sasa Kaya zisizopungua 325 na shule takribani 10 ni wanufaika wa moja kwa moja katika kutumia mbinu hii ya uvunaji wa maji ya mvua kwa kutumia Silanga.
Mafanikio haya yote yametokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Tanzania kwa shirika la IDP Tanzania sambamba na mchango mkubwa kwa mashirika ya kimaendeleo ya ufaransa Agence Française de Développement (AFD), ubalozi wa Ufaransa Tanzania, Shirika la Maendeleo la Kibelgiji Directorate-General for Development Cooperation and Humanitarian Aid (DGD) na Luxembourg (MAEE Lux)
Kwa maelezo zaidi wasiliana na Iles de Paix Tanzania kwa simu namba 0789352021