Usimamizi wa rutuba ya udongo sio tu kuweka mbolea au kupata mavuno mengi peke yake. Ni kuhusu kujenga udongo wenye rutuba thabiti na hai.
Mifumo ya kilimo yenye uzalishaji endelevu inahitaji usimamizi mzuri wa rutuba ya udongo ili kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu wa uzalishaji wa chakula wa kwao wenyewe. Ndio sababu kwa nini usimamizi sahihi wa rutuba ya udongo ni wa umuhimu sana katika uzalishaji wa mazao na kilimo katika kilimo-hai.
Kimsingi wakulima wa kilimo hai hushughulikia rutuba ya udongo kwa kuhifadhi na kulinda udongo wao dhidi ya jua, mvua na upepo na kulisha mabaki ya viumbe hai kwa njia inayofaa, ili kuuruhusu kulisha mimea katika urari sahihi wa virutubisho. Udongo unapokua na rutuba kwa maana ya kilimo hai, unaweza kuzalisha mavuno mazuri ya mazao kwa miaka mingi.
Mbinu ya hatua tatu
Usimamizi wa rutuba ya udongo katika kilimo hai unaweza kuchukuliwa kama ni mbinu inayotumia hatua tatu, ambapo kila hatua inajenga msingi wa hatua inayofuata.
Lengo ni kuhimiza udongo kurudia hali ya asili na kupunguza matumizi ya mbolea za viwandani, viongezwa vya kurekebisha hali ya udongo na maji ya umwagiliaji.
Hatua 1 – Kuhifadhi udongo, mboji na maji kutokana na upotevu.
Hatua 2 – Kuboresha kiwango cha mboji katika udongo
Hatua 3 – Kushamirisha mahitaji ya virutubisho pia kuboresha mazingira ya kukua mimea kwa kutumia baadhi ya viongezwa vya kurekebisha hali ya udongo.
Hatua ya kwanza
Katika hatua ya kwanza, wakulima wa kilimo hai wanalenga kujenga udongo thabiti ambao haupati athari za mmomonyoko kwa urahisi kama msingi wa kusimamia udongo wenye rutuba. Wanafanya hivi kwa kufanya yafuatayo:
- Kuzuia udongo usimomonyoke kutokana na mvua au upepo kwa kuufunika kadri inavyowezekana. Wanafunika udongo kwa kutumia mimea hai hasa kwa mazao ya kudumu au kufunika na mimea iliyokufa (matandazo). Pia wanachimba na kujenga vizuizi kukatisha mteremko ili kupunguza kasi ya mwendo wa maji ya mvua kuelekea kwenye mteremko.
- Kupunguza kutifua udongo. Wakulima hutifua ardhi kidogo sana au hatifui ardhi kabisa, na kuruhusu matayarisho ya ardhi mapema kabla ya mvua kubwa. Kilimo cha aina hii huifadhi umbile la udongo hupunguza hatari ya udongo kuwa mgumu, kuongeza upenyaji wa maji ardhini, kupunguza maji kutiririka ovyo na kuboresha hifadhi ya maji.
Hatua ya pili
Katika hatua ya pili, lengo ni kujenga udongo hai wenye umbile zuri, ambao unaweza kuhodhi maji na kuipatia mimea virutubisho.
Wakulima wa kilimo hai wanafanikisha hili kwa kutumia mbinu ambazo huboresha wingi wa mboji katika udongo na kukuza shughuli za viumbe hai kwenye udongo. Mbinu hizo zinajumuisha:
- Kupanda mbolea za kijani, mara nyingi hii ni mimea aina ya mikunde kwa ajili ya wingi wa majani na matawi wanayozalisha. Mimea hii ikishakua inakatwa na kuchanganywa kwenye udongo ili kulisha viumbe hai kwenye udongo na virutubisho kwa mimea inayofuata.
- Kilimo mseto kwa mazao yanayofunika udongo kama vile maharage yanayotambaa na mazao mengine yanayotambaa kama matandazo hai. Kwa kawaida mazao haya hufyekwa mara kwa mara ili yasishindane sana na zao kuu.
- Matandazo na mabaki ya magome au miti ambayo huchukua muda mrefu kuoza. Hii huoza taratibu na kuchangia katika kuongezeka kwa mboji muda unavyokwenda.
- Kupanda miti na vichaka kwaajili ya kilimo mseto kwa mashamba yenye mazao katika kingo za mashamba yenye mazao au mashamba yaliyolimwa lakini hayajapandwa, ambapo majani na matawi hupunguzwa mara kwa mara na kutumika kama matandazo.
- Kurudisha shambani mabaki ya mavuno kama makapi, majani, mizizi, maganda, matawi na vitawi ikiwa kama mboji, matandazo au kitu cha kuongezea kwenye udongo.
- Kuongeza mboji inayotokana na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, kwa mfano maranda, au maganda ya kahawa au mchele.
- Kuingiza mifugo shambani kwa ajili ya kupata mbolea mara kwa mara na malalo kwa ajili ya matandazo.
Hatua ya tatu
Katika mazingira ambayo pamekuepo na matumizi makubwa ya virutubisho au mazingira yasiyofaa kwa mmea kukua vizuri, wakulima wa kilimo hai hutumia njia za kuongeza virutubisho ambazo ni muhimu kuhakikisha maboresho ya mazingira ya ukuaji wa mmea:
- Kutumia mbolea ya maji kudhibiti mapungufu ya muda ya virutubisho na kuchochea kukua kwa mimea. Mbolea za maji zinatokana na mbolea za mifugo, mboji au majani au miti mibichi yenye naitrojeni nyingi.
- Kutumia mbolea za kilimo hai ambazo hazina mabaki ya kemikali, kama zinapatikana au zenye bei nafuu. Mifano inajumuisha mashudu ya alizeti na mbegu za mafuta, mbolea ya kuku iliotengenezwa kama punje punje, mabaki ya viwanda vya bia, maganda , makapi ya kahawa, Maranda na vumbi la randa, makapi ya mchele majivu ya mimea, n.k.
- Kutumia viongezwa kama vile chokaa ili kurekebisha kiwango cha uasidi kwenye udongo na mbolea inayotokana na viumbe hai vya kwenye udongo, kwa mfano mizizi ya kuvu aina ya rhizobium na mycorrhiza ili kukuza mchakato wa kuongezeka kwa madini na naitrojeni kwenye udongo.
- Kutumia umwagiliaji ili kushamirisha mahitaji ya maji kwenye udongo.
Maelezo haya yametoka kwenye kabrasha ya mwongozo wa mafunzo ya kilimo hai Afrika. Kwa maelezo zaidi wasiliana na TOAM Tanzania, Mob: 0732975799