Katika matoleo mengine ya gazeti hili, tutaangazia mahitaji maalum kwa kila aina ya ufugaji wa mifugo ili kuhakikisha tunatembea nawe hatua kwa hatua katika kuanzisha na kukuza biashara yako. Ukiwa na swali au ungependa aina fulani ya ufugaji liangaziwe, wasiliana na MkM, na utujulishe hitaji lako ili tuendelee kushirikishana mafunzo.
Ufugaji unachangia maendeleo
Biashara za ufugaji hupata pesa kupitia uuzaji wa mifugo yao iliyokuzwa na rasilimali zingine ambazo mifugo inazalisha.
Kwanza, uzalishaji wa mifugo huongeza upatikanaji wa vyakula vya asili vya wanyama ambavyo ni vyanzo vya protini na virutubishi vingine vinavyohitajika na mwili kwa viwango vidogo, na ni muhimu kwa watu wenye afya. Kaya zenye mifugo hutoa lishe bora kwa wanafamilia wote; wanakula nyama, mayai, na vyanzo vingine vinavyotokana na wanyama.
Pili, uzalishaji wa mifugo huchangia maendeleo ya kiuchumi katika ngazi ya kaya na jamii kupitia kazi hii ya kipato na kuweka akiba. Mnyama anayetembea ni mali, rasilimali inayotumika kuzalisha zaidi, na ni akiba inayoweza kubadilishwa kuwa pesa taslimu sokoni, na kutumika kugharamia mahitaji tofauti ya familia, mfano, kulipa karo shuleni.
Tatu, kuna kipato kwa wafanyabiashara wa bidhaa na huduma zinazotumika na wafugaji. Daktari wa mifugo anapata sehemu yake, muuza chakula cha mifugo dukani, afisa ugani, wasimamizi serikalini, watafiti, mchinjaji, mchuuzi na wengine wengi wanachuma kipato kutokana na ufugaji.
Nne, na kutokana na hayo, nafasi ya uzalishaji wa mifugo katika maendeleo ya taifa ni kubwa.
Tafuta nafasi yako na ujikite, ujenge na upate sehemu yako ya kipato cha sekta hii!