Mkulima anaweza kupunguza gharama, kuongeza rutuba kwenye udongo, mavuno pamoja na kipato kwa kutengeneza mbolea mwenyewe.
Mimea inaweza kukuonyesha inahitaji nini. Ni rahisi sana kugundua endapo mimea haipati virutubisho vya kutosha. Majani kubadili rangi ni ishara tosha kuwa mimea ina upungufu wa virutubisho. Ni lazima mkulima awe tayari kutatua tatizo hilo kwa haraka kabla hali haijawa mbaya. Upungufu wa madini ya nitrojen na fosiforasi ni jambo la kawaida kwa mimea. Virutubisho hivi vinahitajika kwa kiasi kikubwa sana kwenye mimea hasa katika hatua ya ukuaji.
Wakulima wengi wamekua na imani kua mbolea za viwandani zinatija kwa mkulima kwani inakuza mazao kwa haraka. Ilhali hili limekua kimbilio kwa baadhi ya wakulima, Bwana Albert Samawa Mkulima kutoka Karatu wilayani Manyara ameweza kujifunza na kubuni jinsi mbolea ya maji inaweza kuboresha mazao shambani.
Akiwa mfano kwa wakulima wengine ambao bado wanatumia mbolea za viwandani, ameamua kuita mradi huu turudi asili. Turudi asili akimaanisha wakulima tutumie mbolea ya asili, na mradi huu unahusu mbolea ya asili ya maji. Bwana Albert Samawa ni mkulima kutoka wilaya ya Manyara. Yeye anajishughulisha na shughuli za kilimo hai. Ni mkulima wa mboga mboga, nyanya pia matikiti maji. Bwana Albert amekua akitumia mbolea hii ya maji ya asili katika kukuza mazao yake. Kutokana na hilo amejishughulisha kufunga teknolojia hio kwa wakulima wengine na kujipatia kipato.
Mahitaji ya mbolea ya maji
- Kinyesi cha ng’ombe, popo, sungura, kuku, nguruwe
- Tanki 1 ya lita 1000, au jaba hii inategemeana na kiasi cha mbolea kinachohitajika shambani.
- Mifuko ya salfeti ya kilo 30-50 kwaajili ya kuwekea mbolea
- Kamba ya manila kwaajili ya kufungia mifuko ya mbolea
- Kijiti cha kuwekwa juu ya tanki ili kufungia mifuko yenye mbolea
- Kijiti kwaajili ya kukorogea maji ndani ya tanki
- Karatasi nyeusi ya polythene
- Kiunganishi (connector) ili kupeleka maji ya mbolea shambani kama ni shamba la umwagiliaji wa matone.
Uandaaji
Aina hii ya mbolea hutengenezwa kwa kuchukua kiroba kilichojazwa samadi, aina mbalimbali ya mimea yenye virutubisho na inayoaminika kuwa dawa ya mimea. Kiroba hicho kinafungwa kwenye kijiti, na kutumbukiza kwa kuning’inia kwenye pipa lililojazwa maji. Kiroba hicho ni lazima kichukue kati ya kilo 30-50 za samadi pamoja na aina nyingine za mimea kwa maji lita 500 ndani ya tank la lita 1000.
Mkulima anaweza kushika upande mmoja wa mti na kunyanyua na kushusha kila baada ya siku saba ili kuchanganya na kuharakisha kutolewa kwa virutubisho zaidi. Au anawez kutumia kijiti kukoroda maji kwa kutingisha magunia ya mbolea. Kwa kawaida mchanganyiko huo unakuwa na harufu kali sana maana Nitrojeni nyingi inayopatikana hugeuka kuwa Amonia. Ni vizuri kufunika pipa na karatasi nyeusi ya polythene ili kuzuia kuyeyuka kwa nitrojeni. Harufu ikishaisha, ujue mbolea yako ipo tayari kwa matumizi. Ongeza maji na utingishe vizuri kabla ya kutumia. Nyunyizia mimea yako kila wiki mpaka utakapoona mabadiliko.
Faida
Mkulima anaweza kusaidia hatua hii ya kulisha mimea inayokuwa kwa njia ya kunyunyizia mbolea ya maji. Kunyunyizia inasaidia kuipatia mimea virutubisho moja kwa moja kupitia kwenye majani na shina.
Unaweza kuona matokeo mazuri ya kuweka mbolea kwa kunyunyizia kulingana na kiwango cha mavuno, uwezo wa mimea kukabiliana na wadudu pamoja na magonjwa, kuvumilia ukame, na kuongeza ubora wa mazao. Mimea inakuwa na uwezo wa kunyonya mbolea mara 20 zaidi ya unapotumia aina nyinginezo za uwekaji wa mbolea kwenye mimea.
Vigezo vya kunyunyizia
Ili mbolea ya kunyunyizia iwe na matokeo mazuri, vigezo vifuatavyo vifuatwe:
• Inashauriwa kutumia mbolea iliyochanganywa vizuri ili kuepukana na kuunguza mimea.
• Acha maji utakayotumia kuchanganyia mbolea yako nje katika pipa lililowazi usiku kucha, hii inasaidia kutoa madini hatarishi, na kufanya mchanganyiko wenye faida kwa mimea.
• Tingisha vizuri. Chembechembe ndogo ambazo hazikuyeyuka zinaweza kuziba mdomo wa bomba la kunyunyizia.
• Matokeo mazuri yanaweza kupatikana endapo mbolea imechanganywa vizuri na kunyunyiziwa wakati hakuna upepo.
• Nyunyiza mbolea wakati wa asubuhi au jioni wakati hakuna joto na upepo ukiwa umepungua.
Changamoto
Bwana Albert anaeleza changamoto anazokumbana nazo ni pamoja na wakulima kutoamini, kutokana na mazoea ya mbolea za viwandani. Muitikio wa jamii kuhusu mbolea hii umekua taratibu. Baadhi ya watu ambao amewafungia teknolojia hii wemeweza kushuhudia faida yake.
Kwa maelezo zaid kuhusu teknolojia na mbolea ya maji wasiliana na Bwana Albert Samawa, Namba ya simu 0763824178