- Kuku, Mifugo

Maswali ya wafugaji wa kuku na majibu ya wataalamu

Sambaza chapisho hili

Swali: Endapo nitachanja kuku wangu dhidi ya mdondo lakini jirani zangu hawakuchanja kuku wao, je kuku wangu hawataathirika na ugonjwa unapotokea kwa majirani?

Jibu: Kinga itokanayo na chanjo hufikia kiwango cha juu kabisa siku ya 14 na endapo ugonjwa utafika kwa jirani yako wakati kuku wako wamekwisha fikia kiwango kizuri cha kinga basi ni dhahiri kwamba hawataathirika kwa ugonjwa huo.

Swali: Wakati mwingine tunapochanja kuku kwa kutumia I-2 kuku wetu huanza kufa kwa wingi. Je, hii inatokana na nini?

Jibu: Chanjo yoyote inapaswa kuchanjwa kwa kuku wasio wagonjwa na ambao hawapo kwenye mwatamio wa vimelea vya ugonjwa (muda ambao kuku anapata vimelea hadi dalili zinapojitokeza). Chanjo ina vimelea vya ugonjwa vilivyopunguzwa nguvu ya kusababisha ugonjwa. Endapo chanjo itatolewa kwa kuku wenye vimelea tayari, basi vitaongezea makali ya vimelea katika mwatamio na kuharakisha kujitokeza kwa ugonjwa na hatimaye kwa magonjwa yasiyo na tiba kuku atakufa. Hivyo, chanjo ni lazima itolewe kwa kuku wazima na kabla ya mwatamio.

Swali: Hata kama tukiwachanja kuku wetu dhidi ya Mdondo, bado kuna vifo vya kutisha kwa vifaranga na kuku wakati wakiwa na dalili za kuvimba macho hasa wakati wa kiangazi. Je, huu ni ugonjwa gani?

Jibu: Tatizo la vifo vingi vya vifaranga na vifaranga wakubwa baada ya kuvimba macho linatokea wakati wa kiangazi na mwanzoni mwa mvua kutokana na ukosefu vitamini na hususani vitamini A ambazo hupatikana katika majani mabichi. Ugonjwa huo wa upofu wa macho/kuvimba macho hujulikana kama Avitaminosis A (ukosefu wa vitamini A mwilini). Pia mbali na upungufu wa vitamin A magonjwa mengine muhimu katika kusababisha vifo vya kuku hata kama wamechanjwa kudhibiti mdondo ni wadudu wa ndani (minyoo), wadudu wa nje, ndui, kansa ya ini na mengine mengi.

Swali: Je ni ugonjwa gani unaoambatana na kutokwa kwa vipele/vidonda hasa sehemu za kichwa kwa kuku?

Jibu: Ugonjwa huo hujulikana kama ndui ya kuku (Fowl pox) na huathiri kuku wa rika zote, ijapokuwa wale wadogo huathirika zaidi na hata kufa kuliko wakubwa. Hata hivyo, ugonjwa huu haujitokezi kwa kuku waliopewa mchanganyiko wa vitamini zenye kiwango kikubwa cha vitamini A ambayo huimarisha ngozi. Vinginevyo, ugonjwa hukingwa kwa chanjo ya kuchoma kwenye mabawa ambao huhitaji utaalam.

Swali: Mara baada ya kuku kuanza kunya kinyesi chenye minyoo, hudhoofika na ghafla unaweza kumkuta kuku kafa bandani. Je tufanyeje ili kuepuka hasara kama hiyo?

Jibu: Minyoo ina tiba na dawa zinapatikana katika maduka ya dawa za mifugo. Mbali na kutibu kuku wenye minyoo mfugaji anaweza kuwa utaratibu wa kuwapatia kuku wake dawa za minyoo mara moja kila baada ya miezi mitatu.

Swali: Ni kwa nini kuku hunyonyoka manyoya?

Jibu: Kuku hunyonyoka manyoya kutokana na upungufu mkubwa wa protini kutokana na majani yenye protini kukauka, wadudu kuwa wachache wakati huo na upungufu wa vitamini A ambayo ni muhimu katika kuimarisha ngozi inayoshikilia manyoya.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

4 thoughts on “Maswali ya wafugaji wa kuku na majibu ya wataalamu

    1. Habari,
      Karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa swali lako. Mara nyingi kunaweza kusababishwa na mambo mengi, huenda ni ugonjwa wa mdondo, au upungufu wa Vitamin E na mengineyo hivyo ni muhimu kumtafuta mtaalamu wa mifugo aliye karibu na wewe kwa vipimo na uchunguzi zaidi. Lakini pia ni muhimu kumtenga kuku mgonjwa kwa muda ili kuzuia kuku wengine kuambukizana magonjwa.

Leave a Reply to Mkulima Mbunifu Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *