- Mifugo

Hifadhi Guatemala kwa malisho wakati wa kiangazi

Sambaza chapisho hili

Majani haya yanatumika kama chakula cha ziada kwa mifugo wakati wa kiangazi, hayatakiwi kutumika kama chakula kamili.

Majani aina ya Guatemala (Tripsacum andersonii) imesambaa kwa kiasi kikubwa katika ukanda wa tropiki. Aina hii ya majani inahitaji kiasi kikubwa cha mvua, au udongo wenye unyevu, lakini hata hivyo huweza kubaki yakiwa na kijani kibichi wakati wote wa kipindi cha kiangazi.

Nchini Tanzania, majani haya yanapatikana kwenye nyanda za kati, na sehemu zenye miinuko, hasa zenye rutuba ya kutosha kama vile kwenye safu za mlima Kilimanjaro, mlima Meru na Milima ya Usambara.

Mimea hii inakuwa kwa wingi, na inafaa zaidi kama chakula mbadala kinachotumika kwa ajili ya mifugo wakati wa kiangazi. Guatemala ina uvumilivu zaidi ya matete (nappier grass), lakini ni dhaifu katika uzalishaji na ina virutubisho vichache sana.

Kupanda

Guatemala hupandwa kutokana na vipande vya mashina, na huwa tayari kuvunwa baada ya miezi 4-6 tangu kupandwa. Hakikisha kuwa unapata mapandikizi kutoka kwenye chanzo kinachoaminika.

Unaweza kupanda kipande cha shina chenye pingili 3, au sehemu ya shina iliyoanza kuota kwa kulaza chini, kwenye sehemu yenye nafasi ya ½ mita x 1 mita. Inahitaji mbolea nyingi kwa ajili ya ukuaji mzuri.

Mseto

Guatemala inaweza kupandwa mseto na desmodium, leucaena, sesbania, au calliandra ili kuongeza mavuno ya malisho makavu yenye protini kwa wingi.

Mavuno na matumizi

Hekari moja ina uwezo wa kuzalisha Guatemala kiasi cha tani 9-22, yakiwa yamekatwa kiasi cha sentimita 10-25 kutoka kwenye usawa wa ardhi. Guatemala hasa hutumika kama akiba ya malisho ambayo hukatwa na kulishwa mifugo wakati wa kiangazi yakiwa mabichi.

Majani haya hutengeneza sileji yenye ubora wa wastani. Majani haya yanaweza pia kutumika kama uzio sehemu ya kuishi, au kwenye kontua kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa ardhi, matandazo shambani, au kwa ajili ya kukausha maji sehemu yenye tindiga. Inatumika pia kama kizuizi cha baadhi ya wadudu kwenye chai, kahawa na viazi.

Guatemala haiwezi kuvumilia kuchungia mifugo au kukatwa mara kwa mara. Haishauriwi kuchungia mifugo kwenye aina hii ya malisho. Inashauriwa kukata kwa uwiano wa siku 30 wakati wa mvua, na uwiano wa siku 42-45 wakati wa kiangazi. Ili kuepuka kuvimbiwa, inashauriwa kukata na kuacha majani haya yanyauke kabla ya kulishia mifugo.

Ubora wa virutubisho

Kwa kiasi kikubwa hii inategemeana na ukataji wa mara kwa mara, mashina yakikomaa yanakuwa na nyuzi nyingi na pia kuwa na kiasi kidogo cha protini na wanga kama hayakutunzwa na kuwekwa mbolea vizuri.

Wakati wa hatua tofauti za matumizi, kiasi cha protini pia hutofautiana.  Sehemu ya juu iliyokauka inakuwa na asilimia 6.4, sehemu ya juu ambayo ni mbichi inakuwa na asilimia 8.8, sehemu ya majani ambayo ni mabichi inakuwa na asilimia 6.1, shina linakuwa na asilimia 4.6.

Kiwango cha protini kinakuwa juu wakati wa wiki 3, na kuzidi kupungua kadri yanavyozidi kukomaa na nyuzi nyuzi kuongezeka. Majani yanakuwa na kiasi kikubwa cha madini aina ya manganese, chuma, zink na potashiamu.

Kutokana na kiasi kidogo cha protini kwenye aina hii ya malisho, malisho mbadala yenye kiasi kikubwa cha wanga na protini inafaa kutumika kwa pamoja na Guatemala kwa ukuaji mzuri wa mifugo.

Miongoni mwa vyanzo vya protini vilivyothibitishwa ni pamoja na vyakula vyenye mchanganyiko wa samaki, soya, aina hii ya malisho huwa na matokeo mazuri zaidi kuliko vyakula vinavyotokana na mashudu ya pamba, hasa kinapotolewa kwa kiwango cha kutosha pamoja na majani ya Guatemala.

Miti ya malisho

Guatemala inaweza kupandwa mseto na miti ya malisho. Kwa kufanya hivyo, mkulima anaweza kupunguza au kuondokana kabisa na matumizi ya virutubisho. Utafiti unaonesha kuwa kilo 3 za malisho yanayotokana na miti kama vile calliandra, leucaena, desmodium, viazi vitamu, haradali na aina nyingine za jamii ya mikunde zina virutubisho sawa na pumba aina ya diary meal. Mfugaji anaweza kupunguza gharama kwa kutumia aina hii ya malisho kwa ajili ya mifugo wake.

Ni muhimu kwa mkulima kufahamu kuwa ng’ombe wa maziwa wanahitaji mlo kamili wenye kutia nguvu, protini na vitamini. Mlo huo ni lazima uwe na wanga kiasi cha asilimia 75, Protini asilimia 24 na asilimia 1 ya madini.

Taarifa hii imeandaliwa kujibu swali lililoulizwa na kikundi cha wakulima cha MOWE kutoka Machame Mkoani Kilimanjaro.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *