Gliricidia ni mti ambao kisayansi hujulikana kwa jina la gliricidia sepium ambao hutumika kwa ajili ya mbolea au kurutubisha ardhi.
Mti huu wa gliricidia ni jamii ya miti ya malisho ambayo majani yake hutumika kurutubisha udongo na kulishia mifugo hasa katika kipindi cha ukame. Hii ni kutokana na uwezo wake wa kumudu kuzalisha wakati wa kiangazi pamoja na kudumisha hali yake ya ukijani wakati wote.
Maandalizi ya shamba
Shamba la kuotesha gliricidia liwe limeandaliwa mapema kwa kulima. Hii ni kwasababu uoteshaji wake mara nyingi hufanyika kwenye shamba la kuoteshea mahindi, au kuoteshwa kwenye kingo za shamba.
Uoteshaji
Miti ya gliricidia huweza kuoteshwa kwa kutumia vipandikizi au kwa kutumia miche ambayo tayari mbegu zilishasiwa.
Mbegu ya gliricidia husiwa kama mbegu zingine za miti katika makasha ya kusia mbegu. Huchukua miezi miwili mpaka mitatu toka kusiwa hadi kufikia kupelekwa shambani.
Wakati wa kuotesha gliricidia katika shamba la mahindi unahitaji kuotesha katika nafasi ya mita 5 upana na urefu wa mita 5. Hii itasaidia kuweka nafasi na uwiano wa kutosha kufanya kazi shambani na kuwepo kwa uzalishaji bora wa gliricidia na mahindi.
Utunzaji
Miti ya gliricidia ikishaota na kufikia urefu wa mita 5 kwenda juu, hakikisha unaanza kupogoa matawi ili kupunguza kivuli hasa inapokuwa imeoteshwa pamoja na mazao mengine.
Faida za miti ya gliricidia
- Miti ya gliricidia hutumika kurutubisha ardhi (kilo moja ya majani ya gliricidia ni sawa na kilo moja ya mbolea ya samadi).
- Majani ya miti ya gliricidia hutumika kama malisho kwa mifugo wakati wa njaa au ukame.
- Hutumika kufukuza panya kwani ganda la shina la gliricidia ni sumu. Jinsi ya kutumia: chukua ganda la shina na kuchemsha kwa nusu saa, kisha changanya na chakula wanachokipenda panya, kisha tega mahali panya wanakuepo.
- Hutumika kufukuza fuko shambani kwani fuko hawapendi harufu yake.
- Fito zake ni imara na mara nyingi hutumika kubebeshea mimea mbalimbali kama pilipili manga, vanilla na maharage.
- Miti hii huvumilia ukame hivyo husaidia kuwepo kwa kivuli shambani wakati wa kiangazi.
- Hutumika kuimarisha kingo na kusaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo hasa kipindi cha mvua.
- Miti hii huvumilia magonjwa na wadudu waharibifu hivyo kuondoa gharama za utunzaji.
- Fito zake hutumika pia kujengea uzio na hata kujengea vibanda vya kuku.
- Katika maeneo mengine duniani, maua ya mti wa gliricidia hutumika kama chakula hasa katika kipindi cha ukame.
Changamoto
- Miti ya gliricidia huwa na kivuli kikubwa hivyo inahitaji kupogoa mara kwa mara ili kuondoa kivuli, hasa ikiwa imeoteshwa sehemu yenye mimea isiyopenda kivuli.
- Wakulima wengi hawafahamu faida ya miti hii katika kilimo, hivyo kutokuipa kipaumbele kama moja ya aina ya miti ya kuotesha shambani.
- Miti hii pia huvutia wanyama kwenye mashamba wakati wa ukame. Hii ni kutokana na kuwa na ukijani wakati wote na kuonekana vyema hasa eneo linapokuwa limeoteshwa miti hii peke yake.
- Ikiwa gamba la shina lake ni sumu, basi si nzuri kutumia kuswakia hasa katika maeneo ya vijijini ambapo wakulima wengi hupenda kutumia vijiti vya miti mbalimbali kama mswaki.
Muhimu: Wakati wa kuotesha mahindi, ni vyema kutumia majani ya gliricidia kama inapatikana kwa wingi. Tumia majani yake ujazo wa viganja viwili vya mkono wako kuweka katika shimo kisha kufuatisha mbegu ya mahindi.
Majani haya ya grilicidia hutumika kama mbolea kwani huaoza haraka na kuweza kurutubisha udongo na hivyo kupata mahindi yenye afya.