- Mifugo

Fuata kanuni sahihi za kilimo upate mavuno bora

Sambaza chapisho hili

Wakulima walio wengi wamekuwa wakijikita zaidi katika matumizi ya mbolea    ili kupata matokeo mazuri katika kilimo,  na kusahau kuwa kanuni bora za uzalishaji pia huchangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka na kupatikana kwa mavuno yenye ubora.

Nini cha kuzingatia ili kupata mavuno bora

Ni lazima mkulima kufuata utaratibu wa uzalishaji wa mazao katika kila msimu wa kilimo. Hatua zifuatazo ni lazima zizingatiwe;

Fanya tathmini ya awali

Mkulima anahitajika kutafuta chanzo cha maji, kuchunguza wadudu na magonjwa katika eneo husika, kuchunguza magugu pamoja na aina ya mazao yaliyo jirani na shamba.

Pia, kujua gharama za uzalishaji hasa kiasi cha pesa kitakachotumika kumudu gharama za uzalishaji pamoja na uwepo wa kiasi cha mazao, ubora, muda, tarehe na sehemu ambayo mnunuzi atachukulia mazao.

Kuandaa shamba na kutenga muda wa kutosha kabla ya kupanda

Ili kufanikiwa katika uzalishaji, ni muhimu kuandaa udongo siku 30 hadi 45 kabla ya kupanda au kupandikiza miche. Hii itawezesha mambo yafuatayo;

  • Kuhakikisha hakuna magugu yoyote wakati wa kupandikiza miche ili kusaidia kudhibiti wadudu na magonjwa kabla ya kupanda zao jingine.
  • Kama magugu ni ndago, unashauriwa shamba liandaliwe siku 45 kabla ya kupanda au kupandikiza ili kupata muda wa kutosha kuondoa magugu hayo.
  • Maandalizi ya udongo yawe na uwiano na aina ya zao linalooteshwa na kama utatumia vifaa vya kukodisha, hakikisha ni safi ili kuzuia kuleta wadudu na magonjwa kwenye shamba lako kutoka mashamba mengine.

Kufunga na kufanya majaribio ya mfumo wa umwagiliaji

Hakikisha mfumo wa umwagiliaji uko sawa kwa kufunga na kujaribu pale inapobidi. Hii itasaidia pia katika udhibiti na utoaji wa magugu na kuiweka ardhi katika hali ya unyevu kwa ajili ya mazao yatakayooteshwa.

Kupanda uzio

Ni vyema ukapanda mazao ya uzio kama mtama au mahindi siku 25 hadi 40 kabla ya kupanda mazao yako.

Uzio unatakiwa kuwa na urefu wa sentimeta 30 hadi 40 wakati wa kupanda mazao ili uweze kufanya kazi ya kuzuia wadudu na virusi visivyotarajiwa. Ni vizuri pia kuupunguza uzio huo na kuutunza kama mazao mengine

Kusafisha kingo za shamba

Hakikisha umeondoa magugu yote yanayozunguka shamba lako ili kufanya wadudu wakose makazi na mazalia mpaka pale unapootesha mazao.

Kuondoa magugu ni hatua ya kwanza ya kuangamiza wadudu na magugu hivyo inashauriwa umbali wa mita 10 kuzunguka shamba kusiwe na magugu. Kadri umbali unavyokuwa mrefu ndivyo udhibiti wa wadudu na magugu unavyodhibitiwa ipasavyo.

Ni vyema pia kuweka vinasa wadudu siku 10 kabla ya kupanda ili kudhibiti wadudu.

Kupandikiza

Ratibu upandaji kwa muda muafaka. Usijaribu kupanda mbegu kabla hujaandaa matuta yako, uzio kupandwa, vinasa wadudu na mfumo wa umwagiliaji haujawa tayari.

  • Andaa udongo na uwe na unyevu wa kutosha kwa ajili ya kupandikiza Udongo uwe na mbolea ya kutosha
  • Tumia kipimo kuweka alama za kupandia zenye kipimo sawa kati ya mimea
  • Tumia mchanganyiko wa kuotesha ili kusaidia miche kwa ukubwa unaofanana. Miche iwe imenyooka na imara
  • Shindilia udongo kuondoa hewa wakati wa kupandikiza

Tambua wadudu na magonjwa

Utambuzi uanze siku moja baada ya kupandikiza na ufanyike mara mbili kwa wiki. Ikiwezekana, pima udongo wako maabara kabla ya kupanda na kupandikiza miche.

Tumiza madawa yanayoshauriwa wakati wa kupandikiza

Matumizi ya dawa za kuzuia fangasi wa udongo yafanyike wakati huu kwa kutumia Trichoderma sp kama haikutumika wakati wa kuotesha

Anza mipango lishe ya mimea katika mizizi

Weka mbole kwa kutumiaa mfumo wa umwagiliaji wa matone kama unatumia mfumo huo (fertigation).

Anza taratibu za umwagiliaji na lishe baada ya kunyima mimea maji

Anza kumwagilia na kuweka mbolea wakati mimea inaonekana kunyauka, hii ina maana mizizi ina uwezo wa kutumia mbolea iliyowekwa.

Tekeleza majukumu ya kawaida

  • Tumia fito (ikiwezekana ziwekwe dawa)
  • Rekebisha mipira ya kumwagilia
  • Dhibiti magugu
  • Ondoa mazao yote yaliyoshambuliwa na virusi.
  • Weka fito, fungia mimea kwenye fito
  • Punguza machipukizi
  • Kusanya na tokomeza mimea/matunda yaliyoshambuliwa na wadudu na magonjwa
  • Fuata taratibu za kuvuna, kuhifadhi mazao kabla ya kuuza au kutumia

Nyuki ni muhimu kwa mazao yanayohitaji

Kiasi cha mizinga itategemea aina ya mazao kwa mfano:

  • Jamii ya matikiti mizinga 7 kwa hekta na inahitajika kwa siku 15
  • Matango mzinga 6 hadi 8 kwa hekta kwa siku 30
  • Zuchini na Squash mizinga 5 hadi 6 kwa hekta kwa siku 30 hadi 45
  • Stroberi mizinga 6 hadi 8 kwa hekta kila mwezi, ambapo inaweza kuwa miezi 6 hadi 10

Ondoa masalia siku moja kabla ya kuvuna

Hii ni muhimu ili kuzuia kuwapa wadudu muda wa kuingia kwenye mazao, kuzaliana na kusambaza magonjwa kwa mazao mengine.

Wadudu hawa hubeba virusi na kuvihamishia kwenye magugu. Kuondoa mazao yote baada ya kumaliza kuvuna huzuia kusambaa kwa magonjwa.

Masalia ya mazao ni mazalia mazuri ya wadudu na magonjwa.

Matumizi ya dawa za wadudu kwa kiwango kikubwa yafanyike ili kupunguza idadi ya wadudu kabla ya kusafisha eneo.

 

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *