Magonjwa yaenezwayo na kupe yanasababisha zaidi ya asilimia sabini na mbili (72%) ya vifo vyote vya ng’ombe vinavyotokea kila mwaka. Magonjwa hayo ni Ndigana Kali (East Coast Fever – ECF), Ndigana Baridi (Anaplasmosis), Mkojo Mwekundu (Babesiosis) na Maji ya Moyo (Heartwater).
Aidha magonjwa hayo hulisababishia taifa hasara ya takribani shilingi za kitanzania bilioni mia nane na kumi na tano (815,000,000,000/=) kila mwaka. Pia takribani asilimia sabini (70%) ya ndama wanaozaliwa wanakufa kwa Ugonjwa wa Ndigana Kali. Hasara nyingine ni kupungua kwa uzalishaji, kushuka kwa thamani ya ngozi, kupoteza wanyama kazi na udumavu wa ndama.
Magonjwa yaenezwayo na kupe, mbung’o (mfano ugonjwa wa Ndorobo) na wadudu waumao hudhibitiwa kwa kutumia njia mbalimbali ambapo njia kuu ni matumizi ya dawa za kuua kupe kwa kuogesha mifugo kwa kutumia majosho, kunyunyiza au kupaka. Njia nyingine ni kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ndigana kali.
Dawa za kuogesha mifugo zimegawanyika katika makundi manne (4) ambayo ni Amitraz, Synthetic pyrethroids, Organophosphates na mchanganyiko wa Synthetic pyrethroids na Organophosphates. Ni vizuri kufahamu makundi haya ya dawa za kuogesha mifugo ili kudhibiti usugu wa kupe dhidi ya dawa hizi za kuogesha mifugo unaosababishwa na kutumia dawa ya kuogeshea mifugo ya kundi moja kwa muda mrefu.
Mfano wa dawa za kuogesha mifugo zilizopo katika kundi la Amitraz ni Norotraz, Twigatraz, Bamitraz, Alphatix, Tixfix n.k.
Mfano wa dawa za kuogesha mifugo zilizopo katika kundi la Synthetic pyrethroids ni Paranex, Albadip, Dominex, Tantic, Cybadip, Ectomin, Vectocid, Tantix, Ecotix n.k.
Mfano wa dawa za kuogesha mifugo zilizopo katika kundi la Organophosphates ni Steladone n.k.
Mfano wa dawa za kuogesha mifugo zilizopo katika kundi la Mchanganyiko wa Synthetic pyrethroids na Organophosphates ni DuoDip n.k.
Tunaposema dawa za kuogesha mifugo mfano Paranex, Albadip, Dominex, Tantic, Cybadip, Ectomin na Vectocid zipo katika kundi moja liitwalo Synthetic pyrethroids ina maana kwamba:-
• Dawa hizi zina kiambata kinachofanana kinachoua kupe
• Dawa hizi zina mfumo unaofanana wa kufanya kazi
• Kama dawa mojawapo katika hili kundi ikishindwa kuua kupe ina maana dawa zote katika hili kundi zitakuwa haziwezi kuua kupe
• Pale dawa ya kuogesha mifugo iliyopo katika kundi moja inaposhindwa kuua kupe kutokana na usugu wa kupe ni kosa kubadilisha dawa hiyo na dawa nyingine iliyopo katika kundi hilohilo.
Ili kudhibiti usugu wa kupe dhidi ya dawa za kuogesha mifugo ni vizuri mfugaji akawa anabadilisha dawa za kuogesha mifugo kwa kufuata mzunguko wa makundi haya manne ya dawa za kuogesha mifugo (Acaricide rotation).
Mfano mfugaji akitumia dawa ya kuogesha mifugo iliyopo katika kundi la Organophosphate, baada ya muda anatakiwa abadilishe dawa na kutumia dawa ya kuogesha mifugo ya kundi lingine mfano ya kundi la Synthetic pyrethroids.
Ni vizuri wafugaji kwa kushirikiana na wataalam wa mifugo waliopo katika maeneo yao kutambua aina ya kupe waliopo katika maeneo yao. Hii itafanyika kwa kuchukua sampuli ya kupe waliopo katika maeneo yao na kupeleka kwa wakala wa maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa ajili ya utambuzi. Jambo hili litasaidia:-
• Kujua aina ya kupe waliopo katika eneo husika
• Kujua ni kundi lipi la dawa za kuogeshea mifugo linaweza kuua kupe waliopo katika eneo husika
• Kujua mzunguko mzuri utakaotumia wakati wa kubadilisha makundi ya dawa za kuogesha mifugo (effective acaricides rotation)
• Kudhibiti vizuri kupe na kupunguza magonjwa yaenezwayo na kupe
• Kupunguza upotevu wa fedha
Faida za kutumia dawa za kuogesha mifugo kwa kuzingatia mzunguko wa makundi ya dawa za kuogesha mifugo (acaricide rotation) ni:-
• Kutokubadilisha dawa ya kuogesha mifugo kwa kuangalia jina la kibiashara la dawa.
• Inahakikisha kundi moja tu la dawa ya kuogesha mifugo linatumika kwa muda fulani wakati makundi mengine ya dawa za kuogesha mifugo yatatumika baadaye.
• Kupunguza usugu wa kupe dhidi ya dawa za kuogesha mifugo.
Mfugaji zingatia yafuatayo unapotumia dawa za kuogesha mifugo:-
• Dawa za kuogesha mifugo zilizopo katika kundi la Amitraz hazitumiki kuogesha farasi, punda na paka.
• Unapotumia dawa za kuogesha mifugo hakikisha umevaa vifaa kinga kama vile kiziba uso (masks), gloves, koti, buti n.k.
• Hakikisha dawa unayotumia imesajiliwa.
• Nawa mikono kwa maji na sabuni baada ya kutumia dawa ya kuogesha mifugo
Makala hii imeandaliwa na Dkt. Linus Prosper, toka halmashauri ya Arusha). Kwa mawasiliano zaidi piga namba 0756 663 247
Asanteeeni kwa kutuandalia makala hii wafugaji.
Habari
Karibu sana Mkulima Mbunifu. Tunafurahi kusikia kutoka kwako na kuwa makala tunayoandaa ni ya muhimu kwenu wafugaji na wakulima.
Karibu sana na usisite kuuliza tutakujibu ama kukusaidia namna ya kupata jibu la swali lako.
Ni dawa au dip gani inanguvu sana kutumika kuongeshea kwenye josho la ngo’mbe naomba jibu samahani lakini maana mm nimesha jalibu kila dawa lakini bado wateja wanalalamika naombeni msaada
Habari Bw. Michael
Karibu sana Mkulima Mbunifu. Samahani pia kwa kuchelewa kujibu swali lako nilikutana na changanmoto ya kimtandao kwenye tovuti yetu.
Kuhusu dawa, tafadhali wasiliana na Daktari wa mifugo toka Halmashauri ya wilaya ya Arusha Dk. Linus Prosper kwa simu namba 0756 663 297
Karibu sana
Halafu naomba mnisaidie kitu kimoja nitumie dawa gani zaidi
Kuna shida yoyote iwapo nitatumia aina 2 tofauti za dawa kwa wakati mmoja?
Namaanisha kuchanganya dawa za aina 2 tofauti kwenye josho kwa pamoja, mfano paranex na albadip n.k
Habari, Karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala zetu.
Kuhusu kuchanganya dawa haitakiwi kabisa, unatakiwa kutumia dawa moja ikiwa haijaonyesha ufanisi ndipo utumia dawa nyingine na usitumie dawa zinazotoka katika kundi moja kwa kubadilisha bali badilisha kwa kutumia dawa inayotokakatika kundi lingine
Ngo`mbe nitumie sabuni gani ili ngo`mbe wangu awe msafi?
Habari,
Hakuna sabuni ya kutumia kumsafisha ng’ombe. Kinachotakiwa ni kumuweka ng,ombe katika eneo safi na kulifanyia eneo hilo usafi wa mara kwa mara ng’ombe asilalie kinyesi chake wala mkojo