Kama ilivyo ada, Mkulima Mbunifu tumeendelea kuwatembelea wakulima na wanufaika wa jarida hili kufahamu ni kwa namna gani elimu wanayoipata kupitia makala za kila mwezi zimeendelea kuleta chachu katika shughuli zao za kilimo na hata kuweza kuwabadilisha kimaisha.
Bi. Esther Kitomari ni miongoni mwa wanufaika wa jarida la MkM na anaeleza kuwa amejifunza mengi kupitia makala zinazochapishwa kila mwezi hasa juu ya ufugaji wa kuku na ng’ombe pamoja na kilimo cha mbogamboga.
Bi. Esther anaeleza kuwa, ameweza kufanya shughuli zake za kilimo na ufugaji kwa ufanisi mkubwa, na kwa njia za kitaalamu zaidi kwa muda mfupi toka kuanza kusoma jarida la MkM. Pia elimu itolewayo kwenye jarida hili imemuwezesha kupunguza gharama za uzalishaji ambazo kabla ya kupata jarida hili zilikuwa za juu sana.
Alianza lini kusoma jarida la MkM
“Mimi nilikuwa mwajiriwa wa serikali lakini nilipostaafu niliamua kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji ambao hata nilipokuwa muajiriwa nilikuwa bado nafanya ila sasa nikaanza kuweka jitihada zaidi. Katika kuendeleza kazi za kilimo nilikutana na jarida la MkM mwaka 2020 na nikaendelea kulipokea na kulisoma na hadi sasa nimenufaika sana na elimu itolewayo na jarida hili”.
Nilikuwa nikikutana na changamoto mbalimbali katika ufugaji na kilimo. Mojawapo ya tatizo kubwa lililokuwa linanikabili ni la wadudu na magonjwa hasa kwa kuku na pia kukosa mbogamboga kwa ajili ya matumizi ya lishe ya kila siku’’.
Ninashukuru MkM kwa elimu waliyonipa kwani nimejifunza njia mbambali ya kuzuia magonjwa kwa mifugo yangu, kubwa zaidi ikiwa ni kwa kuzingatia usafi na kinga kwa wakati. Si hayo tu, lakini pia kupata dawa sahihi kwa ajili ya kutibu pindi magonjwa yanapokabili mifugo yangu”.
Aidha Bi. Esther anasema kuwa, amejifunza njia rahisi ya uzalishaji wa mbogamboga yaani kuwa na bustani ndogo ya nyumbani ambayo humuwezesha kuwa na mboga za kutumia na familia yake kila siku lakini zaidi ikiwa ni mboga salama iliyozalishwa na kukuzwa kwa njia ya asili bila kutumia kemikali.
Anasema kuwa, matumizi ya dawa za asili yana faida sana kiafya, kimazingira, kwa mimea na hata kwa wanyama lakini anaweza kutengeneza mwenyewe kwa kutumia malighafi zinazomzunguka.
“Unaweza kutumia dawa mbalimbali za asili kama vile majivu, mwarobaini, ndulele na mengine kutibu magonjwa ya kwenye mazao ya mbogamboga na dawa hizi zimeonyesha mafanikio makubwa sana shambani bila madhara yoyote’’ alisema.
Mbali na ufugaji wa kuku, ng’ombe pamoja na kilimo cha ndizi na mbogamboga, Bi. Esther anajishughulisha na utengenezaji wa vyungu kwa kushirikiana na mume wake. Vyungu hivi hutumika kupandia maua pamoja na vile vya kuweka mkaa kwa ajili ya kutumika kwenye chumba cha kukuzia vifaranga ili kutunza joto.
Wito kwa wakulima
Bi. Esther Kitomari anatoa wito kwa wakulima kujikita katika matumizi ya dawa na njia mbalimbali za asili katika kilimo na ufugaji ili kulinda afya za walaji na mazingira kwa ujumla na kuondokana na gharama zisizokuwa na msingi.
Pongezi kwa MkM
“Nawashukuru sana na kuwapongeza MkM kwani hatua niliyopiga kwasasa ni kubwa ukilinganisha na huko nyuma. Pia ninaomba watutafutie masoko ya bidhaa zetu za mifugo na kilimo’’.