Kwa mara nyingine tena, wakulima katika maeneo mbalimbali hapa nchini, wanapanda mazao na hata wengine kukazana kufanya palizi ili kutumia mvua ambazo zimenyesha sehemu mbalimbali. Mbali na kupanda mazao, shughuli nyingine muhimu ambayo wakulima wanaweza kujihusisha nayo katika msimu huu wa mvua ni upandaji wa miti.
Ni jukumu la kila mkulima kuhakikisha kuwa shamba lake lina miti mipya kila mwaka. Njia pekee na nzuri ya kufanya jambo hili ni mkulima kutenga sehemu ya shamba lake ambayo inaweza kupandwa miti kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Pia, miti inaweza kupandwa kwa kuzunguka mipaka ya shamba.
MkM limeandika mara kwa mara na kwa upana umuhimu wa miti inayosaidia kuongeza Nitrojeni kwenye udongo. Baadhi ya miti iliyozoeleka na inayofahamika zaidi kwa kazi hiyo ni pamoja na kaliandra, desmodiam, gliricidia, lusina na sesbania. Mingi ya aina hii ya miti ina mizizi inayoenda chini sana, jambo ambalo husaidia kupata nitrojeni kutoka kwenye tabaka la kati la udongo.
Majani yake ambayo hudondoka mara kwa mara, huboresha udongo kwa kuwa yana kiasi kikubwa cha Nitrojeni. Mizizi yake mikubwa husaidia kuimarisha udongo, na ukuaji wake wa kiasi kikubwa husaidia kuongeza maozo na kuimarisha upitishaji wa hewa kwenye udongo.