- Kilimo, Mazingira, Udongo

Jarida la MkM limetupa hamasa ya kutekeleza shughuli zetu za uzalishaji

Sambaza chapisho hili

Kuna msemo aliowahi kuutoa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa; “Elimu sio njia ya kuepuka umasikini bali ni njia ya kupigana na umasikini”. Msemo huu wameudhihirisha wazi na kwa vitendo wakulima wajasiriamali wa kikundi cha kusindika kitarasa ambao wametumia elimu inayotolewa na jarida la Mkulima Mbunifu kupiga vita umaskini na kufanikiwa.

Kikundi hiki kinachofanya shughuli mbalimbali za uzalishaji kama vile kilimo ikolojia, usindikaji hasa wa unga wa kitarasa, unga wa mbegu za maboga, pamoja na mafuta ya parachichi wameonyesha hamasa kubwa na kujivunia jarida la Mkulima Mbunifu.

“Huu ni mwaka wa tatu sasa toka tumeanza kupokea jarida la Mkulima Mbunifu, na kwa hakika tumefaidika kwa mengi kupitia elimu inayotolewa huko na kila mkulima ana kitu cha kukumbuka kupitia jarida hili’’. Alisema mwenyekiti wa kikundi hiki Bw. Antipas Shao.

Wakulima hawa wanasema kuwa, kupitia kusoma jarida la Mkulima Mbunifu, kila siku wanapata hamasa ya kuendelea kufanya shughuli za kilimo, ufugaji na ujasiriamali kwani pale wanaposoma na kujionea jinsi wengine walivyofanya na kufanikiwa, hakika wanapata moyo na kuzidi kufanya kazi zao kwa nguvu na kwa umoja.

Angelina Kimaro (M/Hazina wa kikundi) anasema kuwa, “jarida hili limekuwa chachu kwetu kwani linatufundisha mambo mengi yahusuyo kilimo na ufugaji pamoja na ujasiriamali na tumekuwa tukifanyia kwa vitendo yale tunayoyasoma na kwa hakika vimetuzalia matunda’’.

Naye Delfina Uromi anasema kuwa, kupitia jarida la Mkulima Mbunifu tumejifunza madhara ya sumukuvu na namna ya kujikinga nayo toka mazao yakiwa machanga, kitu ambacho hapo awali hatukuwa tunafahamu na tumekula sana sumu kuvu kupitia mazao mbalimbali kwani hatukuwa na uelewa.

Tumejifunza pia kuhusu gugu karoti, gugu ambalo hatukuwa tunafahamu kama ni sumu, tulilichukulia tu kama magugu mengine ya kawaida na hata mifugo ilikuwa ikila kama malisho, ila kwasasa tumefahamu madhara yake na namna ya kulidhibiti.

Aidha, tumejifunza kuhusu ufugaji wa kuku, magonjwa na namna ya kudhibiti na kuwapa kuku chanjo, lakini pia kuhusu mpera ambao utupatia matunda, faida za majani ya mpera na namna ya kutumia kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu. Alisema Delfina.

Naye Joyce Kimario aliongeza kuwa, kupitia jarida la Mkulima Mbunifu, nimejifunza kuhusu kilimo cha bamia, karoti na mbogamboga lakini pia nimeweza kuzalisha kwa kusoma na kufanya kwa vitendo.

Aidha, nimeweza kujifunza namna ya kuzalisha mbolea ya mboji, kutengeneza dawa za asili kwa kutumia malighafi mbalimbvali kama vile kitunguu saumu, pilipili, majani ya mpapai, sabuni na hivyo kuondokana na tatizo la magonjwa katika shamba langu.

Changamoto

Waswahili wanasema ‘’penye mafanikio hapakosi changamoto’’, hivyo pamoja na mafanikio wanakikundi hawa pia wanakutana na changamoto mbalimbali katika uzalishaji ambapo wameweza kubainisha na kuomba kama kuna namna wanaweza kusaidika katika kutatua.

Wanakikundi hawa wamesema kuwa, changamoto kubwa ni mabadiliko ya hali ya hewa, yaani kupungua kwa mvua au wakati mwingine kutokunyesha kwa wakati jambo ambalo linapelekea kushindwa kwa uzalishaji.

Aidha, ukosefu wa malisho, magonjwa mbalimbali ya mimea hasa ugonjwa ma migomba, magonjwa ya mlipuko kwa mifugo kama kuku pamoja na ukosefu wa masoko hasa wakati ambapo mavuno yanakuwa mengi kama uzalishaji wa ndizi.

Wito kwa Mkulima Mbunifu

Wakulima hawa wanaomba kuendelea kupokea majarida ya Mkulima Mbunifu na kuwezeshwa kwa njia zingine ikiwa ni Pamoja na elimu kwa vitendo ili kuweza kusonga mbele zaidi katika kujikumu kimaisha na kiuchumi kwa ujumla.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *